Sunday, 7 June 2015

WAZUNGU WANAREJEA MAMBO YALIYOKUWA ASILIA YA WAAFRIKA ZAMANI



Mwafrika mwenzangu umegundua nini jipya miaka ya karibuni?
Ukichunguza utaona maradhi yaliyokuwa yakiwang’ong’a  wazee, leo yanaua vijana. Ugonjwa wa moyo, utasa, mapafu dhaifu, uume tata,  uchovu kila mara bila sababu, kisukari, chafya upitapo kwenye vumbi, magari au moshi wa sigara; kiharusi, nk. Maumbile na mazingira yana sheria kali sana. Tusipoyaheshimu hutufunza adabu. Je, kweli tunayaona? Maana sikio la kufa halisikii dawa...
Matokeo nini?


 Leo tumejenga tabia ya lawama kwa wengine kuhusu matatizo yetu. Hatuisikilizi miili yetu. Wanyama tu ndiyo bado wanaheshimu maumbile. Siku Tsunami kubwa la mwaka 2004 lilipoutingisha ukanda mzima wa nchi za bahari ya Hindi, wanyama wengi walikimbilia milimani au nyanda za juu kujiokoa. Wanadamu wasiojali wala kuhisi tena maumbile walibaki kama vigogo (vyenye kiburi cha teknolojia) wakisubiri kiama kiwakute. Tumepoteza hisia asilia tulizozawadiwa na Mwenyezi Mungu.
Madhila yetu wanadamu yametokana na sisi wenyewe kutokubali nguvu tulizo nazo. Imezuka desturi ya wahubiri  kuzusha eti huu mwisho wa dunia. Ukweli haya yamesikika kila karne. Hakuna kipindi chochote cha historia  ambapo sisi wanadamu hatukupiga kelele kuwa tamati ya sayari yetu inawadia. Hutokana na kushindwa kujua au kuona kiini cha matatizo yetu. Tunaposhindwa kuelewa tunabaki “kuotea” alamsiki ya kila kitu, kukata tamaa na uhai.
Kila karne ina matatizo na raha zake.
Starehe ya karne ya 21 ni kukua kwa  teknolojia ya habari na mawasiliano.  Shida ni namna teknolojia hii inavyotumika.  Siku hizi pamezuka majambazi wa mtandaoni (“hackers”) wanaotumia msitu huu ( wa raha) kuhujumu. Siku chache zilizopita, mathalan, shirika la upelelezi Marekani, FBI, lilitangaza lilivyomtia mbaroni mjuzi wa usalama wa kompyuta , Bw Chris Roberts.  Bw Roberts alitumia tarakilishi yake kuingilia mitambo  ya ndege na kuipaaza kiupande upande mapema mwaka huu. Alishawahi pia kuingilia ndege kadhaa kati ya 2011 na 2014.
 Mwezi jana magaidi wa Mashariki ya Kati waliingilia moja ya idhaa za televisheni za Ufaransa (TV5 Monde) na kuiteka (kupitia kompyuta) kwa siku kadhaa.
Lazima tuwe macho na majambazi wanaotumia ujanja huu kutuhadaa. Eti tumeshinda bahati nasibu na mamilioni ya fedha . Nadhani msomaji unayetumia barua pepe umewahi kupokea nyaraka hizo. Teknolojia hii nzima imeanzia kwa Mzungu. Na hapo hapo...
Iko chuki inayozagaa Afrika kwamba kutoendelea kwetu ni kosa la Mzungu. Hatukatai Wazungu wameua wanadamu wengi sana kwa miaka 500 sasa. Wiki iliyopita safu hii ilizungumzia ustaarabu wa demokrasia ya Wazungu; lakini hawa hawa Wazungu walikuwa wakichinjana  wakati wa vita vyao vikuu vilivyokwisha mwezi Mei 1945 na kusababisha vifo milioni 80.  Leo Wazungu wamejifunza. Mtoto mdogo huwa haogopi kijinga cha moto hadi kinapomchoma. Waafrika tuliteswa na utumwa. Hadi leo makovu yapo. Waafrika tunapitia majanga yaliyokwisha kwaruzwa  na Wazungu. Bado tunalaumu, bado tumeathirika; wengine tuna vinyongo...
Vinyongo vimetuelemea; tumejaa maluwe luwe; hatuoni, hatutathmini sawasawa. Tunasahau ukweli mmoja, lakini.
Siyo sisi tu tulioteswa au kutawaliwa. Kila taifa lina historia ya kunyanyaswa. Wachina walitawaliwa na Wajapani; Waingereza walitawaliwa na Warumi ( Italia); Waarabu walitawaliwa na Waturuki; Wahindi walitawaliwa na Waingereza, nk.
Usiku mmoja miaka zaidi ya ishirini iliyopita, nilikaa na kundi la Wazungu baada ya kuwatumbuizia ngoma.
“Vipi Tanzania?” Wakaniuliza.
“Kwema tu.”
“Kwanini ulihama?”
“Kutafuta maisha.”
“Nimewahi kufika Tanzania. Kuzuri. Wenyeji wema sana.”
“Kweli.”
“Mbona unaishi huku? Baridi kali...”
“Mbona Tanzania pia kuna wenzenu, wamehamia, wanapahusudu? Kila mtu anaruhusiwa kwenda atakako.”
“Lakini ni vigumu zaidi kwenu Waafrika  kuishi hizi nchi zetu.”
Gumzo likaendelea. Ghafla nikawachamba.
“Nyinyi lakini mna dhambi sana. Mmesababisha vita kila mahali. Ukoloni, ukoloni mambo leo, uporaji mali...”
Mwanamke mmoja wa makamo, nywele ndefu, nyeupe kama sungura,  sigara mkononi; akatingisha kichwa.
“Unajua huu ukoloni, ukiuchunguza ulikuwa ni sera tu ya watawala. Uingereza ni jamii ya matabaka. Walioshika madaraka walikuwa wanaume wachache waliotoka familia za kitajiri. Hata  wanasiasa wa sasa ni milionea wachache. Humwoni rais au waziri mkuu yeyote duniani  maskini...”
Nikanyamaza. Ukipewa somo kubali. Mwanamke wa Kizungu akasambaza moshi wa sigara lake.
“Huu ukoloni ulikuwa siasa ya wachache. Wachache hao waliohodhi dhahabu, farasi, bunduki, majambia na meli ndiyo walioamua  kila kitu. Wachache hawa hawa walikwenda zao nje wakapora makoloni, wakatwaa ardhi za wengine, wakaua, wakaiba madini. Sisi wanawake tulifuata tu mkumbo. Enzi hizo wanawake tulifanya kila mwanaume alichosema. Ukombozi wa kina mama hauna zaidi ya miaka 30. Maskini hawakuwa na la kusema. Ukoloni si Uzungu. Ulikuwa uamuzi wa tabaka dogo la waliojiweza.”
Kimya kikatua pale.  Nikabaki nikitafakari. Iko siku nilikuwa warsha fulani ya lugha, hapa London. Waafrika hupandwa sana na jazba kuhusu mada hii. Ukaanza mjadala kuhusu lugha za Kiingereza na Kifaransa zinazotumika zaidi barani. Kwamba ni lugha za kikoloni. Baada ya malumbano makali tukakubaliana kuwa lugha haina kabila au rangi. Lugha ni chombo tu cha anayeitumia.
Wenzetu Wachina, Wajapani, Wahindi na wengine bara Asia wameshaachana na lawama. Wameachana na vinyongo kiasi ambacho Wazungu sasa wanajiuliza mbinu za kukabiliana nao kiuchumi. Hii ni kwa vile wenzetu ni wachapa kazi. Hawapotezi tena muda kupiga domo. Sisi bado tunawashtaki kunguru, mwewe na yange yange, walioshapaa zao.
Juu ya lawama tumeyaacha ya kwetu tunaiga ya wengine. Mosi kabisa, tumbo. Chakula kinachopendwa na wengi siku hizi si tena ubwabwa, ugali, ndizi au chapati ila viazi Ulaya vya kukaanga. Asili yake ni hawa hawa  wakoloni wetu. Waingereza. Chips kwa samaki. Chips kwa kuku. Mafuta yaliyoko vyakula visivyo vya asili yetu yanatuvimbishia vitambi na unene unaotuumiza kwa visukari na viharusi.
Wazungu waliotuletea teknolojia  wameshagundua dhila lake. Wanarejea siri ya maumbile. Leo Ulaya na Marekani utakuta vyakula vingi vilivyojazana Afrika  vinauzwa aghali maduka  ya afya. Viazi vitamu, madafu,  maparichichi, komamanga, mibuyu, Alo Vera, upupu, nk. Mzungu anatafuta bidhaa ambazo sisi tumezitupilia mbali. Anajua faida ya kuzila ni haiba (na siha) ya mwili wake.
Tumalizie mada juma lijalo.

-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili, Mei 24, 2015.





No comments:

Post a Comment