Sunday, 14 May 2017

KILIO CHA WATOTO KARATU : TUENDELEE KUHUZUNIKA HADI LINI?


Ingawa muda umepita  tulioko Ughaibuni  tunawapa pole waliofiwa Karatu. Tumeangalia picha zilizosambazwa kwa uchungu, maastajabu na majonzi. Kama mzazi picha moja iliniuma sana. Watoto wa Lucky Vincent wamesimama  wakijitayarisha kuondoka safari yao ya mwisho.  Wamevalia mavazi ya shule: furaha ya mtoto. Masomo, maisha, matumaini. 
Ila picha inayostahili  kujadiliwa zaidi ni ya wanaume kadhaa wakikwea basi , wakijaribu kunyofoa maiti zilizojibana bana.  Hapa ndipo kilipo kilinge na janga letu Waafrika leo.
Inapotokea ajali kama hii watu wa kwanza kufika na kufanya kazi ya kuratibu, kuokoa  majeruhi  au maiti huwa askari, waokoa ajali na vyombo vingine vya huduma. Kawaida zingekuwa helikopta zikipita, juu, zikifanya doria. Maana penye ajali pia hufanywa mengi. Kupima sababu za ajali. Kuhakikisha mali za maiti na majeruhi salama, nk.  Lakini bara Afrika likifikwa na ajali utawaona wananchi wa kawaida wakifanya kazi za wahudumu kwa mikono mitupu. Ushahidi wa janga hauwekwi. Rasilmali zetu dhaifu.
Kuna jamaa nilikuwa nazungumza naye, mzawa wa Trinidad.  Alipoona picha akamaka kwa hasira:
 “ Karne zilizopita tumeona Warumi wakitawala, kisha Waingereza , Wamarekani , na hatimaye itakuwa Waafrika. Lakini kipindi hicho mali zetu zote zitakuwa zimeporwa...bara halitakuwa tena na madini wala mimea. Tutakuwa juu lakini maskini kirasilmali.”
Akiwa na maana gani?
Utajiri wetu hausemeki.  Ila bado maskini. Tunaibiwa neema zetu, ama kwa kuuza bei nafuu au kwa wageni  kuzipora kwa mwendo mkali. Na hizi safari za mabasi ya umma zinazidi kuwa za utata na huzuni. Si kwamba Wazungu au wenzetu wengine hawapatwi ajali. Wanapata, tena sana. Ila hujifunza.

 Hapa Uingereza mathalani miaka 40 iliyopita ajali za mabasi zilizidi. Baada ya uchunguzi na utafiiti ikapitishwa sera kuwa mabasi hayaruhusiwi kukimbia zaidi ya kilometa 30 kwa saa. Mabasi ya shule , vyuo na wagonjwa hayakubaliwi mwendo wa zaidi ya kilometa 20. Unapopanda basi la kadamnasi hutegemei dereva kukimbia. Mabasi yana mikanda na hiyo ndiyo huzuia wasafiri kubingirika na kupasuka vichwa yanapobwagika.
Au tudadavue ndege ya Lufthansa iliyoanguka milimani Alps, Ufaransa,  Machi 2015. Abiria 144 wengi wao wanafunzi wa shule walifariki. Ndege za Lufthansa huwa hazidondoki ovyo. Baada ya uchunguzi kufanywa iligundika kuwa rubani wake, Andrea Lubitz, alipindua ndege makusudi, ili kujiua mwenyewe shauri alikuwa na matatizo yake. Bw Lubitz alivizia rubani mwenzake alipokwenda msalani akafunga mlango kwa kitasa.
Baada ya angamio uchunguzi mkali ulifanywa na sasa imepitishwa sheria kuwa marubani hawaruhusiwi kukaa peke yao chumba cha kuendesha. Juu ya hapo vipimo kamili vya kiafya vinatakiwa kufanywa kwa marubani kabla ya kuendesha ndege.
Jingine lililowatokea wafiwa ni malipo ya fidia ya Euro 50,000 kwa kila familia. Baada ya majadiliano fedha ziliongezwa. Ingawa fedha hazirudishi marehemu hii inaonesha thamani ya makampuni haya makubwa kwa wasafiri wake.
Mbali na masaibu,  mafunzo yamepatikana na sheria (na utaratibu) rasmi kupitishwa.
Je sisi tutafanyaje kuzuia majonzi kama ya Karatu hayatufiki tena?

Ilichapwa Mwananchi Jumapili  14 Mei 2017


No comments:

Post a Comment