Monday 17 June 2013

KIFO CHA ALBERT MWANGEA -KINATUULIZA MASWALI GANI?- Sehemu 1



Babu wa fasihi ya Kiswahili, Shaaban Robert alifariki mwezi huu  mwaka 1962. Ingetakiwa sikukuu ya kifo  chake yaani Juni 20  ifanyiwe maadhimisho kila mwaka. Sisi na wenzangu wa bendi ya Sayari tuliwahi kusheherekea kwa maonyesho ya 1983. Hazina hii tukufu ya taifa inatakiwa zaidi ya hilo.
  Moja ya vitabu vyake babu ni  “Kielezo cha Fasili” (kilitolewa upya na mwongozi wa wachapishaji Tanzania; “Mkuki na Nyota” ,2004) kinafafanua mashairi yake kwa wasomaji mintaarafu  ya kujenga mapafu kilugha.
Ananyambua  Shairi la “Jina”: “Mwanadamu mwenye fikra njema huacha fahari au sifa kwa watu ambayo vizazi vyake vya nyuma yake hupenda kuiona, na ambayo itakuwa kama hazina kwa watu wote katika dunia.”
Albert Mangwea hakua Shaaban Robert;  kafa akiwa na miaka 31 tu. Lakini  Mangwea au Mangair alitumia fani ya ushairi kuchangia kuiendeleza fasihi ya Kiswahili  na kipaji chake alichomegewa na Muumba.
Kifo  hiki kilichokua Usauzi (Afrika Kusini) kimeongelewa na kinaendelea kuongelewa. Mwaka jana wakati huu Tanzania ilimpoteza Steve Kanumba. Vifo vya chipukizi hawa vimeacha utata na mijadala marefu.
 Mangwea alifia ughaibuni.  Maisha ugenini ni magumu maana habari huwa hazitangazwi sana. Mbali na taratibu za kisheria na itikeli, kinachongojewa kutufariji huwa viongozi wa dini na serikali.


Vipo vifo vya aina nyingi. Ila  vifo vinapokua na utata husubiri mkono wa sheria utubembeleze. Kanumba alifuatiliwa na mashtaka ya bibi aliyekua naye; Mangwea, hatuyajui  bado kiuhakika...
 Miaka iliyopita habari za vifo vya Waafrika hasa zile zilizohusiana na UKIMWI au dawa za kulevya hazikuwekwa wazi, shauri ya aibu, miiko na staha. Nakumbuka wanamuziki wawili maarufu Hukwe Zawose na mpwake, Charles Zawose walipofariki, wanahabari hatukueleza chanzo ili kuheshimu hisia za familia zao.
 Magazeti ya ughaibuni , walakin, hayakupepesa.
 Mwanamuziki Charles Zawose alifariki ghafla akijitayarisha kupanda ndege Sweden alikokua akifanya maonesho ya muziki wa kijadi, 2004. Kwa kuwa Charles na babake mkubwa walishajenga sana majina ugenini habari  zilichambuliwa katika magazeti viongozi. Mwandishi John Lusk wa “Independent” ( linaloheshimika sana Uingereza) :
 “Kifo kimenyamazisha moja ya himaya kubwa sana ya familia ya wanamuziki wa Tanzania... Walikuwa mabalozi viongozi wa muziki wa Kigogo.” Akaongeza kuwa Zawose  kafariki kutokana na “maradhi yaliyosababishwa na UKIMWI.”
 Nyumbani, lakini, ugonjwa haukutajwa.
Inasemekana Mangwea alikua mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya. Majadiliano yaliyoendelea juma lililopita ni iwapo aliwekewa sumu, dawa feki zilizokwisha muda wake, nk. Baya lolote lililofuatia matumizi hayo basi haliwezi kuacha kuleta utata na hatimaye malumbano mazito. Muhimu sana ni mafunzo tunayobakiwa nayo.
 Si ajabu kwa wasanii kufariki kutokana na dawa hizi. Huku ughaibuni ni mkasa uliozoeleka tangu zamani. Miaka miwili iliyopita mwimbaji Amy Winehouse alinyauka –akiwa na umri mdogo wa miaka 27-baada ya muda mrefu kujiharibu na ulevi huu wa Kishetani na Kiza.  Alikutwa peke yake nyumbani ameshakauka kutokana na pombe nyingi kuzidi; lakini ni karibuni tu ndipo maelezo rasmi ya sababu za kifo, yametolewa rasmi.
 Mpiga gitaa stadi kuzidi wote katika historia,  Mmarekani mweusi, Jimi Hendrix vile vile, aliaga dunia jijini London akiwa na miaka 27 mwaka 1970. Hendrix alitumia sana dawa hizi za ki-fisi, hususan unga wa “cocaine “ na vidonge vya kusisimsha. Usiku wa kuamkia asubuhi aliyofariki alikunywa vidonge  tisa vya Vesperax- badala ya kimoja (ilivyotakiwa ) kusudi eti apate usingizi.  Tisa!
Bibi wa Kijerumani aliyekuwa naye, Monica Dannemann( aliyekuja akuandika kitabu kuhusu maisha yake na Hendrix) alijiua 1996 akiwa na miaka 50. Moja ya sababu za kujiua ni wanahabari na wanawake wengine kumghasi muda mrefu kwa kutoamini maneno aliyosema. Monika (kama dada aliyekutwa na marehem Kanumba) ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na kamanda huyu wa magitaa.  
Vifo hivi viwili vi mfano wa namna wasanii wanaotumia vilevi kuzidi- hata nchi zilizoendelea  -wanavyosababisha utata wakishafariki.
Somo kwetu nini?
Kutangaza habari za vifo kama hivi ni fundisho kwa  jamii nzima. Fikra iliyoenea kwamba msanii lazima ule dawa, bangi  au pombe sana ndiyo utunge ni potofu, maana kuna wasanii kibao (tena wakali) wanaotunga bila “madude” hayo- na wangali hai.
Jambo la pili ni kujua unapokwenda na unachokifanya.
Kama kweli marehemu Ngwea alipewa dawa “feki”  au zenye sumu je alichanganyikana na watu gani?
Ughaibuni ni msitu wenye miiba na chemchemi  safi pamoja. Vijana wengi wanapokuja huku, huwa hawajafanya utafiti  tosha, na hata wakiufanya huwa  wa juu juu. Leo makampuni yanatakiwa na serikali mbalimbali kueleza wazi wazi bidhaa zimetengenezwa lini na wakati wake utaisha lini. Niliwahi kuwa na wageni wenzangu wa Kibongo na nilipowakatia mkate nikagundua tarehe yake ilishapita kwa siku tatu. Ingawa ule mkate haukua na dosari ukiutazama,  nilikua tayari kuutupa jaani.
“Hapana hapana ; tutaula tu” wakasema.
Nikasisitiza usiliwe.
“Ah wacha tu tutakula. Kutupa chakula vibaya.”
Kweli, kutupa chakula si vizuri. Lakini desturi za nchi zilizoendelea ni kutokula vyakula vilivyopita wakati. Hii ni sababu bidhaa huwekewa dawa zinazozifanya zisioze; hivyo ukizila zaweza kukudhuru. Kwa Kiingereza neno linalotumika ni “preservatives.” Preservatives hutumikwa katika vyakula ( au vinywaji)  ndani ya mikebe, vyupa , plastiki, nk.  Kutokana na Waafrika wengi kutoelewa hilo, wafanyabiashara mafisadi wa nchi tajiri (leo) wana tabia ya kutuma bidhaa hizi kwetu maana wanafahamu hatujali au hatujui. Tunapodhurika au kufa tunasema Ah kazi ya Mungu.
Kazi ya Mungu haiendi hivyo.
Na serikali zetu, je?
Mwaka 1994 kijana wa Kitanzania  aliuawa Italia. Huyu kaka alijihusisha na biashara ya dawa za ki-Ibilis.  Mambo yalikaa kimya kimya, hadi leo habari zake hazisemwi. Uongo hapana; makosa yalikua yake. Utamaduni wa biashara hii ni kwamba mkiudhiana, usipolipa au ukiwasaliti wale unaojihusha nao – ambao huwa majambazi katili- wanakutosa.
Lakini la ajabu serikali zetu ughaibuni huchelea kujihusisha na watu hawa. Ndugu za mhusika hupewa mwili, mambo (kimya kimya) yakaishia chini ya mkeka. Wenzetu waliondelea hutuma maofisa serikali na  kutangaza habari runingani kusudi liwe funzo kwa jamii na taifa.
Tumalizie mada hii muhimu juma lijalo.






No comments:

Post a Comment