Thursday, 2 April 2015

NASAHA KWA WATANZANIA WANAOULIZIA WAFADHILI NJE- 2


Lipo tangazo linalorudiwa takriban kila kituo cha runinga huku Uzunguni, siku za karibuni. Tangazo humwonyesha mtoto mdogo wa kike, mweusi kama mpingo; mzuri ajabu, macho maangavu na uso uliotulia. Mwafrika. Watoto ni malaika, wahenga walisema. Na kweli wajihi wa msichana huyu wa Kimatumbi ni mkono wa Mungu. Namkisia ana miaka miwili au mitatu.
Sekunde kumi baada ya tangazo sauti ya mtu itasema kwa Kiingereza kuwa msichana haufahamu mustakabal wake. Hajui kitakachomfika mbeleni, maana yeye si mwaamuzi wa maisha yake. Atakapotimiza miaka 13 atakuwa ameshaolewa na miezi 24 baadaye keshajifungua mtoto mmoja na kuharibikiwa mimba mbili . Hapo hapo atakuwa kabanwa na maisha ya ndoa ya kitoto kwa jibaba kumzidi umri litakalomgeuza kijakazi, mtumwa, punda, mama watoto; udhia mtupu.
Tangazo huwaomba “wafadhili” watakaomsaidia mtoto husika aondokane na adha inayowakumba wasichana kuolewa mkuku kabla hata hawaja balehe sawasawa. Tutathmini  zaidi hoja. 


Msichana aliyeshakuwa mama mzazi. Picha ya Sauti Moja...
Takwimu zinatueleza, kiwastani, msichana wa Kitanzania hupata mimba akiwa na miaka 19 na kuolewa muda mfupi, baadaye. Kidesturi kipindi hiki cha kijana yeyote humkuta akiingia chuo kikuu kukamilisha taaluma ya maisha yake. Lakini, nyoo. Tukihesabu mitaani je ni wanawake wangapi waliochishwa shule, baada ya kupata mimba;  baba watoto hawaonekani, wanalea peke yao? Shida na mashaka. Kichuguu, msumeno, dhihaka, kokoto.

Turudie  tangazo letu la TV.
Matangazo mengi “yanayotafuta wafadhili” huku Uzunguni leo yanahusu mambo kama haya. Kawaida “wanaosaidia” si matajiri. Ni wananchi wa kawaida wanaopigwa kofi la huruma wanaposikia kisa kama kile; maana Uzunguni ni hatia kuoa mtoto chini ya miaka 18. Wananchi walioguswa, basi, huombwa kutoa kama shilingi 6,000 kila mwezi ambazo huenda moja kwa moja kukimu miradi ya kuwaendeleza watoto nchi zinazoendelea.
 Maendeleo hayo huangaliwa na mashirika ya misaada yasiyo ya kiserikali (NGO), ambayo humletea mfadhili ushahidi kila baada ya mwezi au miezi kadhaa. Picha za watoto, shule wanazokwenda,  shughuli wanazozifanya, nk. Siku hizi wafadhili wanahofia sana misaada yao kuibiwa. Nadhani msomaji umesikia habari za utata kuhusu msaada wa wagonjwa wa Ebola. Majuma mawili yaliyopita serikali ya Sierra Leone ilidaiwa kupoteza kiasi cha dola milioni 18 zilizotolewa na mashirika ya kimataifa kukirimu wagonjwa wa Ebola. Mkaguzi mkuu wa mahesabu, Sierra Leone, Bi. Lara Taylor-Pearce  alikiri kupotea kwa mamilioni ya fedha zilizotolewa na wafadhili. Kwa kuwa mama huyu ni mkweli, inadaiwa, baadhi ya mafisadi serikalini wameanza kumpaka matope, huku wananchi wakiendelea kuzongwa na Ebola. 
Bi Lara Taylor Pearce  wa Sierra Leone.

Huu ni mfano.
Lakini tunapoongelea “wafadhili” tuna maana gani?
Tofauti baina ya maisha ya kwetu Afrika na hawa wenzetu ni kwamba jamii zao zilishapitia baadhi ya mambo magumu tunayopitia leo.  Wamejifunza na  hilo huwafanya waonekane wameendelea sana kutuzidi. Kwa vipi?
Kwanza, uchumi.  Huku Uzunguni kuna maskini na matabaka kama  kwetu. Matajiri wachache wanamiliki vyombo vya uchumi na maisha, ilhali wengi wanataabika. Watalii tunawaona wakija mbuga zetu za wanyama huwa wameweka akiba muda mrefu. Huwa wamejinyima kula na kuvaa kumudu matembezi  ugenini.
 Pili, utamaduni. Kidesturi, Mzungu ni yeye na tumbo lake tu. Siyo kama sisi; ukijaaliwa  shilingi laki tano, si zako mwenyewe; utasaidia ndugu zako. Ndiyo maana si rahisi kwetu kuweka akiba. Utamaduni wa “kila mtu na lwake” umetokana na mfumo wa uchumi huria na mali binafsi uliokwea msufi karne nne zilizopita. Ni utamaduni unaopayuka wimbo wa  “hakuna cha bure.” Kutokwa jasho na kufanya kazi. Kujali muda. Time is money, ni msemo mahsusi wa mfumo huu wa maisha.
Sasa unapokopa fedha kwa Mzungu lazima urudishe. Usiporudisha urafiki unakwisha. Unapoomba fadhila lazima kuwe na sababu za fadhila.
Hapa sasa...
Haya matangazo yanayowekwa siku hizi hulenga  Wazungu wa kawaida wanaotoa kidogo walichonacho kusaidia yale wanayoona ni majanga . Si rahisi mtu yeyote tu uliye na matatizo yako ukapewa msaada au fadhila. Kinachozingatiwa ni je, ule msaada kweli unahitajika? Na kama unahitajika matokeo yake nini? Mathalan kijana wa Kitanzania aliyemaliza kidato cha nne au cha sita sasa anataka kusoma zaidi, ila wazazi hawana fedha ( au yatima) hawezi akasaidiwa na watu wa aina hii.
Ngoja lakini...
Bill Gates. Tajiri mkubwa anayetumia maisha yake kusaidia maskini na wasiojiweza duniani.
Picha ya gazeti la Daily Telegraph

Lipo daraja  la pili la utoaji fadhila. Hutoka mashirika yanayogawa fedha za miradi ya maendeleo. Mashirika haya si ya maskini. Huwa ya michango mikubwa ya matajiri, wafanyabiashara waliostaafu (mathalan, Bill Gates mwasisi wa Microsoft), au fedha zilizotokana na salio la mfuko wa bahati nasibu (Lottery Fund). Kuna pia mfuko uliowekwa na mtoto wa malkia Elizabeth yaani Prince Charles kusaidia miradi mbalimbali. Au mashirika yanayosaidia miradi ya wasanii kama Arts Council of England.
Mashirika haya yanao utaratibu mgumu  ila wa miradi ya kufaidisha jumuiya nzima. Mfano mzuri ni taaluma. Kama nyinyi mnalo shirika linalohudumia au lenye malengo ya kusaidia jumuiya nzima, mfano ujenzi wa maktaba, shule, zahanati, huduma za maji na chakula,nk. Mashirika kama haya yanaweza kutoa fedha kuwasaidia.   Lakini fadhila hii si mteremko.
Yataka vitabu, kupanga, ushahidi na ukweli. Yataka muwe mumetafiti vyema mnachokusudia. Muwe mumeweka makadirio dhahiri ya gharama mtakazotumia na kipato hakika cha yale mtakayoyafanya.  Matumizi lazima yawekwe wazi na sawa. Kusiwe na udanganyifu, ubadhilifu na kujilimbikizia mali binafsi. Hapa ndipo fadhila ya kweli inapopatikana.
Hivyo basi Mtanzania unapozungumzia neno wafadhili, zingatia baadhi ya mambo niliyoyataja. Mosi, usidhani kila Mzungu unayemwona ni tajiri. Halafu, zingatia kuwa msaada ni kwa waadilifu. Wizi  na ufisadi unaotokea na unaondelea kutokea nchi zetu ( baada ya misaada kutolewa) umefanya mashirika ya misaada kuwa macho sana. Tahadhari hii si tu Afrika bali kwa wanaohitaji, Uzunguni.
Mwisho zingatia kwamba maendeleo yako yatatokana na kile unachokipenda au kukifanya kwa moyo. Usiwe  na uchu wa kurukia gari au farasi asiye wako.  Zingatia mifano tuliyoitoa wiki jana ya baadhi ya watu mashuhuri waliofaulu maishani. Walifanya na walizingatia kile walichokijua na kukipenda toka utotoni.


 -Ilichapishwa gazeti la Mwananchi  Jumapili Machi 22, 2015. Lakini haikuwekwa mtandaoni







No comments:

Post a Comment