Thursday, 2 April 2015

NASAHA KWA WATANZANIA WANAOULIZIA WAFADHILI NJE- Sehemu ya 3



Mti alionyongewa Mangi Meli Makindara wa Old Moshi mwaka 1892. Wakoloni wa Kijerumani waliua viongozi wengi. Mfano mzuri wa kumbukumbu toka Blog la Xanadu.

Toka niishi dunia ya  Wazungu nimejifunza jambo moja. Wenzetu wana mafanikio kwa sababu wanathamini sana vitu vyao. Hapa Uingereza hupenda kuhifadhi sana sanaa yao. Hata zile zilizoibiwa enzi za Ibilisi wa ukoloni, bado zimehifadhiwa.
Kwa mfano rejea siku magaidi wa ISIS walipoharibu haribu na kuvunja vunja makumbusho ya kale ya Iraq wiki kadhaa zilizopita.  Makambusho haya ni sanaa na sanamu zilizojengwa na wananchi wa zamani kabla hata dini za Kikristo na Kiislamu kubuniwa. Tukio  limepingwa vikali na Umoja wa Mataifa. Hifadhi za kijadi ni sawa na makaburi na tambiko za ndugu na mababu zetu.  Sasa tukio “limefutwa machozi”  na Waingereza waliotangaza kuwa wanazo baadhi ya hifadhi hizo katika majumba yao ya makumbusho.
 Sanaa  hizi zilizoporwa kipindi cha ukoloni  ndiyo kumbukumbu pekee za mila na ustaarabu wa Waarabu. Kwanini Mwingereza apende kuhifadhi vidude hivi? Kwanini kichwa cha shujaa wetu Mtemi Mkwawa wa Wahehe (aliyepigana dhidi ya Wakoloni wa Kijerumani) kikarejeshwa na kuhifadhiwa kijiji cha Kalenga? Kati ya mafuvu mengine ni lile la Mangi Meli Ringi Makindara aliyenyongwa mbele ya watu wake Old Moshi, mwaka 1892. Jitihada za kudai fuvu hilo lirejeshwe Kilimanjaro, sijui zimeishia wapi.  Mara ya mwisho (2005), Ubalozi wa Ujerumani ulisema kichwa hakikupatikana.
Hifadhi ni kumbukumbu. Kumbukumbu ni historia. Historia ni muhuri wa maisha ya mwanadamu.
Kwanini hatusikii wengi duniani wakiiga muziki  wa Kitanzania? Lakini vipi sisi tuko radhi kuiga mtindo wa Ndombolo toka Congo DRC? Kwanini utasikia bendi maarufu ya Kitanzania leo ikiwika nje au ndani lakini mapigo yake lazima yamwage Seben? Nini kinawafanya watalii wamiminikie Jamaica kucheza Reggae ; Cuba kusakata Salsa na Brazili kujifunza Samba? Mbona hawaji Tanzania kuchangamkia na kujifunza Mduara, Mdundiko na Sindimba?
Ukiona wengine wanakuiga jua unalo zuri.
Na zuri huwa haliji kwa kukopa, kuiga, kujifanya, kutamani, kuomba, kudai. Huja kwa kuunda. Uvumbuzi hutokana na undani wa mtu mwenyewe. Watanzania lazima tujikumbushe  tunakotoka. Watoto na vijana wanaokua leo shurti tujichunguze sisi nani. Kwamba kabla ya kuja hawa wageni tulikuwa na ngoma, ibada, imani, mila na desturi. Leo tambiko na imani zetu zimepambwa na kufuja utamaduni wa Kizungu na Mashariki ya Kati kuliko makabila na asili zetu. Leo mtu mweusi yuko tayari kupigana (hata kuua) kutetea desturi hizi za kigeni.Yabidi tujirudi na kujipenda.Lakini si rahisi.  Bado tunakabiliwa na ukosefu wa elimu (ujinga), umaskini na maradhi.
Adha hizi zimetugeuza  omba omba. Na sio tu wananchi wa kawaida. Viongozi wetu bado wanategemea misaada na kudra ya wageni. Serikali zinaendeshwa kwa misaada. Mwaka 2010 Benki kuu ya dunia ilieleza kuwa  deni la nchi zinazoendelea lilipanda kutoka Dola trilioni 4.4 hadi trilioni 4.9 miezi kumi na miwili baadaye. Ongezeko hili la Dola bilioni 464 laweza kuwasomesha watoto wote wa Tanzania kwa kuwalipia ada ya dola 150 kila mwaka kwa kipindi kirefu sana.
Kama tulivyoona katika uchambuzi wa makala mbili zilizopita fedha na vifaa vya fadhila havitolewi kwa kila mtu. Hata hivyo wapo wafadhili wanaosaidia shida mbalimbali.
Lakini utawajuaje? 
Tovuti la Forbes limetaja mashirika 50 makubwa ya fadhila Marekani. Picha ya Forbes

La kwanza kabisa jifunze kuwa mtafiti mzuri.  Lazima ujifunze kusoma na kuelewa unachokitafuta. Fedha haipo tu kuchota. Je unajua kutafuta habari katika mitandao? Je unaifahamu Google au Bing?
Yakubidi uelewe maneno ya Kiingereza kama “charities”, “aid trust”, “foundation”, nk.
Ukibofya neno “charities for Africa” (Fadhila kwa Waafrika) ,mathalan, utaukuta msururu wa mashirika mbalimbali yanayotoa misaada barani. Wazungu wengi wanaojiunga na mashirika haya hufanya kazi kwa kujitolea au mshahara mdogo sana.
Dhamira kuu  ni kuondoa umaskini na maradhi kupitia miradi jumla. Mara chache sana utakumbana na shirika la fadhila (“charity organisation”) likijitangazia kumsaidia mtu binafsi. Mfano mzuri ni  tajiri Bill Gates ...mwasisi wa Microsoft. Bill Gates alipostaafu aliamua mwisho wa maisha yake utakuwa kuendeleza wasiojiweza.
Ukisoma na kuchunguza mashirika yake ya fadhila utagundua  anazungumzia matatizo ya watoto yatima, wasichana au kina mama wanaonyanyaswa, maradhi kama Malaria na umaskini uliozidi kiasi. Mfano mzuri wa ya misaada anayoitoa pamoja na mkewe (“Bill and Melinda Gates Foundation”) ni  mtaji kuanzisha duka la pamoja. Unaweza kumwandikia. Lakini itakubidi ujue masharti ya shirika lake.  Mashirika ya fadhila hutakiwa kisheria kuendeleza makundi au watu waliojisajili kuendeleza jamii. Hayatoi fedha za mtaji wa biashara ya binafsi.  Lengo lake si biashara.
Tathmini  msaada wa kutokomeza Malaria unaotolewa na tajiri Bill Gates. Ukibofya ukurasa  wake utaona akisukuma msaada wa waganga wakujitolea kupunguza adha ya malaria; ama kusafirisha nyavu za mbu . Au  kuwahudumia wafanyakazi wa kujitolea kuendeleza miradi ya shirika, yaani kupigana na maudhi ya mbu.
Sasa utajiuliza  je, Bill Gates atanisaidiaje nimalize kusoma? Je nitamwanzaje? La kwanza kabisa yabidi usome vizuri na kujua yeye nani na mashirika yake yana utaratibu gani? Huenda ukimwandikia atakujibu. Lakini lazima ujue namna ya kuiandika hiyo barua. Zingatia masharti kuwa yeye hasaidii mtu kutajirika. Hairuhusiwi.
Prince Charles. Picha ya Wikipedia

 Mfano mwingine ni wa mtoto wa Malkia Elisabeth wa Uingereza. “Prince Charles Trust” wenye misaada kadhaa ikiwemo elimu na mafunzo kwa vijana wasiojiweza  Ila wanaopewa msaada huu ni raia wa Uingereza tu.
Sasa  unapoanza kutafuta watu kama hawa lazima usome sawasawa masharti.  Nimejaribu kuandika neno “International Grant for education” katika Google. Neno “International” lina uzito maana ni la dunia nzima. Nimekuta shirika la   “Trickle Up.” Shirika hili  hutoa mitaji kwa watu wenye kipato kidogo, chini ya dola moja kwa siku  kiwastani,  shilingi elfu moja. Hawa hupewa mtaji wa Dola 100 hadi 250 kuanzishaa biashara au mradi mdogo.
Kwa hiyo yapo mashirika yanayosaidia watu binafsi.
Je nimefikaje hapo? Nimesoma maelezo. Je wewe ni msomaji mzuri au “unaotea” tu bahati?
Makala hizi tatu zimejaribu kutomasa tomasa dhamira ya fadhila. Nimeamua kutazama mada baada ya kupata barua na maombi lukuki ya wananchi wanaotafuta wafadhili ughaibuni. Natumaini angalau nimechokoza utafiti wako msomaji. Na kukuelewesha wapi pa kuanzia.

 -Ilitoka Mwananchi gazeti Jumapili 29 Machi, 2015.





No comments:

Post a Comment