Sunday, 10 July 2011

SOMO KUTOKA MAISHA NA KIFO CHA MWANAMUZIKI GIL SCOTT-HERON

Je, pana faida gani kusikiliza habari za Mmarekani mweusi Gil Scott- Heron aliyefariki mwezi uliopita? Sidhani wapo Watanzania wengi seuze Waafrika waliomjua msanii huyu aliyetoa albam 15 za muziki na vitabu vitano; vitatu vya mashairi na riwaya mbili alizochapa akiwa bado shuleni. Gil Scott- Heron alipofariki Ijumaa Mei 27 akiwa na umri wa miaka 62, alibeba taji la mwasisi wa muziki wa Hip Hop na “Bob Dylan Mweusi.”
Gil Scott-Heron akitumbuiza na bendi yake "Amnesia Express" ukumbi wa Jazz Cafe, London mwaka 1999. Picha na F Macha
<--more--!>

Ilichapishwa safu ya Kalamu toka London-Mwananchi Jumapili-Juni 18, 2011.
Bob Dylan ni Mmarekani (aliyetimiza miaka 70 karibuni) anayeongoza dunia ya fasihi na muziki.  Dylan alijenga sifa miaka ya 1960 kwa nyimbo zilizopinga vita, ubaguzi wa rangi na ufisadi. Myahudi huyu anayeendelea kuwika na gitaa lake alitunga nyimbo maarufu kama “Blowing in the Wind”, “Like a Rolling Stone” (uliodundwa vizuri na mpiga gitaa stadi, Jimi Hendrix) na “Knocking on Heaven’s Door” (wenye mahadhi ya dini na upinzani wa vita vya Vietnam).
Basi vyombo vya habari vilimbatiza hayati Gil Scott Heron,  Bob Dylan Mweusi. Alikataa kofia hiyo.Taji jingine kubwa zaidi alilovikwa lilikuwa “Baba wa Rapu“ (Godfather of Hip Hop). Alikataa pia taji hili akisisitiza yeye mwanasayansi aliyetafiti asili ya muziki wa Blues.
“Blues” ni fani ya muziki wa Wamarakeni weusi uliochipuka mwishoni mwa karne ya 19. Muziki huo ulioanza kama kilio cha watumwa na wafanyakazi katika mashamba ya miwa na pamba kutaka uhuru (na kumbukumbu za Afrika ) ulielezea visa vya mapenzi, maisha, furaha na majuto. Kifupi Blues kwa Wamarekani weusi ni kama zilivyo ngoma na nyimbo za jadi za Kiafrika. Ukichunguza muziki wa kisasa ulimwenguni utagundua una mizizi katika Blues na Ngoma za Kiafrika. Mseto huu umezaa mitindo kadhaa ya Jazz, Rock and Roll, Reggae na  Rhythm and Blues, ambayo wengi huita R n B. Ni kutokana na R n B ndipo ikazaliwa Hip Hop ambayo hapa Afrika Mashariki huitwa Bongo Flava. Gil Scott Heron alivikwa taji la “Baba wa Hip Hop” namna alivyochanganya fani za Jazz, Blues na ujumbe  mzito ulioonyesha machungu ya maisha ya Wamarekani weusi. Waliomvika walikuwa wakimsifu kutokana na msimamo wa kazi zake.
Turudie swali letu. Je iko faida gani kuyajua maisha ya Mmarekani huyu? Kuyajua maisha yake (angalau kifupi) kutatusaidia nini?
Nilianza kuusikia muziki wa Gil Scott Heron nikiwa Arusha mwaka 1982. Rafiki zangu Hussein Mmasai Kikofia na Mmarekani aliyehamia Tanzania, Ikaweba Bunting, walikuwa wakisikiliza “B Movie” wimbo uliouzungumzia utawala wa  Ronald Reagan aliyekuwa Rais wa Marekani kipindi hicho. Baada ya kuhadithia namna kura ya watawala ilivyowahadaa wananchi walioendelea kuteseka Gil Scott Heron anasema:
“Haya si maisha yako; haya si maisha; hii ni sinema...”
Maudhui haya yalikuwa nguzo ya mashairi na visa alivyoandika katika albam 15 alizozitoa kati ya mwaka 1970 na 2010. Daima mtunzi huyu alitukuza ukweli na kukemea ufisadi.
Babake, Mjamaika, Gilbert Heron ni bondia na mwanasoka mahiri aliyekatiwa jina la “Mshale Mweusi” kwa ufundi wake kama mshambuliaji miaka ya 1950. Alikuwa mchezaji mweusi wa kwanza kuajiriwa na timu maarufu ya Scotland, Glasgow Celtic. Mamake alikuwa mwimbaji Mmarekani, Bobbie Scott. Baada ya Gil Scott Heron kuzaliwa mwaka 1949 waliachana akiwa na miaka miwili.  Bwa’ mdogo alilelewa na nyanyake. Akiwa bado mdogo alijifunza Piano na Gitaa. Shuleni sekondari alimstaajabisha mwalimu wake alipoandika insha nzuri; Mwalimu wake alipendekeza kwa mkuu wa idara ya lugha kuwa kijana apewe nafasi katika chuo kikuu cha Lincoln. Chuo hiki huzingatia  fasihi, Jazz na muziki. Akiwa chuoni alitoa riwaya mbili, “Vulture” na “Nigger Factory” zilizoangalia harakati za watu weusi Marekani. Mwandishi anatumia  vile vile maneno ya Kiswahili mathalan, Mjumbe. Hapo hapo chuoni alikutana na mwanamuziki Brian Jackson wakaungana na kutoa albam kadhaa. Kati ya nyimbo zilizowajenga ni “The Revolution will not be televised” (Mapinduzi hayatatangazwa), “Winter in America” (Kibaridi cha Marekani) na “Pieces of a Man”(Vipande vya Mtu). ”Pieces of a Man” inaelezea majanga ya mtu aliyedhalilishwa na maisha; akapoteza kila kitu:
“Nilimwona akivunjika vunjika;alikuwa mtu mzuri sana; alikuwa mtu shupavu sana; ndiyo, nilimwona akipasuka pasuka.”
Nyimbo zake zilivuma miaka ya Sabini na kuendeleza muziki wa watu weusi. Mtindo wake ulikuwa maendeleo ya fasihi na ushairi wa Marekani ambao leo tunauita Hip Hop au Bongo Flava kwetu.
Mtindo huu umeanzia kwa magwiji wa ushairi Langston Hughes, Amiri Baraka, Last Poets na bondia Muhammad Ali. Fani ya kusema haraka haraka imepakana na muziki pia wa James Brown aliyeanzisha mapigo ya haraka (Funk) yaliyo “pilipili” ya Hip Hop. Wanarapu vijana leo Eminem, Public Enemy na Kanye West wamekiri Gil Scott Heron aliwaathiri kimtindo na James Brown, kimuziki.
Baada ya kifo chake magazeti mengi yalimlilia hapa Uingereza. Simon Price wa Independent aliandika “hakuna mtu aliyeunganisha fani simulizi na muziki wa jazz kama Scott-Heron.”
Wamarekani weusi wamepitia machungu ya kutisha kipindi cha miaka 500. Machungu hayo ni vipigo,kunyongwa, kufungwa, kukosa elimu, kazi, ulevi na dawa za kulevya. Si ajabu licha ya mafanikio, Gil Scott- Heron alikumbwa na kinamasi cha dawa za kulevya yaani unga wa Cocaine. Katika miaka yake ya mwisho alipelekwa jela mara mbili. Alivyo mkweli alikiri hadharani ana maradhi ya UKIMWI uliotokana na tatizo hilo, lililomuua. Nilikutana na Gil Scott Heron na kumhoji mara kadhaa. Kila tulipoongea aliniasa kujifahamu, kuipenda Afrika na kutopoteza dira na malengo. Fundisho kwetu?
Wasanii, waalimu, wanafunzi, wataalamu, waandishi wa habari, wabunge, viongozi na wote wenye uwezo wa kuelemisha na kuongoza watu wanatakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu.  Na huwezi kuwa na nidhamu bila kuwa mkweli, rohoni.
Jaribu kusikiliza muziki wake mtandao wa You Tube.
Mungu aiweke roho yake pema peponi, Amina!

 http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/12928-kutoka-londonhazina-ya-mwanamuziki-gil-scott-heron

No comments:

Post a Comment