Monday, 17 June 2013

KIFO CHA ALBERT MANGWEA – KINATUULIZA MASWALI GANI- Sehemu ya PiliKwanza kabla ya kuendelea na (kumalizia) mada tuliyoianza wiki jana,  tuwape pole ndugu wa familia yake Albert Mangwea. Tuwape pia pole marafiki zake na wote waliomjua kwa karibu. Tuwaombe radhi kwa kuendelea kuzungumzia jambo ambalo linawakumbusha uchungu wa mtu aliyekwisha zikwa.
Pamoja na hayo tujikumbushe madhumuni ya kuandika na kuzungumzia suala hili.
Kwanza kabisa kupoteza vijana wanaoanza maisha katika hali hizi mbaya si jambo zuri. Wapo wengi wanaondelea kuzungumzia kwamba ni Mungu kaamua na kwamba kifo ni asili maisha. Hatukatai hilo. Ila kwetu Tanzania imekua sasa desturi kukubali vifo na utamaduni wa kufa mapema.  Wanapoendelea kufariki vijana tunakubali ni maajaliwa. Zikitokea ajali za magari (zinazouzilika) zilizotokana na uzembe  wa madereva pia tunalitaja jina la Mungu. Mungu amekuwa sasa ndiye  mwamba wa kila baya. Kageuka kisingizio. Kwanini sisi tu ndiyo kitakwimu tuna vifo vingi zaidi tena vya watu wenye umri mdogo?
Lakini kabla ya kuendelea zaidi, tukubaliane ...


Kitakwimu duniani, kila dakika hufa watu mia moja. Ina maana baada ya wewe msomaji kumaliza kusoma makala hii(ikiwa utachukua dakika kumi kufikia mwisho) wanadamu 1,000 watakua wamemaliza maisha yao. Takwimu za sensa duniani zinatujuza vile vile, kila mwaka tunapoteza watu 56 milioni. Hii ni takribani idadi ya Watanzania wote. Kila mwaka! Hapo hapo ni vyema kujikumbusha kila sekunde huzaliwa watoto saba duniani. Kila sekunde dunia inatema na kumeza. Siri ya maisha ni mzunguko mzima wa sayari na muda.
Wanadamu lakini tuna wajibu na majukumu. Ulimwengu tuliokuta  umetengenezwa na kuchangiwa na kila aliyepita , aliyekuwepo na atakayekuja. Ndiyo maana unapoanza kuwa mtu mzima  shurti ujue la kufanya kuchangia. Siri yake ni nidhamu na kujituma.
Lawama tunazozitupa kwa Mwenyezi Mungu kila siku zinachangia  kujidunisha. Miaka mia moja iliyopita, magari, simu na tarakilishi (au kompyuta) vilikua ndoto za Abunawasi.
Nakumbuka mwaka 1990 nilisoma gazeti la Kimarekani (Newsweek) likasema baada ya miaka ishirini itakua kawaida kwa watu kutembea na simu mkononi. Sikuweza kubashiri. Leo simu za mkononi ni jambo la kawaida kama yalivyo magari na runinga.  Miaka mia moja ijayo vitakuwepo vitu vipya zaidi.Yote yamefanywa na wanadamu wenye mikono miwili na miguu miwili kama wewe na mimi. Swali.
Je, mchango wako utakua nini? 
Vijana wanaofariki mapema baada ya kuonja maisha mazuri ya kazi waliyoipigania wanajisahau.
 Unapopambana na maisha magumu (katika fani yeyote) kisha ukafanikiwa, lazima ujikumbushe unakotoka. Sisi Waafrika tuna mengi ya kujenga.
Mwaka 1965 mwimbaji Salum Abdallah aliyekuwa mfanya biashara wa kujitegema alifariki kabla hajavuna matunda ya kazi zake. Salum Abdallah kama alivyokuja kuwa mwanamuziki mwenzake Mbarakah Mwinshehe walitafuta studio za kurekodi nyimbo zao Kenya. Kifo cha Mwinshehe kilikua kibaya zaidi shauri baada ya ajali ya gari (mwaka 1978) alikosa damu shauri damu huuzwa Kenya, na hakua na fedha. Alikua Kenya akitafuta pia studio.
Wengine walioishia ughaibuni bila mafanikio ni Patrick Balisidja na Kassim Magati (aliyefariki Botswana 1994). Hii ni mifano michache ya wanamuziki waliohangaika maisha yao yote bila kheri. Leo vijana wengi wa Bongo Flava wana maisha mazuri kuliko wajomba na babu zao hao waliopita. Baadhi ni milionea, wapo waliojenga hoteli. Maisha haya “mazuri” kiwastani ni kipimo kizuri cha maendeleo ya msanii na mfanyakazi wa sanaa za maonyesho Tanzania. Lakini mwisho wake uweje? Msanii na mfanyakazi yeyote aliyefanikiwa anatakiwa asisahau alikotoka na ajikumbushe wajibu kwake na jamii yake.
Wajibu kwa jamii maana yako ni  nini?
Zamani enzi za TANU tuliambiwa maadui makubwa ni ujinga, umaskini na maradhi. Ukiwa maskini elimu inaweza kukukomboa. Ndiyo maana wazazi wengi huwakazania watoto wasome.
Zaidi  ya asilimia 80 ya Watanzania hawajasoma zaidi ya shule ya msingi. Kwa Mwafrika leo elimu ni chombo cha ukombozi. Mtu unapofaulu kupitia njia nyingine zisizo za elimu (mathalan usanii au biashara) unaweza kutumia ahueni hiyo kuwasaidia wenzako. Ndiyo maana nidhamu na kuitambua faida ya mafanikio yako ni jambo muafaka. Utumiaji wa dawa za kulevya, pombe nk kwa wingi ni moja ya mifano michache ya ukosefu wa nidhamu. Ndiyo dawa hizi ni sehemu za maisha ya wasanii hasa wanamuziki. Lakini hatima yake ni nini?
Je, kwanini sasa hivi pameanza kuenea tabia, utamaduni na desturi ya kutojituma na ubinafsi wa kifuska kuzidi ?
Je tabia hizi zinatokea wapi?
Mbali na kujituma, je asasi za serikali zetu hufanya nini yanapotokea mauaji ya wananchi?
Wiki iliyopita tulitazama kidogo mauaji ya kijana aliyeuawa nchini Italia kutokana na biashara Ibilis ya uuzaji wa dawa zakulevya. Mfano huu unaweza kuwekwa kando kwa vile kijana huyo alijihusisha na biashara mbovu na haram. Tunaweza kusema mwanadamu huvuna ulichopanda. Mungu amrehemu.
Lakini je, mwanamke aliyefanya kazi ya kuuza mwili wake (ukahaba) akapigwa hadi alipofariki?
Mwaka 2004  askari wawili wa Kiingereza  waliokua matembezini Tanzania baada ya kuwa vitani Iraki, Nigel David (miaka 23) na Brett Richard (20) walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka na kumuua mwanamke wa Kitanzania , Conjesta Ulikaye Novemba 2004. Kufuatana na habari za magazeti mauaji yalitokea hoteli  ya Silver Sands, Dar es Salaam na kesi ikashughulikiwa kwa siku 36 tu baadaye askari wakaachiliwa huru “kutokana na kukosa  ushahidi.”
Linganisha kesi na habari zinazotokea kuhusu wahalifu wa Kitanzania. Ingekuwa Mtanzania asingenyongwa? Au linganisha kesi kama hii ughaibuni. Ukiua Uarabuni au nchi nyingine za Mashariki za Mbali, huwezi kuachiwa tu hivi hivi. Linganisha na kesi zinazohusu Wazungu. Mara nyingi sana wenzetu wanaposhtakiwa kwa makosa mbalimbali serikali zao hazikai kimya. Miezi miwili iliyopita mama  wa Kizungu (miaka 56) alishikwa na dawa za kulevya (thamani yake Dola milioni 2.4), Indonesia. Alipohukumiwa kunyongwa, serikali ya Uingereza ilipiga sana kelele. Hadi sasa hajanyongwa. Serikali za wenzetu hujaribu hutetea wananchi wao. Lakini familia ya marehemu  Conjesta Ulikaye ina zuri gani la kusema kuhusu binti yao aliyeuawa kinyama vile na waliomtosa kuachiwa? Je, tunawatendea haki wananchi wetu kweli?
Ikiwa wananchi wanahisi hawatendewi haki je,  wataiga wapi nidhamu?
       
 Ilichapwa pia Mwananchi Jumapili

1 comment:

  1. unajua Freddy,Roma haikujengwa kwa siku moja. Mafanikio hayaji kwa "over night". Watanzania hatujui hili na itatusa sana

    ReplyDelete