Thursday 13 December 2012

NINI MIZIZI YA TATIZO LA WAISLAMU KUCHOMA MAKANISA NA AMANI AFRIKA?-Sehemu ya 2


 Jumapili iliyopita tuliona namna mwanamuziki Fela Kuti  alivyoonya kuhusu imani za kigeni zilivyochangia kupotosha utamaduni wa Mwafrika.
Akasisitiza : “Ukristo na Uislamu si dini zetu...Wakristo wana fikra na tabia  za Waingereza na Wamarekani, ilhali Waislamu wana tabia za Waarabu.” 
 Msikilize mwenyewe akijieleza kinaga naga
Jadi mbalimbali duniani  zilijengwa kufuatana na mazingira na hali ya hewa. Dini zilitumia mvua, jua, radi, miti, wanyama nk,  kuabudu na kutambika.  Dini mbili kuu za Waafrika leo zimetokana na utamaduni wa Mashariki ya Kati na Wazungu.


<--more--!>
Ona mathalan sikukuu muhimu ya Krismasi inayotueleza kuwa Bwana Yesu Kristo alizaliwa Desemba. Mnajimu na mwanasayansi, Mchungaji Don Jacobs anasema katika kitabu chake “Astrology’s Pew in Church” alichoandika baada ya utafiti wa muda mrefu kwamba Bwana Yesu alizaliwa Machi mosi.
Hoja hii imekubalika (Uzunguni) miaka mingi kwamba Bwana Yesu hakuzaliwa Desemba. Sababu ya kuigeuza tarehe ya kuzaliwa kwake inatokana na dini ya Wazungu iliyoitwa Pagan (sisi huita Upagani kutokuwa na dini lakini Mapagani waliabudu  maumbile kufuatana na hali ya hewa) ambapo matambiko muhimu ya kula na sherehe hufanywa tarehe 21  Desemba  wakati jua linapokua kaskazi ya Ikweta  msimu wa baridi (“Winter Solstice”). Kinachosemwa na Wazungu  ni kwamba lengo la kuiweka Krismasi tarehe hizi  ilifuatana na shangwe za sherehe hii. Huu ni mfano wa namna dini inavyofuata desturi za jamii. Na ndiyo sababu Mnigeria, Fela Kuti akauliza je pana uhusiano gani  kitamaduni baina ya dini hizi na  sisi Waafrika?

Misingi ya Uislamu ni huko huko Mashariki ya kati. Majina ya manabii wake ni yale yale ya Wakristo, sema kutokana na tofauti kati ya Waarabu na binam zao Wayahudi wakakinzana. Rejea :  Issa kwa Waislamu ni Yesu kwa Wakristo, Yusufu ni Joseph, Ibrahim ni Abraham, Mariam ni Miriam, Hawa ni Eve au Eva, Musa ni Moses, nk.
Mwaka 2005 mkutano mkubwa ulifanywa Mashariki ya kati kutathmini mustakabal wa Waislamu. Ulihudhuriwa na wataalamu 200 wa Kiislamu toka nchi 50 ukasimamiwa na Sheikh Iz Al Din Al Tamimi na mfalme Abdullah wa Jordan.
Washiriki  walihimiza misingi ya Uislamu yaani “huruma, heshima, uvumilivu, kusujudu na uhuru wa kidini.” 
Walikumbusha nguzo kuu tatu  zenye “madhahab” (madhehebu) manane : Hanafi, Maliki, Shafii, Hanbali, Jafari, Zaidi, Ibadi na Zahiri;  zinazowakataza Waislamu kuwasuta wasiofuata dini hii kwa kutamka Takfir. Neno “takfir” lililotokana na  “kafir”  (kufuru au kutokuwa na heshima) huwasema wakosaji. Ila Uislamu unasema wanaoruhusiwa kugombesha ni “walema au walama” tunaowaita maalim na mufti (au waalimu) kwa Kiswahili. Hawa waliruhusiwa katika sheria ya Kiislamu kuwataja au kuwashtaki makafir. Tatu, mkutano ulishutumu vurugu na mauaji yanayotumika kwa jina la dini hiyo. Hivyo basi ikiwa misingi ya dini inatokana  na amani, je adui nani hasa?
Tukichunguza jamii zinazovurugwa na magaidi sasa hivi Afrika  tunaona mizizi iko katika uchumi na siasa. Kufuatana na habari zilizotolewa na shirika la kuondoa Umaskini duniani, kati ya 1975 hadi 2000, Afrika ni bara pekee lililozama (katika njaa, umaskini na ukosefu wa elimu) licha ya Uhuru wa nusu karne.
 Tuanze na Somalia, yenye Al Shabaab. Karibuni bei ya vitu imepanda kwa asilimia 300. Toka mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa Rais Siad Barre mwaka 1991 utawala ni wa vikundi vichache vya makabila na familia zenye mabavu. Kijiografia, Somalia si nchi yenye rutuba; riziki hutegemea ufugaji. Barabara na usafiri  ni dhaifu na kufuatana na ripoti iliyotolewa karibuni na wataalamu mbalimbali wa kimataifa, Somalia inahitaji miaka 20 kujijenga sawasawa. Hilo haliwezekani  bila amani.   
Boko Haram (“ elimu ya Kizungu ni dhambi”) ilianzishwa mwaka 2001 na Mohammed Yusuf kupinga sayansi na sheria zilizopo Nigeria.
Karibuni Nigeria imeorodheshwa kuwa nchi ya saba duniani yenye mkusanyiko mikubwa ya makabila, dini na utajiri wa mafuta. Ila utajiri huu unawanufaisha wachache, waasi wanaamka wakitumia dini kama ngao na sababu.
Hali hii imestawi haraka mwaka huu Mali.
Magaidi wa Mali, yaani Ansar Dine (Dine inatokana na “dini” kwa  Kiarabu) wanajitengenezea fedha kwa kuwakamata wageni au  matajiri kununua silaha. Lengo la Ansar Dine si tu kujenga Sharia, bali kutawala jamii.
Iyad Ag Ghaly ( mpinzani wa serikali miaka 30 sasa )anayeongoza “Ansar Dine” anadai amechukua theluthi mbili ya nchi baada ya mapinduzi dhidi ya serikali iliyoshinda uchaguzi kihalali. Sharia, itikeli na tabia zinazofanana na zile za  Mataliban wa Afghanistan zimepiga marufuku TV,  mpira, pombe,  kuvuta sigara; na huwakata mikono au kuwapiga mawe wahalifu.  Njaa, ukosefu wa umeme na mafuta vimesababisha wakimbizi laki mbili.
Karibuni “Ansar Dine” imevuruga sehemu za tambiko za kijadi zinazoheshimiwa na wananchi wa Mali kwa karne nyingi. Waislamu wengi hawataki kuunga mkono Ansar Dine; ila vijana  wasiokuwa na elimu au kazi  ndiyo wanachama.
 Kisa? Kama huna mustakabal au matumaini katika maisha utafanya nini? Ansar Dine ina “wapiganaji” toka nchi za kigeni (mfano Chad na Mauritania) ambao wameitwa “majihadi wa kijambazi” na vyombo vya habari.
Anayefaidi nani?

Si mwananchi wa kawaida bali watengeneza mabomu na silaha. Kadri makundi haya yanavyoendelea kujijenga ndivyo makampuni ya silaha Uzunguni yanavyotajirika. Mbali na silaha zinazouziwa magaidi na wanajeshi wanaobaka wanawake Kongo,  Sudan na Somalia  yapo makampuni makubwa makubwa yanayoshirikiana na serikali Afrika.
Dini si chanzo bali matokeo. Na haya ndiyo yanayochanua  Bongo. Wananchi wamechoshwa na maneno matupu ya wanasiasa.  Mauaji ya polisi, uchomaji makanisa ( Dar na Zanzibar) kuota mabawa chama cha Uamsho, Unguja ni dalili za mvua ya radi. Ingawa Uamsho haina nguvu kama Boko Haramu, Ansar Dine na Al Shabab, kuwepo kwake kunadhihirisha kuenea kwa waasi wanaosingizia dini  Afrika.
Miaka hamsini iliyopita majeshi  yalikuwa na desturi yakupindua serikali  kujaribu  kurejesha hali njema Afrika. Leo wanadini wanachukua nafasi hiyo hiyo.  Lengo la dini ni amani ya kiroho na ya majeshi ni kulinda taifa. Serikali si idara yao.  Paka asipokuwepo Panya hutawala. Wanasiasa na viongozi wanaposhindwa kazi  wanadini au wanajeshi  hukamata pale matumaini yalipokosekana.  Hali  hii inathibisha namna  Afrika inavyohitaji uongozi na mabadiliko ya kweli.

London:  6 Novemba, 2012- Ilikataliwa kuchapwa...


No comments:

Post a Comment