Wednesday 30 March 2011

KITABU KINACHOELEZEA YALIYOWAFIKA WAPINZANI TANZANIA CHATOKA UINGEREZA...

Kina kurasa 272.
Toka nchi yetu iwe huru miaka hamsini sasa hajatokea Mtanzania akaandika kitabu cha aina hii.  Watanzania tunaogopa. Hofu hiyo imeenea miaka mingi na imetushika hata sisi wanahabari wenyewe.
<--more!-->
Hata waliohusika na upinzani wa maadili, siasa au uongozi wa nchi hawakuandika vitabu au kuelezea yaliyowapata. Kiongozi wa kwanza wa zamani kutoa kitabu chochote kinachoangalia masuala ya kisiasa katika ngazi za juu ni aliyekuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu  Tanzania  Edwin Mtei. Kitabu hicho (“From Goatherd to Governor” , Mkuki na Nyota, 2009) kinamweleza Mtei alivyokulia Kilimanjaro, akamaliza masomo Makerere, akawa serikalini na hatimaye kuanzisha CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo)  1992.
Watanzania wa ngazi za juu hawaandiki vitabu.
Linganisha tabia hii na ya wenzetu. Viongozi wawili wa Kenya, marehemu Tom Mboya (aliyeuawa kwa bunduki, Nairobi, 1969) na  Rais Jomo Kenyatta ( aliyefariki, 1978) walichapa vitabu vya maisha yao. Nelson Mandela keshatoa viwili. Umuhimu wa vitabu vya vigogo si tu kutuelemisha bali kusaidia vizazi baadaye kuelewa jamii zao.
Kwa viongozi wa Kizungu maelezo ya wanaserikali na watu mashuhuri ni vile vile  biashara. Waziri Mkuu wa zamani  Uingereza Tony Blair (1997-2007) hapendwi sana na watu wake (kutokana na vita vya Iraq)  lakini alipomaliza awamu mbili aliandika kitabu kilicholipiwa paundi milioni tano (takribani shilingi bilioni 12) kabla hata hakijatoka.
Sisi hatusomi wala hatuandiki vitabu.
Mpinzani  wa mwanzo wa siasa ya Ujamaa na mtetezi wa demokrasia nchini marehemu Oscar S. Kambona (aliyefariki London 1997) hakuandika kitabu. Mzanzibari maarufu  aliyekuwa Waziri wa Uchumi  serikali ya Muungano, Abdulrahman Babu (akafariki pia hapa London 1996) baada ya kuwekwa kizuizini kufuatia mauaji ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Amani Karume (1972) hakutuachia kitabu. Na Baba wa Taifa mwenyewe Mwalimu Nyerere hakuandika  kuhusu maisha yake.
Ndiyo maana hili si andiko la kawaida.
Mwandishi ni Mbongo ambaye amekuwa mkimbizi toka alipoachiwa kizuizi alipofungwa na serikali 1983- 1985 anasema tafsiri ya kitabu kuja Kiswahili itakuwa tayari kuuzwa Afrika Mashariki (kwa bei nafuu kuliko ya sasa Majuu) mwezi Mei au Juni.
Kilichapishwa mara ya kwanza 1994 (Dark Side of Nyerere’s Legacy) na kampuni ya Wisdom House Publications mjini Leeds kilometa 273 toka London kaskazini ya Uingereza; kama  umbali wa Tabora hadi Mwanza. Toleo la sasa limeongezea utangulizi, maelezo zaidi na picha mbalimbali.
Anaitwa  Ludovick Mwijage.
Habari za kimataifa za mzawa huyu wa Ziwa Magharibi zilianza kuandikwa mwaka 1985 akilalamika kuteswa na kufungwa katika gazeti la “New African” linalochapwa London.
Anasema katika utangulizi  kwamba  alimpelekea nakala Baba wa Taifa, mwaka 1994:
“Nilitegemea Nyerere angeangalia masuala niliyoongelea kitabuni na kuyahakiki wakati akiandika kuhusu maisha yake. Hata hivyo Nyerere hakuandika kitabu jambo ambalo si la kawaida kwa mtu aliyewahi kutafsiri  “Mabepari ya Venisi” cha William Shakespeare kuja Kiswahili na mara kwa mara kuandika maoni ya uhariri  gazeti la serikali la Daily News.”
Je, anaongelea nini kizito?
Kwanza anaangalia suala la demokrasia na uhuru wa kujieleza.
Anatoa majina ya takribani wapinzani WOTE,  waliowahi kufungwa au kuuawa na serikali, bara na visiwani, picha zao na familia, kuelezea mitazamo yao na vipi walipotea bila kujulikana walipokwenda.  Mengi ya majina na habari enzi zile  za uongozi wa Mwalimu Nyerere  yalinong’onezwa kwa woga na dharau. Kuanzia  Abdallah Kassim Hanga, Oscar Kambona, mwandishi wa habari Melek Mzirai Kangero (aliyeandika habari kuhusu Kasella Bantu, 1968 na kutiwa mbaroni) ;  wapinzani mashuhuri waliofikishwa hatiani miaka ya Sabini akiwemo Bibi Titi Mohammed na Mchungaji  Uria Simango  aliyehukumiwa kifo mwaka 1975 chini ya Rais wa Msumbiji marehemu Samora Machel. Au habari za kijana aliyeteka nyara ndege ya Shirika la Tanzania (1982)  Mousa “Lee” Membar na hatimaye kuuawa baada ya kukimbilia Uingereza. Ama Wazanzibari waliofungwa au kuuliwa: Sheikh Othman Sharif, Salehe Sadala Akida, Sheikh  Ali Muhsin Barwani,  Sheikh Shamte na kadhalika.  Anaelezea pia suala la wapinzani kunyang’anywa uraia mathalan Kambona na karibuni mwandishi maarufu wa habari Jenerali Ulimwengu. Anasaili, je, kifo  cha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Sokoine, kilikuwa kweli ajali?
Lakini haelezi tu wapinzani wa kisiasa bali watu wa kawaida waliotiwa ndani kwa kutengeneza gongo au uhalifu mdogo  wakafungwa shauri hawakuhonga askari wetu. Ama wakimbizi wa Afrika Kusini na Rwanda walioteswa au kuuawa Tanzania, kisirisiri.
Hilo mosi.
La pili lamhusu mwasisi wa Jamhuri ya Tanzania. Anauliza katika jalada la kitabu: “Julius K. Nyerere : Mtumishi wa Mungu au Mtawala Dhalimu?”
Anaangalia pendekezo lililotolewa kwa kanisa la Kikatoliki kwamba Nyerere apewe utakatifu.
“Habari hizi  ziliwastua wale walioghafilishwa na serikali ya Nyerere na familia zao...” anaandika ukurasa 12.
Anauliza vipi Mwalimu hakuruhusu upinzani ? Anaangalia  suala la amani ambalo ni taswira kuu ya Tanzania. Anatoa mifano ya nchi  zenye machafuko mathalan Ethiopia, Ivory Coast, Sierra Leone na Liberia. Anadai masuala yaliyosababisha tafrani zake  kama umaskini na ufisadi yameshaota mizizi Bongo.
“Kwa mfano, rushwa imeenea Tanzania leo ; lazima iangaliwe iwapo hali hii haitazusha utawala mwingine au kuharibu kabisa amani yetu ya baadaye.”
Mwandishi Kaijage mkazi Denmark anaelezea kirefu alivyokamatwa, akateswa na kufungwa akiwa Swaziland mwaka 1983 hatimaye kusafirishiwa Tanzania. Anadai aliteswa kutokana na msimamo au mawazo tofauti miaka ile ambayo fikra za aina hiyo hazikuruhusiwa. Kaweka picha mbalimbali  akiwa jeshini Makutupora, Dodoma (1970), akihutubia kikao cha haki za kimataifa (1983) au bega kwa bega na Oscar Kambona (1992).
Hiki ni kitabu kinachochimba mambo yasiyoongelewa au hayajawahi kuzungumziwa waziwazi Tanzania. Masuala ya usalama wa nchi na haki ya kuongea ukweli.
Wapo watakaodai maandishi yanasaliti nchi; wapo watakaoulizia nini hasa malengo ya mwandishi. Ila yabidi kila mzalendo anayeijali nchi hii akisome na kufikia uamuzi wake mwenyewe. Kinaweza kuagizwa duka la Amazon mtandaoni  au: simon.mwijage@gmail.com . Simu +32-470521663, +45-50290427. Anuani ya posta : Ludovick S. Mwijage, Jagtvej, 215B, 3-2, 2100 Copenhagen, East Denmark. Bei pamoja na usafirishaji ni Kroner 139 ( kama shilingi 39,000).
 -London, Jumanne, 22 Machi,  2011


Ilitoka Mwananchi, Jumapili Machi 27, 2011.
Na Citizen, Ijumaa Machi 25, 2011.
http://thecitizen.co.tz/editorial-analysis/47-columnists/9352-a-chat-from-london-book-on-who-is-who-in-tanzania-opposition-history


5 comments:

  1. Kaka Macha,
    asante kwa taarifa hizi njema za kitabu cha ndugu Mwijage. Ni kweli kuwa wabongo wengi sana hatutengi muda kusoma achia mbali kuandika juu ya mada mbalimbali. Ni dhahiri kuwa mabadiliko ndo kitu cha kudumu; hivyo utamaduni wetu mbaya wa kutokusoma na kuandika unaweza kubadilika kwa juhudi binafsi na pia za viongozi wetu.

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa taarifa ya kitabu hiki kinachoeleza yaliyowafika wapinzani Tanzania, THE DARK SIDE OF NYERERE LEGACY. Vile vile kwa jina la kitabu cha Mtei ulichotaja, FROM GOATHERD TO GOVERNOR.

    ReplyDelete
  3. aksante sana kaka, nime-google leo habari za nyerere baada ya kusikia mambo ya utakafifu na kukuta ishu yako hii

    ReplyDelete
  4. Ni jambo jema sema kutufahamisha baadhi ya mambo yaliyokuwa yamefichwa

    ReplyDelete
  5. Ni vizuri kutujuza mambo hayo lakini Mwalimu alikuwa anafanya siasa za kweli na alimaanisha nn anachokisema kutoka moyoni lakini ninyi wengine ni janjajanja tu kuleta maneno matamu na kutafuta huruma ya watu kwamba mlionewa.

    ReplyDelete