Monday, 18 July 2011

GAZETI MAARUFU NA ZEE KUSHINDA YOTE DUNIANI LILIVYOTINGISHA SERIKALI NA MAISHA UINGEREZA...

Habari zilizotanda Uingereza majuma mawili yaliyopita zimehusu gazeti maarufu la News Of The World. Lilifungwa wiki jana baada ya  mashtaka ya uhalifu. News of the World ilikuwa ikipata habari kwa kuingilia barua pepe na simu za watu maarufu ili kuwaiba. Miongoni mwa waliokuwa wakifanyiwa wizi huo ni Malkia Elisabeth, mwanae Prince Charles, Waziri Mkuu wa zamani Gordon Brown, viongozi mbalimbali na wacheza mpira mashuhuri. Mwishoni  gazeti liliwaudhi wananchi zaidi ilipofahamika lilikuwa limekita makucha yake kusikiliza habari za watu waliouliwa au kufa. Kati yao ni wasichana watatu waliouliwa kinyama Milly Dowler, Jessica Chapman, Holly  Wells na ndugu za waliofariki Julai 2005 kutokana na mabomu ya magaidi  mjini London.
Suala la  kutafuta habari hata za maiti lilikuwa kilele cha uhalifu na gazeti lilifungwa na mwenyekiti wake Rupert Murdoch.
Mzee Murdoch na mkewe mzawa wa China,Wendi Deng, aliyezaliwa mwaka 1968...
Picha ya Gettys...
<--more--!>

Bilionea Murdoch ni miongoni mwa watu wenye nguvu sana duniani. Alizaliwa Australia 1931 na kununua News of the World (na magazeti mengine, ikiwemo The Sun)  mwaka 1969. Alianza shughuli za vyombo vya habari zaidi ya miaka 60 iliyopita. Ana mali bara Asia, Uingereza na Marekani. Mwaka 1986 alianzisha runinga maarufu ya Marekani iitwayo Fox Broadcasting Corporation (FBS). Kitakwimu FOX na CBS ndizo runinga kubwa  kuzidi zote Marekani.  Mbali na The Sun, News of the World na Times hapa Uingereza alianzisha  runinga maarufu ya Sky mwaka 1989.
Tajiri Murdoch anatawala pia  vyombo vya habari bara Asia. Mwaka 1993 alinunua Star TV toka mfanyabiashara Richard Li aliyekuwa na matatizo ya kifedha kwa dola milioni moja.  Star TV yenye makao makuu Hongkong ina nguvu kuzidi zote bara hilo, ingawa Wachina wamekuwa wakizuia nguvu zake. Pamoja na hayo mkewe Murdoch wa tatu pia ni Mchina (anaitwa Wendi Deng na alizaliwa mwaka 1968). Kifupi himaya yake inahesabika kuwa ya pili kwa utawala wa habari dunia nzima.
Tuangalie News of the World.
Gazeti hili la kila Jumapili lilianzishwa 1843; miaka 168 iliyopita. News of the World ina maana Habari za Ulimwengu. Mtindo wake umekuwa kutangaza mambo ambayo wanahabari wengine hawayapata. Kwa lugha ya kihabari huitwa Scoop(tamka Skuup). Waandishi wa habari siku zote hujaribu kutafuta Scoop; ni ushindani wa kumpa mteja jipya zaidi.
Mwaka 1901, News of The World walikuwa wa kwanza kutangaza kifo cha Malkia Victoria aliyeongoza himaya ya Uingereza kwa kipindi cha mwanzo cha ukoloni wa kimataifa (ubeberu). Malkia Victoria alikuwa maarufu kiasi ambacho sehemu kadhaa za makoloni ya wababe hawa zilibatizwa jina lake likiwemo Ziwa Victoria hapa Afrika Mashariki na Maporomoko ya maji ya Zimbabwe. Kiini cha neno Victoria ni Kilatini chenye maana, ushindi.
Mwaka 1963 News of The World ilifichua kasheshe zilizosababisha kuanguka serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Harold Macmillan,  baada ya Waziri wake, John Porfumo kulala na malaya maarufu Christine Keeler. Mwaka 1984 na 1986 gazeti lilifyatua kashfa  za ngono kuhusiana na  mtoto wa malkia Prince Andrew na mwandishi maarufu wa vitabu Jeffrey Archer waliolala na mashangingi na machangu doa.  Ingawa habari kubwa kubwa zilizotolewa zilihusu wakubwa kulala na malaya pia wanawake mashuhuri walifichuliwa. Dadake malkia, Margaret alitangaziwa barua zake nyeti za mapenzi mwaka 1994.
News of The World haikufukua tu habari za ngono, mahaba, vifo na vita.  Mwaka 2000 msichana wa miaka minane Sarah Payne alipouliwa kinyama gazeti lilianza kampeni ya kutangaza majina ya wauaji wa watoto wanaoitwa “Paedophile” kwa kimombo.
Karibuni gazeti lilitoa habari za wacheza mpira mashuhuri waliokutwa na wanawake nje ya ndoa mathalan, Ryan Giggs, Wayne Rooney na John Terry (Chelsea).
Hulka ya gazeti hili kutoa habari kabla ya chombo kingine chochote ilifanikiwa kupitia njia za kihuni na rushwa. Mathalan mwanzoni mwa juma ilitangazwa kwamba baadhi ya polisi mafisadi walipewa pesa kutoa habari kuhusu Malkia Elisabeth.
 Kitendo hiki kinachotegemea pia simu huitwa “Hacking” na kimesababisha gazeti kufungwa na mmoja wa wahariri wake kushtakiwa.  Ubaya ni kwamba ingawa wafanyakazi 200 wameachishwa kazi mhariri, Rebecca Brooks pia mwanae Bwana Murdoch,  James Murdoch hawajashtakiwa. Lengo la kufunga gazeti na kuwafukuza kazi ni kujizatiti kununua televisheni kuu iitwayo BskyB.  BskyB ni kifupi cha BritishSky Broadcasting ambayo ni runinga ya kulipia.
Kwa miaka mingi bilionea Rupert Madoch ametaka kuihodhi BSKyB. Kwa sasa anamiliki asilimia 30 tu ya BskyB.
Wakati nikiandika makala hii mwanzo wa juma, mazungumzo London yamehusu suala la tajiri Mudoch kuichukua BskyB na kumiliki vyombo vya habari Uingereza na Marekani. Pamoja na utajiri, bwana Rupert Mudoch  anahesabika kuwa mtu wa 13 mwenye uwezo na mabavu duniani. Amekuwa na mahusiano ya karibu na viongozi wakubwa wakiwemo Mawaziri wakuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher (1979-1990), Tony Blair (1997-2007) na leo David Cameroon. Inadaiwa wanasiasa wanamwogopa;  vile  vile kwamba mfanyibiashara huyu anao uwezo mkubwa sana katika uchaguzi wa viongozi wa juu wa serikali mbalimbali za Uingereza.
Kisa hiki kinachoendelea bado kinaonyesha namna mamlaka na uwezo wa habari vinavyoweza kuathiri maisha, siasa, fikra, hisia na uhai wetu.  Moja ya athari za mwanzo mwanzo za kashfa hii ilikuwa makampuni makubwa kukataa kutuma matangazo yake ya biashara katika News of the World. Siku hizi wafanya biashara huwa macho sana pale wanaowafadhili wakikiuka maadili. Mfano mzuri ni namna wacheza mpira maarufu wanavyonyimwa nafasi ya kutangazwa na wafanyabiashara.
 Mcheza “golf” mashuhuri, Tiger Woods alipokumbwa na kasheshe ya kulala na wanawake wengi mwaka jana alipoteza pesa nyingi sana baada ya wafanya biashara kukataa asitumie majina yao kujitangaza. La kuzingatia ni kuwa wanahabari na wafanyabiashara wanapaswa kuheshimu ubinadamu.
Ila  mara nyingi  hayawi...

Ilitoka Mwananchi -Jumapili, 17 Julai...na maoni mbalimbali toka kwa wapambe!
http://www.mwananchi.co.tz/editorial-analysis/20-uchambuzi-na-maoni/13707-kutoka-londongazeti-maarufu-na-zee-kushinda-yote-duniani-lilivyotingisha-serikali-uingereza.html

No comments:

Post a Comment