Sunday 30 November 2014

MJADALA WA MADHARA YA UVUTAJI BANGI WAPAMBA MOTO UINGEREZA




Bangi.
Neno lenye maana na majina mengi. Marijuana. Cannabis. Sigara kali.  Spliff. Kaya. Na kadhalika. Kwa Kiswahili asili ya neno “bhang” ni Kihindi. Sina hakika kama zamani kabla ya ujio wa wageni tulilienzi jani hili. Jani lililo mkebe mmoja na “kunguni” wa dawa za kulevya. Heroin. Unga wa Cocaine. Na mengineyo.  Dawa zinazomgeuza mwanadamu dude, afriti,  mahoka,  jambazi. Dawa zenye uwezo wa kuharibu  jamii  kama ilivyo Mexico sasa hivi. Unabisha? Ingia, You Tube.
Uuone uhayawani wa dawa za kulevya ulivyoshawabadili wanadamu   mafisi. Kuwapeleka wake, mabinti na dada za majambazi wenzao mwituni kuwafyeka shingo na mashoka. Tunaambiwa magaidi wa ISIS huko Syria na Iraq, hukata shingo. Mexico hukatakata mwili vipande vipande  kisha wakaviacha viozee vichakani mithili ya vinyesi.
Hebu tafakari  ufisi kama huu ujipenyeze Tanzania. Ndiyo mwisho. Hatuna tena nchi ya amani wala kuingia mitaani wikiendi kula nyama choma; kuzamia misikitini, jamatini au makanisani. Ni harufu ya damu kila mahali. Ulaghai kwisha kazi. Hamnazo.
Sasa bangi...

 Katika miaka arobaini iliyopita wanamuziki dunia iliyoendelea wameiremba bangi kama asusa, starehe, ubabe,  nk. Miaka ya Sitini bendi za Kizungu zilisisimka na utamaduni mzima ukaitwa Flower Power- nguvu ya maua. Matamasha mashuhuri mathalan, Woodstock (1969), Marekani yaliitukuza. Kuanzia hapo vifo vya wanamuziki maarufu vikawa “kawaida”.... Miongoni mwao-  mpiga gitaa mkali kuzidi wote - Jimi Hendrix (27), mwimbaji Janis Joplin (27) na Jim Morisson (27) aliyeongoza bendi ya The Doors.  Vijana  hawa wenye vipaji tosha, walifariki kipindi cha 1970 na 1971. Karibuni, 2011 mwimbaji wa Kiingereza Amy Winehouse, naye alititigwa kwa ukunguni  huu akiwa na  miaka 27! Astafurlah.
Awal kabla ya haya, miaka ya 1940 na 1950, wanamuziki waliobobea humo walikuwa  wapigaji wa Jazz. Mfano, Charlie Parker (mpiga Saxafoni babu kubwa anayeigwa hadi leo) alikufa ghafla  1955. Alikuwa na miaka 35 tu, lakini mganga aliyetathmini maiti yake alishangaa  alivyochakaa akaonekana  ajuza  wa miaka 70.  
Muziki wa Reggae toka Jamaica uliovuma miaka ya Sabini, NDIYO ulioiweka bangi mbele ya taswira. Wanamuziki wa The Wailers, Peter Tosh , Bunny Livingstone Wailer  na Bob Marley, walidai bangi ni sehemu ya dini ya Rastafari yenye mizizi Ethiopia. Kutokana na maudhui ya muziki wao uliozungumzia jamii na unyanyasaji, bangi sasa ilipewa hadhi mpya.  Mwaka 1978 Bob Marley alitoa Albam nzima (Kaya) iliyoghani mapenzi, mashairi, siasa na kutukuza bangi.
“Bangi,” aliwahi kusema marehemu Marley, “ni jani linalookoa taifa; ilhali pombe ni uharibifu.”
Basi  uvutaji bangi kama kitu kinachoua, ukageuzwa kheri. Hususan kwa maudhui ya Reggae yenye siasa za kimaendeleo na dini ya Rastafari. Kwamba ukiivuta utauona ukweli wa harakati.
Mwaka 1976, Peter Tosh, alichapuka na Albam kuchangia kampeni ya kuihalalisha bangi kisheria. Jalada la “Legalize It” lina picha ya mwanamuziki huyu -aliyekuwa pandikizi la mtu- akivuta kiko kinafoka moshi wa bangi. Marehem Tosh aliuawa na majambazi nyumbani kwake  (1987). Na alifafanua sababu za msimamo huu  ndani ya mahojiano na gazeti la London, New Music Express, 1978.  Akasema aliamua kutunga nyimbo za kutetea kuvuta bangi na kuihalalisha kutokana na kile alichokiita kuonewa na kunyanyaswa na polisi wa Jamaica.
Baadhi ya maneno ya wimbo “Legalize it”  hudai:
“Ihalalishe.
Waimbaji wanaivuta,
Wapigaji vyombo pia,
Madaktari wanaivuta; wauguzi; mahakimu .
... Usiikosoe. Ihalalishe
Ni nzuri kwa mafua, pumu,  kifua kikuu
Ndege wanaila, mchwa na sisimizi wanaipenda
Mbuzi hupenda kucheza nayo...”
 Marehemu Peter Tosh akiwasha bangi. Picha ya mtandaoni...

Kitaaluma, ziko aina tatu za jani la bangi : Cannabis Sativa, Cannabis Indica na Cannabis Ruderalis. Cannabis Sativa na Indica ndizo huvutwa zaidi; ilhali Cannabis Ruderalis (yenye miti mifupi, na inayolimwa  nchi za baridi kama Urusi) hutengenezea dawa.  Katika miaka 30 iliyopita watetezi wa bangi wamepigania kuhalalishwa kwa bangi kijumla.
Baadhi ya jamii zimeiruhusu. Kiongozi ni Uholanzi ambapo bangi huuzwa katika mikahawa na vitafunio vingine. Mji  wa Amsterdam hutembelewa na watalii wengi kutokana na “uzuri” huu. Baadhi ya majimbo ya Marekani mfano Colorado yamepata kibali cha kulima na kuuza bangi kama dawa kwa wagonjwa wenye maumivu makali na wavutaji holela.
Nchini Uingereza kampeni imepingwa sana. Hapo hapo imetetewa na baadhi ya  wanasiasa na matajiri mathalan mwanamuziki Sting, mchekeshaji Russell Brand, mwandishi Wil Self -ambaye vitabu vyake vimetafsiriwa  lugha 22 -na mfanyabiashara milionea, Richard Branson anayemiliki ndege za Virgin.
Dhana imepingwa lakini si kwa ushahidi kama juma hili.
Mtafiti na mtaalamu wa chuo kikuu cha King’s College London,  Profesa Wayne Hall alisema madhara ya bangi ni makubwa kuliko faida.  Profesa Hall ambaye ni mshauri wa shirika la Afya Duniani (WHO)  kasimamia utafiti yakinifu wa miaka 20 na kufikia hatima ifuatayo.
Kwamba kiasi kikubwa cha vijana chini ya miaka 20 wanaovuta  bangi  huanguka darasani, hupungikiwa uwezo wao wa kufikiri na hatimaye kuitegemea kwa kila kitu. Ni kama ulemavu.
Kwamba ukishakuwa sugu wa bangi utataka vikali zaidi!
Kwamba bangi inaongeza hatari za kuwa mwenda wazimu kwa maradhi kama “psychosis” (kupoteza hisia za hali halisi) na  “schizophrenia”. Maradhi ya “schizo” humfanya mhusika kusikia kelele au sauti kichwani. Kelele hizo humtoa mhusika katika ukweli wa mambo na kumjengea njozi za kila aina. Baadhi za kuua.
Kwamba kina mama waja wazito wanahatarisha maisha ya watoto,  tumboni.
Kwamba ni rahisi kwa madereva waliovuta bangi kusababisha ajali hasa wakiongezea pombe juu.
Fikra za Profesa Hall zilizotangazwa na magazeti makubwa Uingereza zimesabisha zogo kali. Wavutaji wengi Majuu ni watu wanaojiweza.
Je, kwetu ambapo wavutaji ni maskini, vijana wasio na elimu au ajira maalum?  Uzunguni maradhi ya akili hutafutiwa tiba na serikali ina idara na mifuko maalum ya kuhudumia wasiojiweza. Je, kwetu kusikokuwa na “starehe” hii ya kusaidiwa? Je, serikali zetu nchi changa zitapata wapi muda wa kuhudumia walevi wa dawa za kulevya badala ya kuelemisha kiasi kikubwa cha wananchi wanaohitaji mabadiliko ya maisha yao?  Ushauri mmoja tu. Kwako Mwafrika. Achana na bangi.  

 Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili Oktoba 12, 2014







No comments:

Post a Comment