Sunday 30 October 2016

KISWAHILI KINAVYOZIDI KUPARAGANYA HERUFI “R” NA “ L”





Watanzania tuamke jamani. Tumelala.
....Kiswahili kilianzia kwetu. Nchi kumi na moja zinazungumza lugha hii iliyotuunganisha na kutuletea amani zaidi ya miaka 100!
 Nchi kumi na moja! Ongezea idhaa kadhaa za redio, TV na mitandao jamii ughaibuni inayokitukuza Kiswahili. Jazia, vyuo.
 Hapa London kiko chuo maarufu cha lugha- SOAS ( School of Oriental and African Studies- Shule ya Masomo ya Mashariki na Afrika).
Mtaa wa Russel Square, katikati ya jiji. Si vichochoroni kwa walala hoi.  Hapa Russel Square alipigwa kisu mhadhiri wa Kimarekani miezi michache iliyopita na gaidi  aliyechanganyikiwa akili.  Na 7 Julai 2005  basi lililipuliwa na magaidi wanne waliofariki kishabiki na kishabiki.
 SOAS iko Uzunguni.
Ukiingia chuoni  utashangaa namna vijana – toka mataifa mbalimbali wanavyozungumza Kiswahili,  tena kwa hamasa. Mwaka 2010 niliitwa kutumbuiza ngoma kusheherekea kuanzishwa klabu ya wazungumzaji Kiswahili, SOAS.
Mmoja alinieleza alivyoporwa na teksi ya kihuni akitalii Tanzania. Lakini hakulichukua tendo la kuibiwa na vibaka kujenga chuki kwa Watanzania. Kila mahali huwepo wazuri na wabaya alisema. ”Kila kapu huwa na matufaha yaliyooza na mazuri” – ni msemo wa Kiingereza usiopenda kuweka watu wote katika kundi moja. Wenzetu wanakipenda Kiswahili.
Siku hiyo hiyo ya  2010, alikuwepo pia mzee wetu, mtaalamu msifika wa Kiswahili, Dk Farouk Topan. Namheshimu. 
Mwandishi nikiwa na Dokta Farouk Topan, Ismailia Centre, London, 2016. Picha na Z Macha

Wakati nikisoma bado Mzumbe kilikuwa kipindi cha malumbano makali sana kati ya washairi wa vina na mizani (jadi ) na washairi wa mashairi huria (guni) yasiyofuata kanuni za urari  au mfanano huo. Profesa  Euphrase Kezilahabi (mwandishi mashuhuri wa riwaya za Kiswahili) alitoka na mkusanyiko wa mashairi guni ulioitwa Kichomi. Utangulizi wake uliandikwa na Dk. Farouk Topan. Dk Topan kaandika vitabu vingi vya taaluma ya Kiswahili na tamthiliya.
 Alifundisha muda mrefu SOAS. Kastaafu.  Bado wapo wahadhiri wengi wa Kiswahili toka Kenya na Tanzania.
 Mwezi jana nilikutana naye Dk Topan ndani ya tafrija  kusheherekea miaka 400 ya maisha ya  mwandishi nguli wa Uingereza William Shakespeare. Dk Topan alialikwa rasmi kuhutubia  jumba maalum la Waismailia hapa London. Akaelezea uhusiano wa Kiswahili na fasihi zake Shakespeare. Walijazana wengi pale hasa Wahindi waliozaliwa Afrika Mashariki. Wanakihusudu Kiswahili ingawa walihamia nje zamani.
 Dk Topan alitaja baadhi ya waandishi wetu waliotafsiri kazi zake Shakespeare kuja Kiswahili. Kama Mwalimu Nyerere aliyetafsiri Mabepari wa Venice (Merchants of Venice) na Julius Kaizari, kisa cha mfalme wa Kirumi aliyeuawa na mawaziri wake.

Mitaani je?
Mwezi jana lilikuwepo tamasha la siku kadhaa kusheherekea masuala ya watu weusi jumba maarufu  la starehe  Royal Festival Hall. Nikaajiriwa kuendesha darasa la  Kiswahili kupitia  muziki. Aliyenialika ni dada wa Ki-Eritrea anayekifagilia KIswahili. Nikatumia wimbo mashuhuri wa “Malaika” na “Sura Yako” wa Sauti Sol- wanamuziki toka Kenya. Kwanini nyimbo hizi zilitumiwa? Kwa sababu maneno yake yameandikwa mtandaoni na You Tube. Nani watunzi? Wa Kenya. Zingatia wa Kenya walivyo mstari wa mbele katika utunzi wa nyimbo za Kiswahili. Mwingine unaosifika ni Jambo Jambo (Hakuna Matata) wa bendi ya Uyoga au Mushrooms.
Mwezi huo huo wa Septemba nilialikwa kujiunga na kundi la mtandao jamii wa “WhatsUp”  - Kiswahili Club. Hawa wala si wazee walioishi Tanganyika enzi za Ukoloni na Ujamaa. La hasha.. Wengi ni vijana waliozaliwa baada ya 1980. Wanakienzi Kiswahili.  Hunitaka niwasahihishe kila wanapoandika au kuzungumza....
Mnaona?
Hii ni mifano michache tu ya jinsi lugha hii inavyozidi kusambaza matawi na mabawa duniani.
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa ulitangaza lugha kumi zinazokua kasi duniani na kudai Kiswahili ni ya saba! Nyingine ni  Kispanyola, Kichina, Kiarabu, nk.
Maana yake nini?
Mosi , biashara.
Mnaolilia ajira.
Zingatieni.
Mangapi unayoweza kuyafanya kuuza Kiswahili?
Kwanza je unakimanya vizuri ? Kama bado jifunze sarufi sawasawa. Pili, zingatia matumizi sahihi ya maneno na lahaja. Viko Viswahili vya aina saba. Fasaha, Kingwana (Cha Kongo), Kingazija, Cha ukanda wa  Ziwa Victoria (Burundi na Rwanda),  Kimvita, Kishenge (au Kiswanglish cha Kenya), na Kimrima (cha Dar es Salaam na mwambao). Je unavifahamu?
Zingatia maendeleo mengine muhimu. Wataalamu wawili wa Kiswahili, Profesa Saidi Ahmed Mohammed (mtunzi wa kitabu maarufu Asali Chungu, 1976)na Prof Mohammed A. Mohammed, walichapisha Kamusi ya Visawe,  mwaka 2002. Imechapwa tena.  Kisawe ni neno linalofanana na jingine. Kiingereza ni “Synonym.”
Kamusi ya visawe hukusaidia  unapotaka kusema neno lile lile bila kulirudia . Kwa mfano, mathalan, bimithili, tuseme, nk. Banja, pasua, vunja, bangua, nk. Ruhusa, idhini, ridhaa, itikio, kubalia, achia, nk.
Kamusi hii haikuwepo katika Kiswahili.
Kwa lugha nyingine kubwa, licha ya kamusi, ukiingia tu Google kutafuta visawe vyake utavipata.  Kiswahili hakuna.
Mbali ya Kamusi ya Visawe , kamusi mpya za TUKI za Kiingereza na Kiswahili zimetolewa upya karibuni na kurasa nyingi na maneno zaidi. Ya Kiingereza kuja Kiswahili mathalan, imeongezeka  kurasa 900 hadi 1000. Maana yake nini? Msamiati wa Kiswahili unaongezeka. Kazi nazo zazidi kuwa nzuri.
Maendeleo hayo,  yanakuja.
Kinachoharibu si wataalamu wa lugha: magwiji wanaotunga riwaya, au kufundisha vyuo na kamusi. La hasha.
 Tunaoharibu ni wanasiasa, wanahabari, waalimu mashuleni na watunzi wa nyimbo wanaoendelea kutukuza Kiswanglish na kuparaganya herufi L na R, kama rafiki yangu Masudi Pashamoto Msele.

 Tatizo hili lilikuwa dogo zamani kutokana na watu wa mikoani kutojua sawasawa lugha. Linazidi kukua. Watanzania wengi wanaoandika mitandaoni na  mablogi  hawatofautishi  “ bahili” na “bahiri”, “ mhalifu” na “mharifu”, “mpira” na “mpila.” Zamani watoto wadogo walioota mapengo ndiyo walioharibu. Siku hizi tunashindwa kupambanua. Sikiliza wimbo mpya wa Diamond -Salome. Mara ngapi karudia neno “Sarome”?
Wasikilize watangazaji wa redio FM wanavyochanganya na kuboronga nahau kwa kusema “Nyimbo  hii” badala ya “wimbo huu”- au “nyimbo hizi”-wanashindwa kutaksirisha  wingi wa neno “wimbo” kuwa “nyimbo.”
Toba!
Sasa  ikiwa wanahabari, wasanii, wanasiasa na waalimu mashuleni tunawafundisha watoto kusema “Luninga” kinyume cha “Runinga,” nani ataokoa jahazi la  kesho? Nani atasahihisha wanaokua na kuiga kusema “Sarome” kwa kuwa mtu maarufu kaimba vile?  Je wahusika tunasoma na kujifunza Kiswahili sawasawa? Au tunajimamasa na kubabaisha tu ?

-ilichapishwa sehemu mbili Mwananchi Jumapili  23 na 30 Oktoba 2016





No comments:

Post a Comment