Sunday, 30 November 2014

VITA DHIDI YA KULAWITI NA KUBAKA WATOTO VYAWAKA MOTO UZUNGUNI
 Leo tuzungumzie watoto. Tuangalie afya, mapenzi na usalama wao. Hakuna kipindi cha historia yetu wanadamu ambapo watoto wanafanyiwa  unyama duniani kama sasa.
Mwezi Machi,  Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto (UNICEF) lilisema tangu vita vianze Syria,  watoto 10,000, wameuawa  makusudi. Wengine milioni tano hawana makazi maalum.  Mauaji haya yanafanywa  majumbani,  mashuleni, mitaani na  kambi za wakimbizi. Watoto wanapigwa risasi makusudi na magaidi wa Boko Haram, Nigeria. Miezi miwili sasa wasichana  200 waliotekwa mkuku na wanaharam hawa (wanaotumia dini kama ngao ya uyahawani wao) hawajapatikana. Kila kukicha watoto vijijini na mashuleni Nigeria wanauliwa bila hatia yeyote.

  Wiki iliyopita mtoto wa Kipalestina, Tarik Abu Khdeir, mwenye miaka 15 alipigwa na askari wa Kiyahudi jimbo la West Bank nusura afe. Alipokuwa akiongea na wanahabari uso mzima ulikuwa umemvimba utadhani kaota vichuguu vya mchwa. Kipigo kilifuatilia mgogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi. Watoto watatu wa Kiyahudi walikokotwa njiani wakakutwa wamefariki kitongoji cha Wapalestina. Serikali ya Israel ilidai Hamas iliwaua. Ili kulipiza kisasi mtoto wa miaka 16 wa Kipalestina, Mohammed Abu Khdeir, naye aliburutwa barabarani , akapigwa kikatili na kutupwa msituni kama fuko.
Ingawa waliohusika wameshakamatwa na askari wa Israel, haisaidii kurudisha maisha ya watoto.
Barani Afrika, nchi zenye vita mathalan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan na Kongo, unyanyasaji wa watoto ni jambo la kawaida. Umoja wa Mataifa umekadiria asilimia 65 ya ubakaji uliofanywa Kongo kipindi cha miaka 15 iliyopita uliwaathiri watoto. Asilimia kumi ya watoto waliobakwa Kongo wana umri chini ya miaka kumi! Mbali ya kubakwa, kupigwa au kulawitiwa watoto hulazimishwa kubeba mizigo na kuwa askari.
Kwetu Tanzania mateso ya watoto- kwa njia mbalimbali- yamefikia daraja la kishetani kwa taifa hili lenye utamaduni  mahsusi wa amani. Juma lililopita msichana wa kazi za nyumbani, ambaye jina lake halikutajwa (aliitwa tu “Hausigeli”utadhani kijiti au kifuu cha nazi) aliteswa miaka miwili na tajiri wake, Boko, Kinondoni. Picha za mwajiri huyo, Yasinta Rwechengura, akisindikizwa na askari mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Ulaya ya Kinondoni, ziko sambamba na msichana anayebubujikwa damu kichwani na kifuani; bado kigoli.  Mateso ya watoto wanaofanya kazi majumbani  hayasemeki. Kwa kuwa hawana midomo, haki au cha kuwatetea, hali zao hazifahamiki.
Baadhi ya maoni ya wasomaji wa  “Global Publishers” la Bw Eric Shigongo, yanadhihirisha huruma na mshangao wa wananchi kuhusu mtoto huyo wa kazi.  
“Huwezi  kumtesa binadamu mwenzio kiasi hiki hata kama amefanya nini, unampiga kama mwizi, lahaulaa. Ilhali yeye ndiye anayeangalia nyumba yako?”
Au
“Yaani ukatili  mwanamke unamfanyia mtoto wa mwenzio hivyo au hujawahi kuzaa hujui uchungu? Huyu ni sawa na muuaji hukumu yake ni kifo tu. Je kama ni mtoto wake  alifanyiwa hivyo angejisikiaje?”
Hali inadhirisha ukosefu wa utu na ubinafsi ulioenea leo.
Labda tutasema unyanyasaji huu ni wa waovu wachache tu. Lakini je, watu wazima wenye nafasi zao wanaolala na kuwalawiti  watoto kisirisiri?
Hapa Uingereza mwaka mzima sasa tetemeko la ardhi la habari linaendelea kufichua visa vya watu mashuhuri waliowalawiti au kuwabaka watoto.
Mosi alikuwa Jimmy Saville. Mstahiwa alikuwa mtangazaji mashuhuri wa BBC aliyependwa na mamilioni kiasi ambacho hakuna hata mtu mmoja aliyemkisia mabaya. Jimmy Saville na sigara lake kubwa, nywele nyeupe zilizofanana na katani,  miwani mekundu juu ya pua nene  iliyompa sura ya majigambo na vichekesho alifariki mwaka 2011 akiwa na miaka 84. Baada tu ya mazishi malalamishi na mashtaka zaidi ya 200 yalifanywa na wanawake na wanaume waliodai aliwafanyia uanaharamu wakiwa watoto lakini enzi hizo sheria iliziba masikio. Hawakusadikiwa.
 Wengine wanne walidai aliwachezea wakiwa na miaka kumi. Kutokana na umaarufu wake alipewa ufunguo akaruhusiwa kuingia mahospitalini kutumbuiza wagonjwa ambao aliwanajisi na kuwafanyia uchafu. Aliingia vyumba vya vilema na maiti. Karibuni madai yameongeza kusema Bwana Saville alihusudu kulala pia na maiti. Alifanya vituko hivi toka mwaka 1964 !
Baada ya habari za Jimmy Saville kuzagaa, watu wengine maarufu wanaendelea kushtakiwa. Wiki jana mwanamuziki na mchoraji  aliyetunukiwa taji la heshima na Malkia na kuitwa Sir Rolf Harris, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia 12 za kulala na watoto. Madai yanasema Bwana Harris mwenye umri wa miaka 84 alianza ufuska wake miaka 40 iliyopita. Tarakilishi au kompyuta zake zilikutwa na picha zaidi ya 200 za watoto wadogo wakiwa uchi.
Wakati mashtaka yakiendelea serikali imetangaza mabomu mawili. La kwanza lahusu viongozi serikalini.  Mwaka 1983 enzi za uongozi wa marehemu Margaret Thatcher uchunguzi uliofichua ulawiti na ubakaji wa watoto ndani ya mashirika makubwa ya hospitali, BBC na serikalini ulizimwa. Aliyepewa  mafaili ya uchunguzi Bwana Leon Brittan, tajiri- mbunge na Waziri enzi hizo- inadaiwa aliyaharibu mafaili ya mashtaka. Wiki jana serikali iliamuru uchuguzi ufanywe na maofisa saba wa polisi wameteuliwa kuusimamia.
Bomu la pili ni ukeketaji. Alhamisi  Julai 3, Serikali ya Uingereza
iliwaamuru waganga, waalimu na wafanyakazi  wa taasisi za umma kutotetereka kuzuia ukeketaji eti kwa sababu za kitamaduni. Toka sheria ilipopitishwa kutokomeza desturi hii  mwaka 1985 hakuna aliyeshtakiwa hadi mwaka huu.
“Ukeketaji ni uhalifu. Si suala la kikabila  bali utesaji. Si jando unyago bali unyanyasaji.” Kamati husika ya Wizara ya Uhamiaji ilitamka. Baraza la Waislamu Uingereza nalo lilitoa taarifa iliyopinga vikali ukeketaji na kusema Uislamu hauafiki kitendo hicho.
Wenzetu wameamua vita kutetea watoto.
Je, sisi Afrika?
Ukeketaji, ubakaji na kulawiti watoto vinaendelea kisirisiri (na wazi)  mijini na vijijini Tanzania. Sababu kuu ni umaskini na watoto wengi kutokwenda shule. Watoto kulazimika kulala nje au kuishi maisha ya dhiki. Pili, woga umeenea. Wahusika hawasemwi. Vyombo husika - vya kidini, kijadi au kiutawala- huficha au kutumia mabavu kuuzima moto.
Karibuni nimeelezwa kisa kilichotokea Tanzania. Mzee aliyekuwa na tabia ya kulala na watoto wadogo- wasichana kwa wavulana- akiwapa peremende na vijisenti alishikwa (kama mwizi) lakini akawahonga wahusika. Hawakumpeleka polisi. Walimwachia. Swali ni je, wale watoto aliowadhuru wataendeleaje na vidonda kimwili na kisaikolojia?  Tuendelee na mada juma lijalo.
               

No comments:

Post a Comment