Sunday, 17 March 2019

KISWAHILI CHETU KINADIDIMIZWA NA KUPANDISHWA NA NANI?


Nilimhoji Mkenya mmoja kwa kipindi  cha Kwa Simu Toka London. Jina nitalihifadhi kwa sasa. 
“Nikiwa mdogo sikupenda kabisa kwetu Kenya tulivyolazimishwa kujifunza Kiingereza.  Tulichapwa...”
Nikasema ndiyo maana Kenya na  Waafrika wengine huzungumza Kiingereza  ( na lugha zingine za Kizungu ) kwa ufasaha sana.
“Lakini nilipofika hapa Uingereza nilishangaa au tuseme nikajifunza. Waingereza wanaipenda sana lugha yao.  Huongea tofauti na sisi tunavyoongea. Ukitaka uraia wa Uingereza lazima ujue Kiingereza sawasawa.  Wanakithamini Kiingereza. Majina, barabara, shule, serikali, muziki,magazeti, vitabu, kila kitu.  Hawatumii lugha nyingine. Hawakidunishi. Wala hawakichanganyi na lugha nyingine. Nikatafakari. Ndipo nikaanza kuifikiria Tanzania...”
Akadai miaka mingi amependa sana msimamo wa Watanzania.
  “Zipo nchi kumi na moja zinazungumza Kiswahili. Lakini chimbuko la Kiswahili ni Tanzania. Hata wengine tukijidai, hatuifikii Tanzania...”
Mara, mhojiwa akapaaza sauti.


“Miaka michache iliyopita Tanzania imekichuja kabisa Kiswahili.  Mimi sina zaidi ya miaka arobaini, lakini nafahamu kuwa Tanzania ilikuwa ikitumia kila kitu Kiswahili. Miaka ya karibuni kizazi chenu kipya kimeanza kukiua kabisa Kiswahili. Kila ninaposikiliza vipindi vya TV naona watangazaji wakiongea Kiswahili kisha wanachanganya na Kiingereza. Sijui mnakwenda wapi. Nadhani baada ya kizazi hiki kuzeeka, Kiswahili kitatokomea...”
Mhojiwa akaongea mambo mengi...
Hebu tumwache...
Kila kukicha mitandao jamii inasambaza video za wageni  (hasa Wazungu) wakizungumza Kiswahili fasaha. Walisoma vyuo vya nje. Wengine wameishi Tanzania mida sasa wanazungumza Kiswahili vizuri sana.
Miaka michache iliyopita video ya Wazungu wakiimba wimbo wa “Tanzania Tanzania Nakupenda kwa Moyo Wote” ilisambazwa mtandaoni. Hawakuwa wakichanganya wimbo huu mtukufu na lugha zao za Kizungu.
Karibuni  wanafunzi wa lugha za Kiafrika walimfanyia sherehe kumwaga mhadhiri wa Kiswahili chuo cha Leipzig, Ujerumani, Abdilatif Abdala.  Mmoja wa magwiji wakuu wa Kiswahili; mzawa wa mwambao wa Kenya na kitabu chake cha mashairi “Sauti ya Dhiki” kilicho maarufu sana. Wazungu hao walimwimbia kumuaga Bw Abdilatif  huku wamevaa vitenge vya Kiafrika. Wanaume kwa wanawake. Wakisifia na kuukabali Uafrika. Kama sisi tunavyosifia na kuukubali Uzungu kwa majina, magari, simu za mkononi, nk.
Kwanini wameuheshimu?
Na ikiwa sisi tunadunisha lugha zetu nani atatuheshimu?
Akizungumza na Mbeya TV Agosti 2017,  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Harrisson Mwakyembe, alisema kati ya  lugha 6,000, Kiswahili ni lugha ya kumi, na ya pili bara Afrika. Imepangwa kuwa lugha mosi Afrika 2063.
Wanaochangia kudunisha lugha si wananchi wa kawaida. Ni watangazaji wa redio, TV, wanahabari, mabloga, viongozi wa kisiasa, waalimu, nk.
 Kiswahili kikizungumzwa lazima kipakiwe neno la Kiingereza.
Kwanini mtangazaji wa TV aseme “Legendary Remmy Ongala” badala ya “gwiji” au “nguli” ? Au mwanasiasa adai nchi yetu inakosa “Organisation” si “Utaratibu”? Hapo kuna ukosefu wa misamiati na udunishaji lugha.
Tunajidunisha.
Kama wanawake wanaovaa nywele za maiti au Waafrika wanaojichibua ngozi wawe rangi chungwa.
Wenzetu wanatucheka.
Hutusema hatuwezi Kiingereza sawasawa. Moja ya kazi zangu hapa Majuu ni kusahihisha vitabu na miswaada ya Kiingereza. Waandishi wa Kitanzania wanashindwa  kuandika lugha hii sawasawa. Sababu kuu ni kuzoea kuchanganya- Kiswanglish- sasa unapokuja wakati wa kuandika Kiingereza tasnifu tunaharibu.   


No comments:

Post a Comment