Thursday, 2 April 2015

NASAHA KWA WATANZANIA WANAOULIZIA SANA WAFADHILI NJE - 1


“Mafanikio maishani yahitaji mawili; kutojua  na kujiamini,” aliandika mtunzi maarufu wa riwaya, Mark Twain. Zamani shuleni tulisoma vitabu vya Mark Twain vinavyofundishia Kiingereza ulimwengu mzima. Kati ya riwaya ya sifa na sambusa ni The Adventures of Huckleberry Finn. Mashuhuri sana. Kisa chenye kejeli na utani kuhusu ubaguzi wa rangi. Nukuu, elimu na hekima za Mmarekani huyu aliyezaliwa mwaka 1835 akafariki 1910, (akatajirika kutokana na fasihi)  hunyofolewa sana na wengi. Wanadamu tunapenda kujifunza kwa wenzetu waliofanikiwa kitaaluma na kimasilahi. 
Mtunzi wa riwaya Mark Twain, mwaka 1871. Kitabu chake , Huckleberry Finn, hutumiwa mashuleni kujifunza Kiingereza ulimwengu mzima. Picha ya Wikipedia

Hebu tuikague nukuu hii kusaidia maongezi ya leo. Kutojua kwaweza kuwa ujinga na Mwalimu Nyerere aliwahi kufafanua ifuatavyo...
 “Mjinga akishaambiwa, inakwisha.Ujinga ni kutojua. Maana hujui kulifanyika nini. Upumbavu ni kipaji kama ufupi na urefu...” Sijui  hayati Nyerere alimaanisha nini  ila msomaji ukichunguza utabaini kipengele kile kile alichoongelea mwanariwaya Mark Twain.  Kwamba kutojua si jambo la kuhukumiwa. Ni motisha wa kuishi.
Nahau ya Mark Twain iliongezea neno “kujiamini.”
Kwa vipi?
Viongozi wa zamani wa TANU walitueleza maadui mahsusi barani ni ujinga, umaskini na maradhi. Kutokana na maadui hawa, (kama tulivyotathmini safu ya wiki jana), asilimia 43 ya watoto Afrika hawasomi. Ukosefu wa elimu ni kitanda cha shida zote za mwanadamu. Chukulia  theluthi mbili ya Waafrika ni vijana chini ya miaka 30; ina maana mazingira yetu yanatawaliwa na ujinga.  Na si tu elimu ya vitabuni. Kuna ulimbukeni, unaotokana na TAABU za kijamii. 
Mwalimu akiwa kijana. Hii picha ya jalada la kitabu cha maisha yake kabla hajatumbukia siasani. Kimeandikwa na Thomas Molony karibuni.

 Mathalan tunaaambiwa karibuni,  mbwa ni kitoweo mahsusi  cha jirani zetu Kongo, “kwa sababu, nyama ya mbwa ni bei nafuu na rahisi zaidi kupatikana kuliko ya ng’ombe.”  
Taabu zinatutwanga mithili ya mchi unaoitandika nafaka katika kinu. Taabu, umaskini na maradhi vimekuwa utamaduni.  Hata mtu anapopata wadhifa mkubwa akawa kiongozi wa nchi atang’ang’ania hadi awe mzee wa miaka 90, ili mradi anatumia nafasi aliyopewa na wananchi kujinufaisha yeye na ndugu zake. Anawapa kazi rafiki zake  akila na kuhakikisha akiondoka damu yake inaendeleza jahazi. Mtu anakaa madarakani hadi anaanguka ovyo na kuwafukuza kazi walinzi wake eti hawakutabiri alivyojikwaa? Tuliache hilo. Tujiulize.
Wangapi wanashangazwa namna vijana wanavyogeuza kila kitu siasa , siku hizi, maana “wanajua” ni ajira? Badala ya siasa kuwa mwongozo wa kuendeleza uchumi- jamii; siasa imekuwa nahau na nukta ya ubadhilifu. Kila msimu Rais wetu anatifua udongo wa baraza la mawaziri.  Kasheshe, jama.
Siasa sio? Mradi ujue kusema, kudanganya na kuugeuza huo uongo kuwa ahadi na matumaini. Tutaona uchaguzi utakavyotifua moto, Oktoba. Penye  taabu, kila mtu mjanja. Lakini hatuko peke yetu. Dunia mviringo.  Dunia ya leo yataka  taaluma na mtaji ili kuendelea. Kuendelea vipi? Mwanadamu anahitaji makazi, mavazi na chakula aishi. Akivikosa huhangaika na kuchanganyikiwa.
Siyo mastaajabu basi kutuona wengi tukibabaisha na kutafuta riziki popote inaponukia. Huanza na mtazamo finyu unaoasa kuwa kila unalolitaka hutokana na kusaidiwa na wageni.
Hapo ni “kutojiamini.”
Ukitafakari historia yetu wanadamu kila jipya linalovumbuliwa huanzia kwa  mtu binafsi. Mara chache sana ikatokea serikali au kundi likagundua jambo zito. 
Mshairi na mwanamuziki maarufu wa Kimarekani Bob Dylan. Picha ya Wikipedia

Mfano. Wasanii. Mwanamuziki  na mshairi maarufu wa Kimarekani, Bob Dylan anaeleza katika kitabu cha maisha yake (Chronicles, 2004) alipoanza utotoni aliamua “ataandika nyimbo kubwa zaidi ya maisha atakayoishi.”
 Na kweli ametimiza azma hiyo. Ujumbe ulioko ndani ya nyimbo za Bob Dylan si wa kawaida. Historia itamkumbuka Bw Dylan, kwa kachangia kubadili namna wanamuziki wanavyotunga nyimbo. Awali mwanamuziki alikariri tu nyimbo za wenzake (covers).
 Mwanamuziki na mtunzi maarufu wa Kijamaika, marehemu Bob Marley, alipoulizwa alianza lini kuimba alijibu “nilianza nikilia” akimaanisha  alipotoka tumbo la mamake, akavuta pumzi, uimbaji ulifungua dimba.  Mzizi.
 Mpiga gitaa na mtunzi wa kusifika wa Kimarekani, Nile Rodgers aliyebuni vibao vilivyoshaimbwa na Madona (Like a Virgin), Diana Ross( Upside Down), Sister Sledge (We are Family), Chic (Le Freak), Get Lucky (Pharrell Williams), nk; alikulia shida za umalaya, dawa za kulevya na ujambazi. Ila alipoiona maiti ya baba yake mlevi na fukara kando ya mtaro, akiwa bado mtoto aliamua lazima afaulu maishani.
 Profesa Tim Berners- Lee, Mwingereza aliyevumbua  tovuti, bpepe na mtandao tunaotumia leo. Picha ya One Life Success.

Je, wanasayansi? Mvumbuzi wa mtandao (inteneti) tunayoitumia leo, kila nyanja, ni Mwingereza Profesa Tim Berners-Lee, mzawa wa hapa London familia iliyofanya biashara ya  kompyuta. Bwana Berners Lee alikichezea chombo hiki na mwaka 1989 akavumbua HTTP,  kiini cha mtandao na tovuti. Akihojiwa mwaka 2010, alisisitiza hakugundua mtandao, bali alichofanya “ni kuyaoanisha  mawasiliano haya yafanye kazi pamoja na hapo pakatokea jipya, yaani WWW.” Kitendo kama hiki chahitaji ujue tayari jambo unalolifanya. Kwa kuwa alishazoea kuchezea chezea tarakilishi tangu  mtoto ilikuwa rahisi kuendeleza chombo hicho ambacho kimeleta mapinduzi ya mawasiliano duniani. Profesa Berners Lee ni mfano mzuri wa mtu KUTHAMINI jambo ulilozaliwa au kukua  nalo.
Yeye na tuliowataja juu waliamua utotoni kufanya walichokitaka bila kutetereka.
NI ushauri mzuri sana kwetu Tanzania.
Kujua unachokiweza na unachotaka kukifanya ndiyo siri ya mafanikio yako. Wengi wetu hutaka kujibu swali HIKI KITANIFAIDIA NINI badala ya kulenga JE MIMI NINAPENDA NINI AU ‘NAWEZA KUFANYA NINI? Mtazamo wa kuanza fikra na azma ya kufaidi  (au kujua matokeo ya) kitendo hutughafilisha pale mafanikio yasipoonekana. Matokeo tunajidanganya hatuna bahati, tuna mikosi; tuelekee tu kwa wachawi kuwapa vipande vya miili ya Albino.
 Mchukue mtu aliyekulia  mazingira ya ukuli, sulubu na kubeba mkokoteni. Ikiwa ataithamini  kazi ya mikokoteni na kuijua anaweza hatimaye kuunda kiwanda kidogo, kampuni au kituo cha kuendeleza mikokoteni. Badala yake mlalamikia Mungu. Kutamani (mosi) magari na majumba ya fahari. Kumbe fahari ni ujuzi wako. Hili liko pia kwa mtu aliyezaliwa mazingira magumu kijijini. Anajua kilimo. Au mifugo. Badala ya kujaribu kujiendeleza na kile anachokimanya atavitupa. Atakimbilia mjini. Huko atakutana na wajuaji. Atafanya asiyoyazoea. Ataitwa bwege kwa vile hajui kuendesha gari, Kiingereza au kuvaa kinamna fulani. Ujuzi wa vijijini  utaishia  mtaroni. Mifano hii michache inaweza kupanuliwa kwa kuangalia taaluma au fani nyingine zozote kama michezo, ususi, upishi, nk. Tumalizie mada juma lijalo.

   -Ilitoka Mwananchi Jumapili, Machi 1, 2015






No comments:

Post a Comment