Tuesday 7 June 2016

WIMBI KUBWA LA MATUMIZI YA NAZI NA MADAFU MAJUU







Zamani wakati nikikua tuliambiwa ukinywa  madafu utaota busha. Njoo sasa katika nazi na mapishi yake. Watoto wa kiume tulibezwa tulipokuna nazi. Nakumbuka enzi nikiishi kikapera Mwananyamala , Dar es Salaam nilitembelewa na dada fulani. Alipogonga mlango akanikuta nimekaa juu ya mbuzi nikikuna nazi hakustahimili.
“Freddy hebu uko...pisha nikusaidie.”
Ilikuwa miaka 40 iliyopita. Sina hakika kama leo mambo yamebadilika.


Tukirudi katika madafu.
Nilipokuwa likizo nyumbani karibuni ilikuwa kazi sana kupata madafu mitaa ya Dar es Salaam. Wakwezi walilalamika nazi hazipatikani. Miti imekatwa katwa. Ilibidi tuvuke Kigamboni kupata nazi. Mji Mwema na kadhalika.
Ukija kwa watu wa mikoani ; madafu ndiyo hayajazoeleka. Nimekutana na Waafrika wanaotoka kanda zisizo na bahari kama Rwanda, Zambia na Zimbabwe. Madafu si mazoea wala kinywaji wanachokienzi.
Si kweli , la hasha.  Madafu hayaleti busha. Busha ni maradhi yanayosababishwa na kirusi kupitia mbu. Kirusi hiki kinachoitwa “filarial” ni aina ya nyungunyungu au mchango. Husambaa na madhara yake, tunaelezwa, hayana tofauti sana na tegu, malaria, nk.
Uzushi na kutojua ndiyo unaotudanganya eti tukila madafu tutavimba miguu au mbegu kuu za uume. Si masihara miaka 50 iliyopita wengi wetu tuliogopa kula madafu tukihofia kupata “mshipa” kama ilivyosemwa kwa lugha isiyo ya kitafiti au kisayansi.
Sasa tukirejea kwenye nazi yenyewe.
Waafrika Mashariki tumezoea nazi kwa mawili. Mafuta ya kujipaka, kupika au tui la kupikia. Nadra sana kumkuta mwananchi wa sehemu hizi akila nazi. Madafu ndiyo , lakini kula nazi mh mmh....

Njoo Ulaya kesho Jumatatu.
Miaka 30 iliyopita Wazungu wameanza kuona na kutambua madhara ya teknolojia na mashine. Vyakula vingi vinavyotengenezwa kwa mashine au kutumia “kilimo cha haraka” - vimegundulika kutojenga ama kutostawisha  mwili. Mifugo inayokuuzwa upesi upesi ili kuuzwa na kufikia lukuki imeanza kukataliwa baada ya wanancchi kugundua madhara yake. Chukua nyama ya kuku na mayai, kwa mfano.
Kuku wa Kizungu zamani alifugwa nje, akaruhusiwa kukimbia kimbia kama ndege yeyote mwingine asiyeruka hewani, mfano bata, bata mzinga, tausi, nk. Miaka ya karibuni kutokana na biashara, ubepari na tamaa wafanyabiashara hufuga ndege ndani ya majumba maalum. Huwanyima mwangaza na jua asilia. Huwachoma sindano na kuwanywesha dawa wakue haraka. Miaka kumi iliyopita kuna kipindi kilifanywa na runinga maarufu ya BBC kikiongelea kuku “ eti wa kisasa” anayefugwa kuanzia kifaranga akawa tayari baada ya majuma matatu. Kuku huyu hana tofauti na picha fulani au mchezo wa kuigiza. Mzuri, mkubwa, mzito, mnene. Malezi yake ni jela. Haruhusiwi kucheza cheza na kuwa kiasilia. Hukua haraka ndiyo lakini akiteseka. Hukaa pale pale alipozaliwa akijinyea, akila, akiimba, akilala;  hapo hapo.
 Kipindi hicho cha BBC kilionya ukitaka kujua ndege kateseka, angalia magoti yake utaona rangi na madoa meusi. Damu itakuwa imesinyaa. Huwa  ndege huyu si mtamu hata kidogo.
Kinachomfanya ndege aina hii wawe watamu ni vikolezo. Chumvi. Pilipili. Mafuta. Na kadhalika. Yote haya huchangia maradhi kwetu walaji. Ugonjwa wa moyo. Ngozi. Utasa.  Matokeo wananchi wengi hapa ama hawali kabisa  nyama au kama wakinunua...lazima maduka maalum wa kuku waliokuzwa “kienyeji” walioruhusiwa kutembea nje na kula wadudu kama ndege anavyotakiwa kuwa kiasilia.
Maskini tu ndiyo  hula nyama hizi za ndege aliyeteswa. Maana bei rahisi. Hata kuku wanaosemekana ni “Halal” huwa hao hao.  Na wageni wanaofika toka nchi mbalimbali maskini hununua haraka haraka bila kuchunguza. Tatizo limezagaa na kufahamika Uzunguni.
 Kwetu Afrika wananchi wanaanza kukataa kufuga kuku kidesturi. Kuku  wa kienyeji siku hizi hawaliwi. Waafrika tunaanza kuiga Uzungu ulioshakataliwa. Matokeo tunaanza na sisi kupata maradhi ya Kizungu. Saratani. Kukohoa ovyo. Mafua na vikohozi vya ajabu ajabu. Maradhi ya ngozi, nk.
Ndiyo sababu sasa Wazungu wanatafuta sana vyakula asilia. Ilianza Aloe Vera.  Ishazoeleka.  Yakaja matunda kama mapapai, maparachichi, maboga, nyanya nk. Karibuni limeingia wimbi la mbuyu na nazi. Mbuyu bado haujajizatiti sana. Lakini nazi? Kuna sabuni za kila aina za kuoga na kufulia, mafuta ya kujipaka na kuosha nywele (“shampoo”) na kupika; dawa za mswaki, juisi na keki, pombe, mvinyo; ili mradi kila kitu sasa hivi maduka ya afya ni nazi, nazi, nazi. Coconut. Tena aghali sana. Vipindi lukuki mitandaoni na runinga vinatathmini manufaa ya nazi.
Kinga maradhi (kama yalivyo maparachichi, Alove vera, mbuyu nk), kuzuia kukatika nywele, kucha,  kubabuka ngozi na kupunguza unene. Tuzungumzie unene. Miaka michache iliyopita nazi ilikuwa ikipigwa vita kwa sababu ina mafuta. Lakini karibuni utafiti umegundua kuwa mafuta yaliyoko katika nazi hayadhuru. Ni kama yaliyomo katika mbegu. Korosho. Karanga. Mbozi. Mbegu za maboga, nk Mafuta asilia. Hupunguza  unene au “cholesterol” – kwa lugha ya kitaalamu
Uchunguzi mmoja uliofanywa kupitia wanawake 40 na wanaume 20 wanene sana ulikubali kuwa walipungua kiasi kikubwa baada ya kulishwa mafuta ya nazi kwa majuma manne. 
Juzi hapa nilikuwa nikitazama kipindi cha jamaa aliyeshaandika kitabu kinachozungumzia faida 99 za nazi. Tisini na tisa! Kati ya faida hizo nikusukutua. Anadai ukisukutua kwa nazi unaua virusi mdomoni.
Kingine jamaa alichosema ni kuimarisha kazi ya ubongo na kichwa. Tunafahamu kadri tunavyozeeka ndivyo kadri mwili na viungo huzeeka. Sasa uzuri wa nazi uko hapo. Mafuta  na ule weupe weupe wake una kitu kinachoitwa “ketone” ambacho mbali na kukupa nguvu kinaimarisha uwezo wa kufikiri na kupunguza kudhalilika kwa ubongo.
Utafiti umeonesha (na kudhihirisha) kuwa wakazi wa visiwa vya bahari ya Pacific (Fiji) huwa hawana matatizoya  kupotewa na akili au kumbukumbu (Alzheimers Disease) kwa vile  asilimia 90 ya mlo wao ni  nazi.  

Afya yako msomaji inakutegemea wewe mwenyewe. Kama ulidharau nazi au madafu; ukidai huleta busha au ni chakula cha Waswahili wa pwani wasiosoma, achana na mawazo hayo finyu. Nazi ni muhimu sana katika maisha yetu.
Tusisubiri wenzetu nchi zilizoendelea watukumbushe kila mara kuwa tulicho nacho Afrika  ni cha thamani sana.
Tuache ulimbukeni wa kuiga na kula vyakula duni na nyama zinazotudhuru tukidhani hayo ndiyo maendeleo.

Ilichapwa Mwananchi Jumapili, 29 Mei , 2016.

No comments:

Post a Comment