Nilipokua nikiulizia basi la mikanda Dodoma mjini; jamaa mmoja akanicheka:
“We siku yako ya kufa ikifika utakufa tu…”
Na mimi pia nikacheka nikikumbuka manabii walioandika maneno ya Mungu. Ndani ya sura ya saba ya Biblia mlango wa Mtakatifu Matayo tunashauriwa :
“Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea ; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.”
Niko Dodoma.
Nnasubiri kukata tiketi ya basi nielekee zangu mikoa ya kaskazi.
Uvaaji mikanda ndani ya magari bado unapuuzwa sana kwetu Afrika na nchi zinazoendelea...
Baada ya kuzoea kuyapanda mabasi ya Kizungu niko kwetu Bongo nikizozana na itikeli, itikadi na desturi kidogo tofauti ambazo ingawa nilizaliwa na kukua nazo naziona kiasi fulani ngeni, za kutisha. Watanzania wenzangu wanakubali tu lile linalotokea na litokee. Mstari huo umezoeleka kana kwamba Mtanzania anadhani maisha yake hayana faida tena; liwalo na liwe. Ni kama keshakata tamaa; ari ya mapigano inaanza kumnyauka; hana moyo.
<--more--!>