Showing posts with label Afya. Show all posts
Showing posts with label Afya. Show all posts

Saturday, 19 November 2022

SUALA LA UVAAJI MIKANDA KATIKA MAGARI LASISITIZWA ULAYA


Mara ya kwanza kuvaa mkanda katika gari ilikuwa nilipopewa lifti  na Mzungu mmoja miaka ya Sabini. Kipindi hicho tuliwaita weupe, walami. Sijui neno lilitokea wapi. Ila yupo jamaa aliyefasiri kuwa “mlami” ilitokana na “lami” yaani barabara safi, isiyo ya matope, makorongo, udongo au mchanga. Barabara iliyowekwa lami ikawa ya Kizungu zungu. Na enzi hizo, walami waliangaliwa kama watu walioendelea. Si tu kitabia pia kiteknolojia. Ukiwa na mlami, unaulizwa maswali. Kakupa nini? Kakupeleka wapi, mlami? Atakupeleka mtoni? Yaani, utofauti.


Sunday, 17 March 2019

MARADHI YA FIGO NA FAIDA ZA KUFUNGA KULA- 4



Maradhi ya figo yamezidi sana kwa watu weusi, seuze Watanzania.
 Majuma mawili yaliyopita tulimpoteza Mtanzania maarufu sana kwa ugonjwa huu. Ni muhimu kujadili kwanini figo linaendelea kuwa tatizo kubwa kwetu.
Makala tatu zilizopita zimeongelea ulaji wa Saladi, mazoezi na kufunga kama njia za kujali figo, ini, moyo, ubongo,nk. Tumeambiwa  matumizi HOLELA ya dawa za kuzuia maumivu  changia tatizo au pia fadhaa (“stress”) dhalilisha figo.
Wiki iliyopita tulikumbushana kuwa kufunga  si tu Ramadhani au Uislamu.Tulitazama faida zake ikiwepo kupunguza unene, maradhi, kuupumzisha mwili na uwezekano wa kuwa na maisha marefu.
Tulitazama aina ya kwanza ya ufungaji, yaani kunywa  maji ( kidogo kidogo kwa wastani wa saa 36-72).

Wednesday, 12 October 2016

VIPI TATIZO LA FIGO LAZIDI KUATHIRI AFYA ZA WAAFRIKA? - Sehemu 1



Tiba na afya za dunia yetu zimegawanyika sehemu mbili kuu.
 Magharibi ni uganga wa Kizungu unaotumia sayansi iliyofikia kilele karne ya 19 na 20. Moja ya nguzo zake kuu ni kutibu kwa kunyamazisha- kupitia sindano, dawa na upasuaji. Tiba ya Kizungu ndiyo inayotawala dunia yetu na ndiyo mara nyingi Wabongo wanaojiweza wakiugua siku hizi husafrishwa nje  kutibiwa.
Tiba za mashariki zinaongozwa na ustaarabu wa Kihindi na Kichina. Wahindi hutumia mwenendo uitwao Ayurveda. Tiba hii yenye zaidi ya miaka elfu mbili huangalia mwili mzima ukoje kabla ya kuushughulikia. Wachina wanao pia mtindo huo huo, unaotazama mtiririko wa nguvu mwilini badala ya dosari. Utaratibu wa Kichina na Kihindi kijumla hautibu tatizo moja kama  Wakizungu. Kwa wazungu mathalani ukiumwa kichwa utapewa dawa ya kuyaondoa maumivu hayo.

Tuesday, 7 June 2016

WIMBI KUBWA LA MATUMIZI YA NAZI NA MADAFU MAJUU







Zamani wakati nikikua tuliambiwa ukinywa  madafu utaota busha. Njoo sasa katika nazi na mapishi yake. Watoto wa kiume tulibezwa tulipokuna nazi. Nakumbuka enzi nikiishi kikapera Mwananyamala , Dar es Salaam nilitembelewa na dada fulani. Alipogonga mlango akanikuta nimekaa juu ya mbuzi nikikuna nazi hakustahimili.
“Freddy hebu uko...pisha nikusaidie.”
Ilikuwa miaka 40 iliyopita. Sina hakika kama leo mambo yamebadilika.

Sunday, 7 June 2015

WAZUNGU WANAREJEA MAMBO YALIYOKUWA ASILIA YA WAAFRIKA ZAMANI



Mwafrika mwenzangu umegundua nini jipya miaka ya karibuni?
Ukichunguza utaona maradhi yaliyokuwa yakiwang’ong’a  wazee, leo yanaua vijana. Ugonjwa wa moyo, utasa, mapafu dhaifu, uume tata,  uchovu kila mara bila sababu, kisukari, chafya upitapo kwenye vumbi, magari au moshi wa sigara; kiharusi, nk. Maumbile na mazingira yana sheria kali sana. Tusipoyaheshimu hutufunza adabu. Je, kweli tunayaona? Maana sikio la kufa halisikii dawa...
Matokeo nini?

Thursday, 4 December 2014

WATANZANIA TUJIFUNZE KUWEKA AFYA MIKONONI, TUSISUBIRI KUDRA YA WAKUBWA AU MUNGU





 Miaka yote niliyosafiri na kuishi ughaibuni nimebaini siri moja  kuhusu afya. Wananchi wengi duniani hawaijali miili hadi wanapougua.  Zamani kidogo nilikuwa nikiongea na mganga wangu wa Kichina. Nilikwenda kuchomwa zile sindano zao zinazobandikwa sehemu mbalimbali mwilini na kuachwa zimesimama juu ya ngozi mithili ya mishale ya nungu nungu. Accupuncture (tamka “Akapan-kcha”), ndiyo jina lake la kitaalamu. Tiba hii iligunduliwa, kutafitiwa na kuendelezwa maelfu ya miaka kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo na Mtume Muhammad SAW.   Kazi ya sindano hizi  ni kurekebisha na kusawazisha nguvu (au umeme) mwilini. Unapochomwa tatizo si maumivu. Haziumi kama sindano za Kizungu tulizozoea. Kinachochachafya ni vile Mchina anavyotafuta “njia sahihi.” Je, umewahi kushika waya wenye umeme? Unaukumbuka ule mstuko? Ukiwa mdogo, ndivyo  Accupuncture ilivyo. 
 Sindano za Kichina. Picha ya Mtandaoni
 

Sunday, 21 April 2013

WATU WEUSI TWAKUMBUSHWA MADHARA YA ULAJI CHUMVI NYINGI



Ladha ni kitu muhimu sana.

Siku moja nilikuwa nimealikwa karamu fulani kubwa- mwenyeji ni Mzungu aliyemwoa bibi wa Kiafrika. Kufumba na kufumbua dada mmoja, (sikumbuki taifa lake, lakini alikuwa Mwafrika)-hakuwa na raha hata kidogo na misosi. Kawaida ukialikwa hizi karamu za kimataifa, si mara zote utakuta vyakula vya kwenu; ulivyozoea. Mathalan, Wazungu wanavyokula ni tofauti sana na sisi. Hutumia vitu ambavyo si mazoea yetu mfano jibini (chizi), kachumbari nzito (“mayonnaise”) yenye mayai, siki, mafuta, malai (“cream”), nk. Au kuna suala la nyama.

Siku hizi idadi ya wasiopenda nyama jamii zilizoendelea imekua kubwa kiasi ambacho ukihudhuria mikutano au makongamano ya kimataifa unaulizwa (kabla) je mlaji nyama au hapana.Basi dada hakua na raha.Meza zilijazana vyakula vya wanga, mboga, nyama na protini. Dada alilalamika ladha.


Sunday, 28 August 2011

KIFO CHA MWANAMUZIKI AMY WINEHOUSE NA FUNDISHO KWETU BONGO

Moja ya nyumba zilizoporwa wakati wa ghasia mjini London majuma mawili yaliyopita ni ya  mwanamuziki maarufu wa Kiingereza , Amy Winehouse aliyefariki mwezi Julai.
Ingawa uchunguzi wa nini hasa kilichomuua ungali ukiendelea hadi Oktoba, Amy Winehouse alifahamika kuwa mchapa pombe kali na dawa za kulevya wakati wa maisha yake mafupi ya miaka 27.
Mwanamuziki huyu Myahudi alikuja juu 2003 kutokana na kipaji chake cha sauti nzito ya kupendeza juu ya utenzi wa maneno  aliyoyaandika kwa ustadi sana.
Akiwa shuleni alifukuzwa sababu ya tabia ya bashasha, kutosikiliza aliloambiwa, kutoboa pua. Aliimba kila mara darasani akawakera waalimu. Ingawa hakuwa bado mlevi ufundi  wake wa muziki (alipiga pia gitaa) ulimpatia nafasi ndani ya vyuo mbalimbali vya sanaa ikiwepo Sylvia Young Theatre School.


Amy akiwa na babake Mitch Winehouse. Picha  Shaun Curry wa Getty Images.
<--more--!>

Wednesday, 27 April 2011

VIPI KISUKARI KINAWAUA WATANZANIA MAARUFU?

Habari kuhusu tiba ya Loliondo zimezigusa hisia za Watanzania wengi. Huku nje suala la mzee Mchungaji Ambilikile Mwasapile; halijafahamika vizuri. Wanahabari wachache tumefuatilia mambo ya “mti wa Loliondo” mitandaoni lakini si jambo la jazba kama nyumbani.  Suala lolote linalowasaidia wanadamu kuondokana na matatizo yao ya kimaisha huwa na umuhimu katika jamii. Loliondo imewika kutokana na afya zetu kuzidi kuwa mbaya. 
Waafrika tunatafuta majibu ya haraka.

Waingereza hutumia neno “Quick Fix” kuelezea ufafanuzi wa kupinda kona. Wabrazili husema “um jeitinho” (tamka, jeichinyo) kufumbua matatizo upesi upesi. Ni kama mtu huna hela ya chai ukala kiporo. Wachagga tuna chakula kinaitwa “Ikato”  (mseto wa maharage na ndizi);  badala ya mkate au maandazi.
<--more!-->

Monday, 7 February 2011

HAJA NDOGO NJE KWA WANAWAKE SI JAMBO RAHISI...

Tupo sebuleni kwa jirani yangu mmoja mwanamke. Katualika majirani kusherehekea siku ya kuzaliwa miaka themanini. Themanini nakwambia! Wanawe wawili wamewasili na wajukuu na vitukuu toka Australia na Afrika Kusini kushangilia siku hii maalum ya ajuza mcheshi, roho safi; kibibi anayependwa na kila mtu hapa mtaani ninapoishi London. Nyumba imetota baraka. Harufu mbalimbali za makulaji zinazitesa pua. Vyakula vimetandazwa mezani. Viazi Ulaya vya kuchemsha na kuoka vinavyotengeneza msosi maarufu uliovum buliwa na hawa hawa Waingereza unaojulikana kama Chips. Mboga mbichi safi za saladi, nyanya, matango, vitunguu, jibini (chizi), mikate ya kila sampuli, samaki na kuku wa kukaanga. Kawaida karamu za Majuu hutenganisha walaji wa nyama na wasiokula nyama (Vegetarians).

Sunday, 30 January 2011

MTINDO WA KISASA WA NYWELE UNAHARIBU AFYA ZA WANAWAKE WEUSI

Watu wa kabila la Chwi kule Ghana wanaozungumza lugha iitwayo Tshi wana methali kuhusu umuhimu wa kupendeza. Inashauri: “Ikiwa mwenda wazimu ataiba nguo zako na kukimbia nazo wakati wewe uko majini unaoga, itakuwa vyema utafute angalau kipande cha kitambaa ujifunge wakati unamkimbiza maana usipofanya vile watazamaji watadhani na wewe umeheuka.”
Hakuna mwanaume ambaye hajawahi kupayukiwa kuwa asuburi wakati ndugu yake wa kike anajipodoa akijiremba. Na kati ya mapambo yote nywele zinaongoza foleni. Mwanaume waweza kutoka bila kuchana nywele, unaweza ukawa nusu kipara (kama mimi mwandishi) lakini hujali mradi u msafi utatoka zako mitaani. Kwa mwanamke kujisanifu nywele ni tendo muhimu sana. Ndiyo maana waandishi mbalimbali wa hadithi hawakosi maelezo ya ususi ndani ya riwaya zao.

Sunday, 9 January 2011

KUJIENDELEZA, MAZOEZI NA KUINUA VYUMA -Sehemu ya Mwisho

Makala kadhaa zilizopita zimesisitiza sisi wananchi wenyewe kujiendeleza. Lengo la insha hizi ni kukumbusha wewe mwananchi kwamba huwezi kusonga mbele bila elimu na maarifa sahihi; kwamba maendeleo yanawezekana.
Jamii ya Marekani imejenga utamaduni huu uitwao Self Help. Ni utamaduni uliozalisha biashara ya vitabu, video, magazeti na vipindi mbalimbali vya runinga vinavyosisitiza mwananchi kujituma badala ya kutegemea uchawi, dini au imani nyingine peke yake. Lengo ni kuweka nguvu za kimaendeleo mikononi mwa mwanadamu. Kelele inayopigwa ndani ya utamaduni wa Kimarekani ni kuwa lolote linawezekana kwa anayejitahidi.

Monday, 27 December 2010

SUALA LA MAZOEZI YA UINUAJI VYUMA KWA WABONGO

Baada ya kuandika kuhusu maradhi ya moyo na kichomi yanavyodhalilisha vijana leo, mwezi Novemba, Watanzania wengi waliniandikia kutaka ufafanuzi kuhusu mazoezi na uinuaji vyuma. Mazoezi na uinuaji vyuma ni mada muhimu sana.
Suala la kwanza ambalo pia limeenea barani Afrika ni kwamba kazi ngumu (sulubu) ni sawa na mazoezi. Eti kama mtu anatembea kwenda kazini au anayo maisha ya taabu yanayoutoa mwili jasho kila siku basi hilo ni zoezi tosha.