Monday, 19 December 2011

INAHITAJIKA TENA KAMPENI YA “MTU NI AFYA” KUHIMIZA VYOO VISAFI AFRIKA

Kuna mambo ambayo kila jamii duniani huyahisi muhimu kuliko mengine. Kwa Mzungu akipita akaona mbwa yuko radhi achutame kumpapasa na kumpa  maneno mema. Kwetu kusalimiana wanadamu muhimu kuliko hidaya kwa wanyama.

Basi la "Baharia" mjini Moshi. Picha na F Macha

Ndiyo fikra inayonizonga nikiwa safarini Arusha kwenda Dar es Salaam. Mabasi yetu Bongo ni ramani nzuri ya kuujua utamaduni na jiografia ya miaka 50 baada ya Uhuru toka kwa Mwingereza. Ukiwa visiwani utasikia Taarabu na Kaswida; hapa Arusha hadi Moshi dereva katuwekea muziki wa Injili. Kama ile Kaswida inayoghani swalaa mbalimbali za Adhana (alfajiri) ya majogoo na Isha (mwisho jioni); nazisikia sifa kwa Yesu Kristo zikiliiza kwa jazba.
<--more--!>
Hiyo ndiyo hulka inayojionyesha miaka hii  50 ya Uhuru; Wabongo tunazidi kuzisabilia nafsi zetu katika fasihi ama za kidini (kwa uwazi kama humu ndani ya basi) au kisiri siri kupitia waganga na wanga wa kila aina wanaotutoza maelfu ya pesa. Kwa kuwa maisha yanazidi kuwa ya shida; imani katika uchawi na dini zinarefuka kama miwa na mahindi yaliyoshtadi nyika, nyanda, michanga na pepo Tanzania bara na Visiwani.
“Mungu Asifiwe! Mungu atubariki! Shetani hafiki humu...”

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete akishuhudia maiti za watoto waliofariki katika ajali ya boti Nungwi, Septemba mwaka huu.

Tunaimbiwa huku basi likifukuta mbuga; tushavuka Moshi, halafu Same na Hedaru; tunaipita sasa milima ya Upare; punde katani zinaanza kujipanga. Kila baada ya mida mabango mbalimbali yanawaasa madereva: AJALI BARABARANI ZINAEPUKIKA. TAFADHALI CHUKUA TAHADHARI. Si kwamba serikali haifanyi bidii kukinga ajali hizi; kinachokosekana ni vitendo. USIENDESHE GARI UKIWA UMELEWA. USIENDESHE GARI UKIONGEA KATIKA SIMU...
 Mbali na maonyo kwa madereva ; abiria nao wameshauriwa wachangie; wasisubiri tu CCM. Ndani ya basi pia mna matangazo yanayowataka abiria wawashtaki madereva wakorofi: TOA TAARIFA KIKOSI CHA USALAMA. PIGA SIMU NA. 0732-98723 /062-887722...na kadhalika wa kadhalika.
Tunapokaribia Mombo huyooo askari garini; kimya kimya.
Kuingia askari huyu ndani ya basi kumetuletea ahueni ya mkono wa serikali unaojaribu kuzitomasa nyoyo zetu zinazodunda. Ila je kwanini ajali zazidi kuongezeka? Juzi tu mwisho wa Oktoba  basi la Deluxe, Arusha kwenda Dodoma, liliua watu 20, pale Misugusugu, Pwani. Watu ishirini, NI WENGI. Mwezi Machi, wasanii 13 wa “Five Stars Modern Taarab” walipoteza roho Mbeya kuja Dar es Salaam.
“Vifo vya wasanii hao vimeacha pengo kubwa katika tasnia ya muziki nchini,” aliandika Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni na Michezo.
Barabara zetu ni uwanja wa mapambano kati ya Bajaji, magari madogo, Jipu , malori, mabasi na Boda Boda...Picha na F Macha

Kitwakimu ajali zilizotokea (na zinazoendelea kutokea) zimesababishwa na uzembe na ubazazi wa madereva ambao bado hawaadhibiwi. Chukua ajali ya lori iliyoua vijana wa chuo cha Kiislamu cha Samsili Maarifa mwaka juzi mjini Tanga. Ilielezwa kwamba dereva aliyesababisha vifo vya wanafunzi 18 na majeruhi 50  “alikuwa akishangiliwa”  alipokimbiza  lori hilo aina ya Fuso lililojaza watoto zaidi ya 100; akashindwa kupinda, akabingirika mara mbili. Baada tu ya kizaazaa, mshashi akatoroka. Maswali ya kujiuliza ni kwanini madereva siku zote hunusurika? Na je, wakishakamatwa na viganja vya sheria je, huadhibiwa ipasavyo ili kuwatisha wenzao? Linganisha haya na kisa cha dereva mjini Dorset, Uingereza aliyefukuzwa kazi wiki hii baada ya abiria kumpiga picha simu ya mkononi (ona taswira chini) akicheza Chemsha Bongo ya Kijapani (“Sudoku”) huku anaendesha basi la vijana wa shule.

Sheria na adhabu zilizowekwa na serikali Uzunguni zinaogopewa na kufuatwa kutokana na hatua kali kama hizo.
Zaidi ya miaka 50 iliyopita mwanamuziki Fundi Konde wa Kenya aliimba “ajali haikingiki.” Sikubaliani na gwiji huyo wa sanaa.
Ndiyo maana nyimbo za kidini ndani ya mabasi zimegeuka  viyoyozi vinavyojaribu kututuliza abiria tukielekea mikondo miwili; kufa safarini au kufika salama. Tunapoipita milima ya Usambara inakumbusha jinsi mazingira ya Tanzania yalivyo mazuri; namna nchi yetu tajiri, kimaumbile. Mungu yuko nasi kijiografia. Na Mungu katufikisha Korogwe salama.
Tumeshuka sasa. Vyoo vimejazana. Kwetu wanaume si tatizo maana hujisaidia tumesimama hata kama mbele yako yamejazana mainzi yanayong’onga na kugombana na vinyesi na mazingira yanayonuka. Kwa wanawake si madogo. Shurti wakae au kukuchumaa; isitoshe vyoo vyetu mara nyingi havina pa kunawa. Kila mmoja atatoka vile vile akaongoza kula hotelini.
Wakati nikila pembe ya basi namwona dada mmoja, niliyekaa naye ndani.
“Vipi hali?” Namuuliza nikidhani labda kapoteza mkoba wake wa pesa. Kafutua mdomo.
“Ah vile vyoo vyetu wala havisemeki.”
“Sasa utafanyaje?”
“Ah nimejitahidi tu hivyo hivyo.”
HIVYO HIVYO, ndiyo maneno yaliyozoeleka kwetu Bongo. Na  si tu Bongo; Afrika nzima. Na hata ukija Ughaibuni mara nyingi klabu au sehemu tulizo Wamatumbi hazina vyoo vinavyoridhisha kwa usafi. Hili ni tatizo ambalo kila mtu analifahamu. Nakumbuka nikitoka Dodoma kuja Arusha tulikuwa mji mmoja mdogo na vyoo vilikuwa vimeharibika. Kila mtu alikuwa akikimbilia porini. Kwa wanaume si tatizo; ila kwa wanawake, je? Bibi mmoja akasononeka:
“Walikuwepo vijana wamesimama simama  wamejicha jificha wakitunguchulia. Mtu wala hujisikii kujisaidia.”
“Sasa mnafanyaje?”
“Inabidi ujizuie tu hivyo hivyo.”
HIVYO HIVYO. Je wakiwa hedhini?
Swali  gumu; akina mama wenyewe ndiyo tu wanalifahamu. Wanawake ni watu wenye mambo mengi:  kupika, kufua, kujifungua, kulea watoto; ila ukiangalia huduma za vyoo vya umma, vyoo vya kadamnasi, mahotelini na barabarani, havithamini au kuzingatia ridhaa na matakwa yao na yetu sote.
 Miaka ya Sabini serikali ya Mwalimu Nyerere ilipitisha sera ya “Mtu ni Afya” kujaribu kuhimiza si tu usafi wa mwili bali mazingira na vyoo. Uzuri wa sera hiyo ulikuwa si tu kujenga mwamko wa lishe bali kuhimiza, siha na  usafi. Baadaye hata neno “siha” ambalo maana yake ni afya likafahamika kutokana na mkate mnono wa boflo ulioanza kuuzwa. Ingekuwa jambo muafaka kuifufua tena sera hiyo ; vyoo vyetu havifai kabisa.
Nilikuwa nikijadiliana suala hili na sahiba yangu mzawa wa Ivory Coast. Akasema utamkuta Mwafrika kasoma, ana wadhifa mkubwa, gari safi, jumba la roshani na marmar; lakini ingia choo nyumbani kwake. Utakoma.
Mama wa Kizungu akisafisha choo.

“Labda,” akasema dada huyu anayetoka kijiji kimoja na mchezaji mpira maarufu Didier Drogba, “Bado hatujazoea desturi za Kizungu za vyoo ndani ya nyumba. Tumekuwa na utamaduni huu muda mfupi sana. Bado sisi watu wa kujisaidia vichakani.”
Ingawa tulicheka; nilihisi najicheka mwenyewe; nikijitonesha kidonda sugu tulicho nacho Afrika.

Ilitoka Mwananchi- Jumapili  4 Desemba, 2011.
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/18087-kutoka-londonkampeni-ya-mtu-ni-afya-ifanyike-upya-afrika

No comments:

Post a Comment