Sunday 21 April 2013

WATU WEUSI TWAKUMBUSHWA MADHARA YA ULAJI CHUMVI NYINGI



Ladha ni kitu muhimu sana.

Siku moja nilikuwa nimealikwa karamu fulani kubwa- mwenyeji ni Mzungu aliyemwoa bibi wa Kiafrika. Kufumba na kufumbua dada mmoja, (sikumbuki taifa lake, lakini alikuwa Mwafrika)-hakuwa na raha hata kidogo na misosi. Kawaida ukialikwa hizi karamu za kimataifa, si mara zote utakuta vyakula vya kwenu; ulivyozoea. Mathalan, Wazungu wanavyokula ni tofauti sana na sisi. Hutumia vitu ambavyo si mazoea yetu mfano jibini (chizi), kachumbari nzito (“mayonnaise”) yenye mayai, siki, mafuta, malai (“cream”), nk. Au kuna suala la nyama.

Siku hizi idadi ya wasiopenda nyama jamii zilizoendelea imekua kubwa kiasi ambacho ukihudhuria mikutano au makongamano ya kimataifa unaulizwa (kabla) je mlaji nyama au hapana.Basi dada hakua na raha.Meza zilijazana vyakula vya wanga, mboga, nyama na protini. Dada alilalamika ladha.



“Hiki chakula sijui kikoje; mdomoni hakiingii.”
 Turudi nyuma. Mtoto mdogo hupenda sana sukari na ndiyo maana lawalawa  humnyamazisha akighafilika. Karibuni hapa Uingereza, serikali imetahadharisha makampuni  yanayojaza sana sukari na chumvi ndani ya vyakula wanavyouziwa watoto. Wafanyabiashara wanawahadaa watoto  ili kupata fedha. Sukari nyingi kuharibu meno ya watoto; huchangia unene na kuwafanya wasitulie wakachangamka kupindukia wakati wa masomo.
Jambo hili limeifanya jumuiya ya mataifa ya Ulaya (EEU) kupitisha sera ya kubandika muhtasari wa nini kilichomo ndani ya vyakula madukani. Utaratibu huu unazifaa jumuiya zenye watu waliosoma ambazo ndizo nchi tajiri. Je kwa nchi maskini? Je, ni kila mtu atafuatilia ni kiasi gani cha sukari na chumvi iliyopo ndani ya vyakula madukani? Ladha ni kitu kinachotumwia sana na wafanyabiashara.  Kila taifa lina ladha zake maalum. Mara nyingi ladha hizi zinapendeza mdomo lakini madhara yake mwilini hayaelezwi na makampuni makubwa. Mathalan ukizidisha sana sukari  na usiposukutua sawasawa waweza kuharibu meno na kuongeza harufu mbaya ya mdomo. Tuendelee.
Hatimaye malalamiko ya dada yalimfikia mmoja wa wahudumu, akaja mbio.
Dada: “Pilipili na chumvi tafadhali.”
Mhudumu akatazama huku na kule.
 “Ipo Reggae Reggae Sauce. N’kuletee?”
Dada akatokwa macho kama mtu aliyeona mwangaza  baada ya umeme wa mgao kupotea juma zima.
“Reggae Reggae Sauce ndiyo yenyewe.  Na chumvi tafadhali.”
Reggae Reggae Sauce ni  mseto wa pilipili, binzari, kitunguu, chumvi, kitunguu saumu,  mdalasini, siki, tangawizi, nk.  Bei ya kachupa kamoja ni wastani wa shilingi elfu saba, London. Mseto ulivumbuliwa na mwanamuziki Mjamaika, Levi Roots mwaka 2007.
Sasa. Mhh. Leo chumvi ni suala linaloongolewa sana katika majarida ya afya, waganga na watu wanaohimiza chakula bora.
Mbali na chumvi kidesturi wengi wetu tumezoea kula chakula huku tukinywa  chai, maji, pombe, juisi, na vinywaji vingine vya sukari sukari. Tabia hii ya kunywa vitu huku tunakula imezoeleka kiasi ambacho tunaiona ya kawaida, lakini si nzuri kwa ini, figo na utumbo.


Chumvi inavutia sana vinywaji shauri hukausha mdomo, tumbo na damu. Kadri unavyozidisha chumvi ndivyo unaharibu damu yako. Wataalamu wengi wa afya wameonya chumvi nyingi inaweza kuathiri wanawake wakati wa siku zao. Kufuatana na maelezo ya shirika la maradhi ya presha ya moyo Uingereza, chumvi ikizidi husababisha maradhi ya moyo, saratani ya tumbo, matatizo ya figo, ubongo (kuwa msahaulifu uzeeni), maradhi ya mifupa (“osteoporosis”), pumu nk.
Hali ni mbaya kiasi ambacho shirika la Afya duniani (WHO) limesema ulaji mkubwa wa chumvi unatakiwa kupunguzwa kama ambavyo uvutaji sigara unatakiwa. Mwaka 2005, WHO ilitangaza vifo 35 milioni duniani vilivyotokana na maradhi yasiyoponyeka- kati yake asilimia 30 yamesababishwa na moyo. Kati ya maradhi haya, manane hutokea kwa watu wenye kima cha chini cha mshahara hasa nchi zinazoendelea likiwepo bara Afrika. Magonjwa husika ni moyo, presha na kisukari cha aina ya Type 2 –  kinachotokana na unene, ulaji mbaya, pombe nk. WHO imeitaja Nigeria ambapo maradhi ya moyo na presha, huathiri watu milioni 8- yaani asilimia 10 hadi 12 ya taifa hilo.
Miezi mitatu iliyopita runinga ya Sky hapa London ilitahadharisha Waafrika na watu weusi duniani kwa utumiaji kupindukia wa chumvi, na kwamba kitakwimu tunaongoza kwa vifo vya madhara yake.
Kiasi cha chumvi  kinachotakiwa kwa siku (kwa mtu  aliye na umri wa miaka 11 kuendelea)  ni gramu tano. Huu ni uzito wa chumvi ya unga ndani ya kijiko kidogo cha chai.  Kipimo hiki kimewekwa na kukubaliwa na mashirika ya kiganga na  WHO yenyewe.
Wapo watafiti wanaokinzana na kipimo; wanadai watu wanaochuruzikwa sana jasho – wanaofanya kazi za sulubu, wanamichezo na wakazi wa nchi za joto- wanatakiwa wale chumvi zaidi. Lakini pamoja na hayo, kutokana na vifo vinavyoendelea,  wananchi jamii hizi bado wanakula chumvi nyingi kuliko inavyotakiwa.
Utafiti uliofanywa mwaka juzi na mganga mstahiwa, Dk Derin Balogun (anayeongoza kampeni dhidi ya kuondoa maradhi ya moyo na presha) uligundua kwamba mahoteli ya Waafrika na watu weusi jijini London hupika vyakula vyenye chumvi nyingi sana. Gramu 12 zilipatikana katika wali na maharagwe, gramu 8.6 ndani ya wali (maarufu) wa “Jollof” toka Afrika Magharibi na gramu 19 kwenye mikate. Hii ni chumvi  zaidi ya gramu 5 zinazotakiwa kwa mtu mzima, kila siku.
Akiongea Nigeria mwaka 2008, Dk Balogun alisema tatizo hili -linaloua wengi- linasababishwa na “chakula chenye mafuta na chumvi kwa wingi; unene, kutofanya mazoezi na kutokula mboga za majani na matunda.”
Suala la mazoezi ni muhimu sana.  Jingine muhimu ni unywaji maji.
Mseto wa majani ya Salad (bila chumvi yeyote) unaweza kusaidia kuweka uwiano kwa chakula kilichojaa chumvi, pilipili nk

Ulaji chumvi nyingi unasababisha kiu; chumvi ina madini inayonyonya damu (“sodium”) na ndiyo sababu wengi wetu tumejenga desturi ya kupata kinywaji wakati wa kula. Si vizuri kunywa maji pamoja na chakula. Maji yanatakiwa kunywewa dakika 15-30 kabla au baada ya chakula ili kutoharibu umeng’enywaji tumboni.
Kuna, aghalabu, starehe na dimba la mazoea. Ilinichukua muda kuzoea kula bila chumvi nyingi. Ilibidi nijifunze. Wataalamu wanashauri ukimudu kupunguza asilimia 60 ya chumvi unayotumia kila siku unajenga nguvu za moyo, miondoko ya damu mwilini na hatimaye kuongeza urefu wa maisha yako. Vyakula na mimea vina chumvi asilia toka ardhini na rutuba ya ulimwengu. Chumvi ni mazoea tu ya kiladha.  Zamani wanadamu hatukutumia chumvi nyingi kama leo.

Ilitoka pia  Mwananchi Jumapili....


No comments:

Post a Comment