Sunday, 7 June 2015

KWANINI LEO WAZUNGU WANAHUSUDU MAMBO TUSIYOYAJALI TENA?


Yupo Mwingereza mmoja maarufu sana aliyetimiza miaka 40 mwezi jana.
Huyu jamaa ana kipindi chake katika TV anachodondoshwa mwituni, jangwani au vichaka vya sehemu mbalimbali za dunia  na kuachwa. Hukaa bila chochote bali kisu kikali, mfuko mdogo na nguo alizovaa. Kuna wakati aliachwa pori moja la Zambia. Huko alizingirwa na wanyama, mito, chemchemi na nyika tupu. Alilala juu ya mbuyu. Chakula  kilikuwa wadudu, nyoka na maji ya mvua. Na hii tabia yake ya kula chochote anachokiona nyikani kiwe buibui,  chura, mchwa, asali, nyungunyungu,mbegu, matunda, madafu, majani, panya, fuko au ngiri ina malengo na mafunzo.
Mosi anajaribu kuonesha namna wanadamu tunavyopaswa kujua kuishi (na kumudu) bila kukata tamaa iwapo majanga yakitutokea au hakuna namna. Pili, anasisitiza wanadamu, (hususan Wazungu) tumeichangamkia teknolojia tukapoteza ubunifu, tukawa wavivu na waoga wa mazingira. Tatu, huelekeza kutokata tamaa, kujitegemea na kuwa wajanja pale shida yeyote inapojitokeza.  Zamani nikiwa jeshi la kujenga taifa (JKT) tulifundishwa ujuzi huu uliobatizwa nahau : “Ujanja wa Porini”...
Jina la huyu “mbabe” anayezidi kupendwa na hasa watoto na vijana  ni Bear Gryllis.
Ujanani, Bear Gryllis (pichani ) alikuwa  askari wa kikosi maalum cha Uingereza.


Bear Gryllis. Picha ya Wikipedia 

Nchi mbalimbali duniani huwa na jeshi la kawaida linalolinda taifa;  na ndani huteuliwa askari wachache makini zaidi, mashujaa, majasiri waliozamia mbinu za kivita, wenye uwezo na akili ya hali ya juu. Vikosi hivi maalum huteuliwa kupambana na mambo magumu ya kitaifa, mathalan ugaidi au ujambazi usio wa kawaida.
 Kwa Wamarekani wanaitwa “Delta Force”, ilhali Israel ni, “Sayeret Matkal.
 SAS (Special Air Service) ya Waingereza ndiyo mwasisi wa kikosi cha namna hii na wameigwa dunia nzima. Asili ya SAS ilikuwa kupambana na jeshi la Wajerumani wakati wa Vita  vya Dunia vilivyokwisha 1945.
Kikosi hicho cha  wachache kilipambana na maadui kikiwa na kila aina ya silaha na mapigano na kilidondoshwa kwa ndege (parachuti) na kufanya maajabu. SAS ilichangia sana ushindi dhidi ya majeshi katili ya Adolf Hitler.
  Awali kazi ya SAS ilikuwa faragha. Ila mwaka 1980 magaidi walipoteka nyara ubalozi wa Iran hapa London polisi walishindwa kuwakomboa  maofisa na wananchi 26 waliofungiwa pale kwa siku tano. Serikali ilituma kikosi kidogo cha SAS kilichoingia kimbinu na kusuluhisha tatizo. Huyu Bear Gryllis alikuwa askari wa SAS hadi alipostaafu baada ya kuumia kazini.
Ameshaandika vitabu kumi na tano vinavyozungumzia  mbinu za kuishi,  mtazamo wa matumaini, kufanya kazi na wenzako kijumuiya, kujitegemea na kutafuta masuluhisho ya haraka  bila kutegemea sana  teknolojia au bahati nasibu. Kwangu mimi mtazamo huu  ulikuwa ndani ya  maadili ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea  ya Azimio la Arusha la 1967, Tanzania.
Wazungu wanachukulia suala hili kwa undani zaidi.
Leo watoto wadogo wanakua wakiogopa kupambana na mazingira. Watoto wa Kizungu  hata watu wazima wanahofia kuchinja mnyama kusudi wamle. Lakini hapo hapo wako tayari kwenda dukani kununua nyama iliyoshatengenezwa tayari katika makasha na mifuko ya plastiki.
Bear Gryllis anachosisitiza ni sisi kukaribia maumbile.
Karibuni alitoa kipindi (documentary) ambapo wanaume na wanawake walipelekwa  visiwa viwili tofauti bahari ya Pacific wakaachwa pale kwa mwezi mmoja na nusu bila ya vifaa vyovyote vya kisasa mbali na camera (kurekodi waliyofanya) na vifaa vya huduma ya kwanza. Wananchi hawa wa kawaida walikuwa mseto wa taaluma mbalimbali tofauti na hawakuwahi kuishi porini.
 Baada ya siku chache wachache walishindwa  kutokana na shida kama namna ya kuwasha moto, maji ya kunywa (yalikuwepo kisiwani, ila ilibidi kujua kuyapata) au nge, nyoka, nk. Humo humo tulionyeshwa hisia zao mfano wanaume kuzozana na kupigana wenyewe kwa wenyewe, wanawake kulia ovyo, nk. Waliomudu waliwinda mamba, ngiri, nyoka na samaki na wakakaa hadi mwisho wa kipindi. Walikiri kujifunza mengi.
Mwisho, jasiri Bear Grylls aliporudi kuwachukua  alitoa fundisho kuwa leo mwanadamu kasahau kupambana na mazingira.
“Kipindi kinatufundisha kuishi kijumuiya. Ilibidi wahusika washirikiane, watumie mikono na akili ya kuzaliwa. Katika shida mtu hujiwa na nguvu mpya...”
Alisisitiza herufi TATU kuu. Wanadamu hatuwezi kukaa zaidi ya dakika tatu bila kuvuta pumzi, siku tatu bila kunywa maji na majuma matatu bila kula.
Yote haya yatuelemisha nini?
Sisi Waafrika tungali na maarifa haya. Bado tunaishi mbugani na mazingira yenye wanyama pori na mimea asilia. Bado hatuogopi kuchinja mnyama ili kumla kitoweo. Bado tunaishi mazingira yenye jumuiya inayosalimiana na kujamaamiana.
Waafrika tuko karibu na maumbile kuliko wenzetu.
 Wazungu wameshaanza kupoteza mengi kutokana na teknolojia na mashine za kisasa. Ingawa kuendelea huku kumerahisisha maisha, pia kumewapooza kiasi ambacho yabidi Mzungu ajifunze tena mambo mengi ya msingi ambayo kwetu ni kawaida. Mifano michache ni kama kuwasha moto mbugani na kutumia kuni. Je kwanini watoto wa shule za Kizungu waoga wa wadudu au moto?  
Juma lililopita tulitoa mfano wa jinsi ambavyo Waafrika tumeacha kula vyakula asilia. Tukichunguza wakati sisi tunaanza kuparamia maendeleo ya teknolojia wenzetu wameshajua madhara yake. Tumechangamkia magari, wao wanahusudu kutembea kwa miguu au kupanda baiskeli. Meya wa London, Bwana Boris Johnson huoneshwa kila mara akienda kazini kwa baiskeli huku kavaa suti na walinzi. Lengo ni kupunguza unene.
 Je, kweli utamwona kiongozi wa Kiafrika akienda kazini kwa baiskeli na suti? Wakati ambapo sisi tunaanza kuchangamkia mazoezi ya mashine (Gym) wenzetu wanahusudu zaidi kutembea mbugani, kupanda milima, kuogelea nk. Hii ni sababu mazoezi ya vyuma yamethibishwa kuhatarisha mifupa, viungo, magoti na mgongo. Wameshaona madhara.  Wakati ambapo sisi tunachangamkia simu za mkononi na kompyuta, wenzetu wametahadharishwa na hatari za mionzi yake inayochangia saratani. Muda wa kula,  kulala  au kupumzika, simu huzimwa kabisa. Sisi tuko nayo saa 24.  Wakati ambapo sisi tunachangamkia TV kwa kuiwasha saa 24 , Wazungu huwa kimya, kusikiliza redio na kuzima runinga wakati wa mlo. Teknolojia hutumiwa kwa nyakati muhimu kama kusaka wahalifu na kulinda nyumba. Maendeleo ya kiteknolojia ni muhimu sana. Ila yahitaji matumizi ya akili na uangalifu.

-Ilichapwa pia Mwananchi Jumapili, Mei 31, 2015






No comments:

Post a Comment