Showing posts with label Watanzania Uingereza. Show all posts
Showing posts with label Watanzania Uingereza. Show all posts

Monday, 23 November 2015

FAB MOSES - MTABIRI WA LONDON ALIYETUNGA WIMBO WA KUSHINDA MAGUFULI


Wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea miezi kadhaa iliyopita, Mtanzania mmoja mkazi London alikuwa na mtazamo tofauti. Mwanamuziki na mcheza sarakasi huyu  anaitwa Fab Moses.
“Nyinyi semeni yenu mnayotaka, lakini CCM na Bw John Pombe Magufuli watashinda tu.”
Rais wa Jamhuri ya Tanzania,  J P Magufuli.   Picha ya Blog la Yinga Boy


Fab Moses si maarufu kwa utabiri bali kwa ucha Mungu wake, upole na ukarimu. Si wale wanaojifaragua au kupiga kelele mbele za watu. Mtaratibu anayejishughulisha na kazi mbalimbali za ajira  za uchovu tosha. Chukua mfano siku niliyomtembelea kwake kumfanyia mahojiano haya. Ilibidi miadi ipangwe saa tisa alasiri, maana aliingia kitandani asubuhi hiyo baada ya kazi ya usiku kucha.

Monday, 16 June 2014

USIKU KUCHANGIA JENGO LA WASICHANA WANAOKWEPA UKEKETAJI TANZANIA


Niko hoteli kubwa la The Russet, katikati ya maskani ya wafanyakazi wa kawaida, kaskazini ya  London. Nimealikwa kutumbuiza ngoma za Kiafrika. Mauzo ya sherehe hizo yatasaidia kijiji kimoja Tanzania. Watayarishaji ni shirika la urafiki baina ya Uingereza na Tanzania, BTS yaani British Tanzania Society. Janet Chapman na mwenzake Jonathan Pace, ni wale wazungu wachache wanaofikiria mazuri tu kuhusu Waafrika, hususan Watanzania.
  Watu wa makamo.
Miaka 30 iliyopita  Janet alifanya kazi ya ualimu Sudan,  vijijini; akichanganyika na wakulima na wafugaji maskini. Kati ya jambo ambalo hakulipenda ni mila ya kuwatahiri wasichana wadogo au kwa Kiswahili cha kileo, ukeketaji.  Janet anasema kwa kuwa mwenyewe alikuwa na mabinti wadogo wawili- ambao leo wameshakuwa watu wazima- yalimgusa sana. Baadaye aligundua adha hii imeenea nchi nyingi   bara Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

 Takwimu za shirika la Afya duniani (WHO) zinakadiria wasichana na wanawake milioni 91 na nusu barani wamekeketwa. Kati ya hawa milioni 12 na robo wana umri mdogo wa miaka 10 hadi 14.  Tovuti la habari za ukeketaji (FGM) linadai nchi 26 za Kiafrika, ikiwemo Tanzania zinabeba bendera ya ukeketaji. WHO inafahamisha kati ya wanaotetea adha hii ni mama wazazi waliokeketwa na  baadhi ya wanaume.

Sunday, 31 July 2011

ANNA LUKINDO: MBUNIFU MAVAZI NA MITINDO ANAYEKUZA JINA LA WANAWAKE WA KITANZANIA LONDON

Hebu turudi nyuma miaka 30.
Tanzania ndiyo imemaliza vita kumwondoa Jemadari Idi Amin Dada ; maisha magumu maana serikali imetumia mabilioni ya shilingi kununua silaha kujenga jeshi imara kuwasaidia Waganda. Bidhaa adimu madukani. Hata chakula kinacholimwa nchini (mathalan unga) kazi kukipata. Utata.
 Licha ya kitatange na mahangaiko maelfu ya wakimbizi wamekaribishwa nchini toka  Afrika Kusini, Angola, Namibia na hiyo Uganda yenyewe. Kisiasa Watanzania waungwana sababu ya uongozi wa Mwalimu Nyerere aliyeujua wajibu wake wa kijadi kwa Waafrika wenzetu.  Ni kipindi hiki ndipo miye na wenzangu watatu tulipounda bendi ya mseto wa fasihi na muziki tukaiita “House of Africa.” Ilikuwa vigumu kumpata mwanamke maana enzi hizo jamii yetu iliwabeza kina dada waliofanya sanaa.
Imetolewa pia safu ya "Kalamu toka London" kila Jumapili, gazeti la Mwananchi:
Waliitwa mabahaluu, wavuta bangi, machangu doa; kuimba jukwaani hakukuwa na heshima wala ajira kama walivyo Kizazi Kipya leo...Wakati sisi tukihangaika, Anna Lukindo alikuwa akionyesha mavazi hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam siku za wikiendi. Kikazi aliajiriwa na kampuni ya kusanifu nyumba barabara ya Mkwepu. Bado mdogo ana miaka 19, lakini mchapa kazi ile mbaya.
Anna Lukindo akiwa kazini. Anayevalishwa ni mwanamitindo, mpiga picha na mwanabloga, Jestina George . Picha na See Li.

<--more--!>