Sunday, 27 November 2011

MACHALARI MGOMBANI MOSHI NA NYAMA CHOMA ZA ARUSHA


Dunia yetu ina kila aina za udongo.
Udongo wa Mpirani nje kidogo ya Moshi mjini unanikumbusha wa Kigoma ambapo rangi yake inakurubia wekundu. Mimea ya Mpirani ni migomba, mapera, machungwa, ndimu, maembe, kahawa na gari analoendesha dada yangu Juliana linakwenda taratibu, likikwepa mashimo shimo ya udongo huu.


“Unaona ule msikiti?” naulizwa. Nikiwa mdogo haikuwepo misikiti mashambani Moshi.  Kidesturi migombani kwa Wachagga hujazana makanisa.
“Wapo mangi wengi Waislamu siku hizi,” dereva anafafanua.
<--more--!> 
 Tumeshachomezea kwa mmoja wa mama zangu ambao sijawaona miaka si haba. Gari linasimama katikati ya migomba. Ua uliozungukwa kwa Masale rangi chanikiwiti kilichokolea (yanayoheshimiwa kimila) una zizi la ngo’mbe wanaouguna mooooo utadhani wameletewa nyasi toka London.
 Baada ya mazungumzo marefu muda wa kula umewadia. Meza imepambwa ndizi mbivu za kisukari, nyekundu za Kiganda, mnanambo na mchare. Ndizi ni zao la kifalme lenye matumizi kochokocho.
 Majani ya ndizi hufungia au kupikia vyakula; yakikauka yaweza kuunda magodoro au viti, kuezeka nyumba pia kuwasha moto. Mbali ya kuliwa mbivu au kuchomwa, hupikwa kwa nazi au nyama zikawa Machalari ; zikipondwa kama uji  ni Mtori; zikitayarishwa na maharagwe na magadi hugeza Kiburu au Ikato; pamoja na mahindi zinakuwa Ngararumu; zikichanganywa na ulezi ni pombe mashuhuri ya Mbege; zikiungwa kwa maziwa zawa Kitawa ambacho kawaida hupewa kina mama waliojifungua ili wawakirimu vizuri wanao.  Mama yangu huyu kazichemsha ndizi kisha akazioka. Pembeni mna mboga ya kisamvu. London hupatikana mihogo ila kisamvu adimu. Kando sahani  la nyama.
kahawa...kinywaji kinachopendwa ulimwenguni

“Karibu ndafu,” naambiwa kwa Kichagga.
Ulaji wa chakula huturejesha pango la utamaduni na desturi. Ninapotembelea ndugu na jamaa mbalimbali Moshi na Arusha inanidhihirikia kuwa Tanzania yetu leo si kweli taifa la viazi vya kukaanga. Chips ni chakula kilichovumbuliwa na Waingereza karne ya 19. Viazi vilivyookwa na kuliwa kwa samaki vilitajwa mara ya kwanza na mtunzi maarufu wa hadithi za Kiingereza Charles Dickens, mkazi wa London mwaka 1838; ndani ya riwaya maarufu inayoelezea hekaya za mvulana yatima, Oliver Twist.
Chips zipo mikoa hii ya kaskazi, ndiyo; walakin ndizi zimetamalaki zaidi. Manispaa hodari ya Moshi  imejitahidi kusimamia mji huu ukazidi Tanzania, Afrika Mashariki na ya Kati yote kwa usafi.
“Ukitupa takataka ovyo Moshi; faini shilingi elfu 50,” naelezwa na wenyeji.
Mbuzi wakila taka zenye miozo ya kila aina ikiwepo kizaazaa cha plastiki katika moja ya majaa yaliyozagaa miji yetu Bongo...

Kutokana na msimamo thabiti wa manispaa hii nadra kuwaona mbuzi wakirandaranda ovyo; wakichakura chakura majaa ya taka kama sehemu nyingi Bongo ambapo viumbe hawa wanaohusudika kwa mishikaki hula hadi makaratasi ya Plastiki. Hata Nguruwe hafui dafu kwa ulafi...
Nakodisha gari kwenda kwetu kijijini mlimani.  Nikiwa mtoto tulitumia pia Landrover kwenda na kurudi mjini.
Gari hili la Mwingereza lililoanzishwa mwaka 1947 leo linamilikiwa na kampuni ya Kihindi, Tata Motors. Landrover na Jeep (la Mmarekani) ndiyo magari ya kwanza duniani yaliyovumbuliwa kupambana na barabara zenye ardhi iliyoelemewa kwa makorongo, matope, barafu, vijiwe na mashimo. “Jeep” zilijaribiwa mwanzoni na majeshi ya Marekani vita vya pili vya dunia. Zilipofaulu mtihani zikaigwa na watengenezaji wengine hususan Wajapani waliounda Toyota na Prado zinazowezana na barabara vururu  za Bongo.
Toka uchumi huria uote matawi baada ya Mwalimu Nyerere kujiuzulu 1985, Watanzania wasio wachochole wameagizia  mashine hizi za kisasa kwa kasi, huku barabara zetu zikichelewa kupanuka. Wingi wa magari na miundo mbinu haviendani na miji inayokua upesi. Inasikitisha kwamba magari moshi yaliyokuwa yakirahisisha usafiri wa mbali Tanzania miaka 40 iliyopita hayatumiki tena. Matreni ya haraka yaliyoshtadi nchi zilizoendela, kwetu wala hayajulikani. Safari inayochukua  saa moja kwa gari moshi la haraka Majuu, kwetu Bongo hubidi nusu siku kwa gari. Ndiyo moja ya sababu mabasi kupinduka ovyo kutokana na madereva wanaojaribu kuharakisha.
 Landrover linanipeleka Mgombani nilikokulia; mlima Kilimanjaro (ambao kiasili uliitwa Kilema Kyaro) uleee... unatukodolea.
 Tunaanzia Kiboriloni ambapo viduka vyake vile vile toka nilivyoviacha ujanani. Tunapenyezea Maringenyi tukilisikiliza Landrover ikipigana na ardhi kahawia kibichi ya mashimo na vumbi, tukielekea Mlimani. 

 Ardhi na njia ziko vile vile ila leo kuna nguzo za kupitishia umeme hadi kijiji cha Mori. Nyumba za makuti na nyasi siku hizi hamna; nyingi ni za mabati hata vigae. Shule niliyoanzia chekechea Tela mwaka 1961  (wakati wa Uhuru) hadi 1965, ingalipo na mmoja wa waalimu hapa ni mke wa jirani yangu nliyesoma naye enzi hizo.  Mashamba ya Mori yamestawi mafenesi,  mananasi, maparachichi na tunda liitwalo Elimu. Kila pahala ulimwenguni huwa na tunda ambalo nadra kuonekana kwingineko. Zabibu za Dodoma, shoki shoki za Zanzibar, mitufaa ya Ulaya, kiwi ya New Zealand na elimu hapa Kilimanjaro.  
Ninapokwea basi la Arusha mechi zile zile.
Mbuga za wanyama  kama hii niliyotembelea kwa huduma za Greenshank Adventures zingali moja ya nguzo kuu za uchumi wa Arusha. Mji huu unapanuka haraka na umeanza kuwa na taswira ya KiNairobi, Nairobi kwa kila hali mbaya na nzuri...

 Tofauti  ya miaka 30 iliyopita ni kwamba leo mabasi mengi. Barabara kuu ya Arusha ni ile ile; vituo hivyo hivyo: Sadala, Sanya Juu, Usa River, Makumira,  Kimandolu, nk. Yanakwenda kasi na ukiniacha miye, mwingine aliyevaa mkanda ni dereva tu. Si ajabu baadhi ya madereva wetu huwa hawafi ajali zinapotokea. Tunapowasili Arusha ni machwea jua; wamachinga na wauzaji bidhaa “vyangu vyangu” mbio mbio wakiharakatika. Wananikumbusha miji ya Rio, Nairobi na Kingston, Jamaica ambako juhudi za uhai ni mchezo wa dama na karata  kuikidhi tumbo.
Siku moja tuko Sakina kando ya barabara kuu inayolengeshea  Namanga hadi Nairobi. Pana mingurumo mikali ya malori na watu wakifanya kila aina ya biashara.
Basi lenye bango linaloshabikia timu maarufu ya Chelsea...
 Mwaka 1900 miji duniani ilikuwa na asilimia 14 tu ya wakazi; mwaka jana idadi iliongezeka hadi asilimia 50; na Umoja wa Mataifa umetabiri ongezeko la asilimia 70 ifikapo 2050. Maisha ya mijini yana ahueni kifedha na kielimu ila kiafya, utafiti wa Umoja wa Mataifa ulieleza wiki jana, ni mazingira ya maradhi ya mioshi ya magari, viwanda, vumbi na petroli.
“Vipi London kuna nyama choma?” Naulizwa na bwana aliyeshauchapa.
 Ukitaka mishikaki kama ya Arusha inayoletwa na kachumbari kwa malimau itakubidi uitengeze tu nyumbani kwako, London. Moja ya sababu za uhaba huo ni kutokana na Wazungu wengi kutokuwa washabiki wakubwa wa nyama. Hawapendi namna wanyama wanavyofugwa kimateso ili wakue haraka, kuchuma pesa. Matokeo nyama Uzunguni si tamu kama Afrika.

Ilichapwa Mwananchi, Jumapili, 27 Novemba, 2011:
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/17876-kutoka-londonmachalari-ya-moshi-nyama-choma-za-arusha

No comments:

Post a Comment