Sunday, 30 November 2014

TEZI KIBOFU, AFYA NA KINGA YA MARADHI YANAYOTUKABILI -sehemu ya 1
Wiki hii,  Mheshimiwa Rais J Kikwete, alikuwa Marekani kufanyiwa matibabu ya tezi ya uume, hospitali ya John Hopkins,  Baltimore. Kitakwimu maradhi haya huwafika asilimia 45 ya wanaume walioshapitisha miaka 60.   Ingawa lengo la makala haya si kuzungumzia hali ya Rais, ni vizuri tukitathimini tatizo hili linalowasakama wanaume wengi. Miongoni mwa walioshafikwa ni marehem Nelson Mandela, kiongozi wa Waislamu Marekani, Louis Farahkan, mwanamuziki maarufu hayati James Brown, mwigizaji mashuhuri wa Hollywood, Robert De Niro, nk.
Miaka michache iliyopita niliwahi kuandika juu ya afya ya uume ( na uke vile vile) na kuhimiza haja ya kuelewa namna ya kutunza na kufanya mazoezi kutunza viungo hivi. Kwa wanaume viungo viwili muhimu husika ni mfuko wa mbegu (korodani) na tezi kibofu. Visipoangaliwa vyema husababisha saratani ambayo kihisabati,  inaua mwanaume mmoja kati ya  saba, duniani. Moja ya suluhisho kuu ni kuzifahamu dalili   kabla hazijaota kutu.  
Lakini tezi ya uume au tezi kibofu, ni nini hasa?

Tezi hii ni kidude cha mviringo, kiwastani,  ukubwa wa  jicho la mwanadamu. Hukaa chini ya kibofu cha mkojo. Kazi ya tezi hii ni kutengeneza maji yanayolinda na kurutubisha mbegu nyeupe za uume. Tezi huanza kuvimba tunapofikisha miaka 50. Mwanaume mwenye bahati kufikisha miaka 90, anategemewa kufikisha uvimbe uliovuka asilimia 90, kiumbo. Ni nadra sana kwa kijana chini ya miaka 40 kusakamwa na adha hii. Hata hivyo leo maradhi ambayo zamani yalikuwa ya watu makamo na wazee yameanza  kuwatoboa vijana.

 Kwa vipi?
 Chukua mfano tezi kibofu. Harufu mbaya toka mbegu za uume au kuumwa  mbegu  zikitoka wakati wa ngono, ni dalili. Hapo hapo tuzingatie kuwa tatizo kubwa zaidi yaani saratani ya tezi kibofu ni nadra sana kwa wanaume chini ya miaka 60.
Je,  huanzaje? Au tuseme matatizo ni yapi?
Yana  matawi  mawili. Tezi kuvimba na hatimaye kupungua likitibiwa au kuangaliwa vyema na mapema au hugeuka  saratani. Saratani ya tezi ya uume,  ni tatizo kubwa zaidi ambalo humbidi mgonjwa kupasuliwa . Upasuaji unapofanywa kuondoa tezi hii mtu hufikwa na tatizo la kushindwa kuzuia haja ndogo  au kubwa (“incontinence”), kupungukiwa kabisa nguvu za uume, nk. Watu mashuhuri waliozungumzia  kwa uwazi ni pamoja na marehemu mwanamuziki nguli, James Brown na Nelson Mandela.

Dalili za kuvimba zinazoanza kuonekana ni njia ya mkojo kuwa nyembamba na kuzuia mtiririko wa haja ndogo. Mtiririko huwa mdogo au wa kubabia babia, wa matone matone. Pili, huhisi mkojo,  haukutoka wote. Matokeo yabidi kwenda chooni mara kwa mara hasa usiku. Yabidi kukimbia shauri musuli ya uume imelegea na huwezi kujizuia. Tatizo hili lipo pia kwa wanawake. Miaka michache nilizungumzia haja yetu sote kufanya mazoezi kukomaza musuli yake. Subiri.
Je, mganga atathibishaje tatizo?
Ni muhimu sana kuwahi kujua dalili. Lakini wanaume wengi (hasa sisi weusi) hatupendi kutazamwa. Huona aibu kuhisi tumedhalilishwa kama madume. Kwanini? Kuna njia mbili, za uchunguzi. Ya kwanza (inayotubughudhi zaidi) ni mganga kuingiza kidole (chenye glovu) kwenye tundu la makalio kupima ukubwa wa tezi. Njia hii ina ugunduzi wa haraka na hakika zaidi. Ya pili, ni kupimwa damu na mkojo kutathmini figo zikoje. Maana tatizo la tezi kibofu huathiri figo na mtiririko mzima wa maji mwilini.
Waganga wanasisitiza ikiwa umeshaathirika usinywe maji saa mbili au tatu kabla ya kutoka nje au kwenda kulala. Ukienda kujisaidia jaribu kurudi tena punde kuhakikisha mkojo wote umekwisha.
Jaribu kutulia kwa kufanya mazoezi ya pumzi wakati wa kujisaidia. Epuka sigara na vinywaji vyenye “cafeine” katika  kahawa, chai na Cocacola. Juu kabisa fanya mazoezi kukomaza musuli iliyo kati ya mlango wa haja kubwa na  uume (uke). Musuli unaitwa PC (“pubococcygeus” ) , kitaalamu.  Mazoezi haya ni muhimu kujenga ustahimilivu kwa wanawake na wanaume. Unakaza na kukamua kamua musuli mara kadhaa kila siku.
Tukiendelea zaidi katika suala la ulaji. Tafiti za karibuni zimeelemisha  kuwa ulaji wa nyama choma au vyakula vyenye masizi huchangia saratani ya tezi.
Tuangalie zaidi tatizo la kuchoma nyama.

Utafiti uliofanywa Marekani mwaka 2013, ulifikia hitimisho la ngazi tatu. Mosi kwamba ulaji wa nyama nyekundu iliyookwa sana katika moto wa mkaa au moto mkali huchangia viini vya saratani (“carcinogens”). Pili, mvuke, joto na masizi yaliyoko katika moto unaozichoma nyama huwa na vimule mule vinavyoingia  mwilini ,  kuathiri maendeleo ya maumbile takikana (DNA) na kuchangia kuanza kwa saratani.
 Tatu, kuna viini vinavyoitwa “heterocyclic amines” (HCA) ambavyo hutokana na nyama kupashwa moto kwa nguvu. HCA hupenya mwilini kupitia utumbo mkubwa na kusababisha saratani mbalimbali kama  ya utumbo mkubwa, matiti ya wanawake nk. Utafiti umethibitisha HCA zipo zaidi katika nyama nyekundu za ng’ombe, nguruwe na kondoo zilizochomwa. Hapa utafiti unasisitiza kula nyama choma hakusababishi saratani. Ila nyama zinazochomwa katika mahoteli au haraka haraka nje kwa moto mkali hadi zikaungua , hadi kuwa na masizi masizi,  ndizo hatari. Jaribu kuzingatia hilo ewe msomaji mpenda nyama choma.
Tatizo jingine la ulaji ni vyakula vyenye mafuta mafuta,pombe kuzidi kiasi na kutofanya mazoezi ya viungo.
Kuna dawa na vyakula vinavyosaidia afya ya tezi kibofu.
Dawa za waganga hospitalini  zinaitwa “blocker” (mzuiaji). Huzuia ukubwa na kuupunguza. Kisayansi ni “Alpha-blocker”....alpha ni neno lenye asili ya Kigiriki linaloimanisha mwanzo. Alpha na Omega. Mwanzo na mwisho. Kazi ya Alpha Blocker ni kuzuia homoni ya kiume (“testestorone”) inayobadili hali mwilini kuwa “dyhrotestorone”...yaani athari mbaya.
Pili ni miti shamba na vyakula. Wamerakani wanayo “Saw Palmeto” mathalan. Inauzwa maduka yote ya afya nchi zilizoendelea. Vyakula kama nyanya, upupu, maparachichi, mboga ya kitimiri (“Parsley”) na mboga nyingine za majani (saladi mbichi). Karibuni, nyanya imesifiwa sana kwa afya ya tezi ya uume.
Matunda, vile vile, kwa wingi na kulala muda unaotakiwa (saa 8 kwa watu wazima)  ni baadhi ya mambo asilia yanayoweza kuhudumu afya. La mwisho.
 Muhimu kwenda kukaguliwa na mganga kila mwaka ukishafikisha miaka 50.

-London, 11  Novemba , 2014
               

No comments:

Post a Comment