Wednesday, 9 November 2011

SANDUKU YATIMA NA SAFARI YANGU DODOMA KUELEKEA ARUSHA

Nilipokua nikiulizia basi la mikanda  Dodoma mjini;  jamaa mmoja akanicheka:
“We siku yako ya kufa ikifika utakufa tu…”
Na mimi pia  nikacheka nikikumbuka manabii walioandika maneno ya Mungu. Ndani ya sura ya saba ya Biblia mlango wa Mtakatifu Matayo tunashauriwa :
“Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea ; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.”
Niko Dodoma.
Nnasubiri kukata tiketi ya basi nielekee zangu mikoa ya kaskazi.
Uvaaji mikanda ndani ya magari bado unapuuzwa sana kwetu Afrika na nchi zinazoendelea...
 Baada ya kuzoea kuyapanda mabasi ya Kizungu niko kwetu Bongo nikizozana na itikeli, itikadi na desturi kidogo tofauti ambazo ingawa nilizaliwa na kukua nazo naziona kiasi fulani ngeni, za kutisha. Watanzania wenzangu wanakubali tu lile linalotokea na litokee. Mstari huo umezoeleka  kana kwamba Mtanzania anadhani maisha yake hayana faida tena; liwalo na liwe. Ni kama keshakata tamaa; ari ya mapigano inaanza kumnyauka; hana moyo.
<--more--!>
Kuwepo mabasi yenye mikanda ni jambo la kufurahia; ila nauli ya mabasi haya ni kubwa zaidi ya yale yasiyo nayo. Tena yashangaza kwamba mabasi haya haya ya mikanda ambayo pia huendeshwa kwa mwendo wa tahadhari zaidi ni ya bei kubwa.
“Wengi hutaka ya haraka haraka ili wawahi safari,” naambiwa.
Kitakwimu mabasi yanayopinduka zaidi ni yale yanayokwenda haraka. Kufuatana na Utafiti uliofanywa kimataifa uvaaji mikanda ndani ya magari husaidia kupunguza majeruhi wakati wa ajali. Hii ni sababu ya migongano na mibingiriko kupunguzwa na mikanda hiyo.
Ah….
Nimeshakata tiketi; nimekaa.
Nawaangalia wasafiri wenzangu wengine wakiingia kwa makeke na masumbuko. Kuna msela kaingia na sanduku akaliweka kitini kisha akatoweka. Naliangalia sanduku lile kwa karaha. Abiria wengi wanaopita pita hawaliangalii. Baada ya kama robo saa bado lile sanduku li kitini. Moyo uko mdomoni…
Nawaangalia abiria wenzangu. Hakuna hata mmoja anayeshutumu uwepo wa sanduku hili yatima.
Baada ya nusu saa sasa basi linatoka Dodoma  (ya vumbi  na upepo mkali )tukielekea lami itakayotuelekeza mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga.
“Vipi lile sanduku la nani?” namuuliza mkaguzi wa tiketi.
Badala ya kugutuka ananiambia nisubiri kidogo maana kuna mama mmoja kule nyuma anadai kuna mtu kachukua kiti chake.
“Tiketi nilishakata !” anafoka mama.“Nafasi yangu siioni!”
Bado naliangalia lile sanduku.
Mawazo yangu yamerejea London.
Mauaji ya mabomu yanayosambazwa na magaidi kwa magari nchini Iraq yamekuwa jambo la kawaida siku hizi. Taswira hii inayomwonyesha jamaa akimbeba mtoto aliyeshateketezwa, ilipata tuzo la picha bora iliyopigwa na mwanahabari, Carlos Barria wa Reuters, Februari 2007.

 Nimezoea kule Uzunguni ukiona sanduku au mfuko umewekwa sehemu bila mwenyewe unatakiwa mara moja umuarifu mkaguzi (kama huyu) au upige simu afriti, polisi. Tahadhari hii inatokana na uangalifu Wazungu walioshakuwa nao kuhusiana na mabomu na harakati za ugaidi dunia ya leo.
Mara ya mwisho Watanzania kukukumbwa na tufani la ugaidi ilikuwa mwaka 1998, wahasimu wa Al Kaida walipotegesha mabomu yao ubalozi wa Marekani , Nairobi na Dar es Salaam. Mtoto aliyezaliwa mwaka 1991 ambaye wakati huo alikuwa na miaka saba kama leo ndiye mmoja wa abiria atakuwa na miaka 20. Sidhani anafikiria sana suala la mabomu ya Al Kaida, mijini Nairobi na Dar es Salaam. Ila kwa wazee na watu wa makamu kama miye lile litakuwa jambo lililotokea juzi kushinda jana …
Abiria wenzangu wala hawastuliwi kuwepo kwa kijisanduku kile. Kila mmoja anashughulika na mizigo yake; akitafuta sehemu ya kukaa. Wapo wanaosoma magazeti; yupo aliyetegesha redio masikioni; sina hakika kama anasikiliza mpira wa Simba na Ruvu (ambapo matokeo yalikuwa mabao 2-0)…sina hakika kama abiria wenzangu wanafuatilia habari zilizoshatangazwa kuhusu majeshi ya Kenya kushambulia wapiganaji wa Al Shabab mpakani kwao na Somalia. Kwamba Al Shabab sasa hivi ni kikundi hatari sana Afrika Mashariki. Kwamba magaidi hawa washateka mabomu mjini Nairobi na Kampala; na kwamba ingawa waliouawa ni majirani zetu; ukiona kwa mwenzako kunaungua moto anza na wewe kutafuta maji. La hasha.
Basi linaendelea kukitoa…
Baada ya vituo kadhaa anaingia mwanamke mwembamba aliyevalia suruali nyeupe ya kubana na fulana inayoonyesha kila aina ya haiba yake.
“Hili sanduku la nani?” Anauliza akiangaza macho upande wangu.
“Hata miye nataka kujua.” Namjibu.
Mkaguzi anakuja.
“Sanduku la nani hili jama?”
Hakuna jibu.
Kinachoendelea kunipumbaza ni namna abiria wenzangu wengine wasivyoshtuka. Hili lingekuwa bomu la wana Al Kaida au Ala Shabab saa hizi tungeshageuka majivu na masizi.
Mwanamke yule aziza  analiinua sanduku bila tuhuma (niliyokua nayo) analiweka pembeni; utadhani andazi tu. Miye moyo unanidunda.
Mkaguzi analiangalia sanduku sasa si kwa ile aina ya kero niliyokuwa nayo mimi bali kwa hisia nyingine. Kwamba sanduku limechukua nafasi ya wateja.
Basi hilo linachuna mbuga za Bongo.
Sanduku liko kando; msichana yule mzuri keshakaa sasa anatazama sinema iliyowekwa mbele ya basi na dereva. Muziki wa Bongo Fleva unarindima;
“Kila siku vitu vinapanda bei!”
Wimbo unasindikizwa na mbwembwe na harara zake Blad Key, mmoja wa wasanii ambao sikuwahi kuwasikia nikiwa Uingereza.
Kila siku vitu vinapanda bei !”
Basi hili lisilokimbizwa; linaendeshwa kwa mwendo mzuri usiotisha.
Na ingawa lina mikanda; sioni asilimia kubwa ya abiria  wakiwa wameivaa. Ni kama mapambo tu. Kinachowafurahisha wapambe zaidi ni zile sinema, tamthiliya na muziki unaoonyeshwa ndani yake. Tunapofika Morogoro mkaguzi anatutahadharisha kubeba mifuko yetu kutokana na kile anachokiita wezi wanaojaribu kujipenyeza ndani humu wakijifanya wasafiri, saa abiria wakiwa nje wakila.
Ni wakati huu ndipo mwenye sanduku anajitambulisha. Kumbe alikuwa kiumbe yule aliyekuwa akisikiliza mpira wa Simba na Ruvu katika simu. Mpira umemchota ilhali wengine tumekuwa tukihaha.
Ndiyo Bongo hiyo.
Gari letu linapovuka Pwani kupitia daraja la mto Wami kuelekea Korogwe nayasoma mabango mbalimbali juu ya mabasi mengine yakinidhihirishia fikra hizi za kusubiri ubaya uje bila kuukabili:
BWANA NDIYE MCHUNGAJI WANGU…
ALLAH WAAKBAR.
Wakati basi likiendelea; ghafla imewekwa video ya wanawake watatu . Video ile toka Marekani ya Kusini (muziki na lugha inayozungumzwa ni Kispanyola) inawaonyesha majike yakikatika viuno, sidiria zikichomolewa wazi; sehemu za siri nje; bila soni. Namwita mkaguzi.
“Vipi bwana huoni ndani ya basi mna watoto wadogo na akina mama wanaonyonyesha?”
Anashtuka.
“Kumradhi bwana. Dereva kapitiwa kidogo.”
Anapoiondoa ile video baadhi ya abiria wanakasirishwa. Wanauliza dereva ana ugomvi gani na ile video(ingawa ya matusi)?
Ama kweli Bongo hii; nchi yetu tukufu.


Ilichapishwa Mwananchi, 30 Oktoba, 2011 :
http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/20-uchambuzi-na-maoni/17013-kutoka-londonsanduku-yatima-na-safari-yangu-ndani-ya-bongo

No comments:

Post a Comment