Tuesday, 10 September 2013

MTINDO WA KISASA WA NYWELE UNAHARIBU AFYA ZA WANAWAKE WEUSI


Watu wa kabila la Chwi kule Ghana wanaozungumza lugha iitwayo Tshi wana methali kuhusu umuhimu wa kupendeza. Inashauri: “Ikiwa mwenda wazimu ataiba nguo zako na kukimbia nazo wakati wewe uko majini unaoga, itakuwa vyema utafute angalau kipande cha kitambaa ujifunge  wakati unamkimbiza maana usipofanya vile watazamaji watadhani na wewe umeheuka.”
Hakuna mwanaume ambaye hajawahi kupayukiwa kuwa asuburi wakati ndugu yake wa kike anajipodoa akijiremba. Na kati ya mapambo yote nywele zinaongoza foleni. Mwanaume waweza kutoka bila kuchana nywele, unaweza ukawa nusu kipara (kama mimi mwandishi) lakini hujali mradi u msafi utatoka zako mitaani. Kwa mwanamke kujisanifu nywele ni tendo muhimu sana. Ndiyo maana waandishi mbalimbali wa hadithi hawakosi maelezo ya ususi ndani ya riwaya zao.