Wednesday, 20 July 2016

LAWI SIJAONA MFANO WA NAMNA TUSIVYOTHAMINI KUMBUKUMBU ZETU


 Wabunge wa TANU mwaka 1959. Picha ya Facebook.

Moja ya mambo makubwa niliyojifunza Ughaibuni ni namna wenzetu, (hasa weupe) wanavyothamini mambo YAO ya kale. Na tunaposema “kuhifadhi” si tu watu maarufu au kadhia fulani fulani za kiserikali.  


 Chukua vyakula. Zamani Wazungu walikuwa wakioka mikate katika majiko ya mikaa, kama leo Afrika. Majiko hayo yalikuwa aina ya tanuri. Kuna kipindi kilioneshwa mwaka jana kuhusu historia ya mapishi. Wakachagua wapishi wanne wa kisasa. Wakawavalisha magwanda ya karne ya kumi nane na kumi na tisa.  Tukaoneshwa wakikanda unga na huku ule mvuke na moshi vikiwaghasi. Wapishi wa “kizazi kipya” wakapata shida sana. Mikate ilipokuwa tayari wakaionja. Wakasema mitamu sana.
 Lakini ilikuwa pia na chumvi. Ambapo siku hizi kuna uchaguzi Uzunguni wa chakula chenye chumvi au kisichokuwa nayo. Chumvi si kitu kizuri sana kiafya hasa moyo. Moja ya mafunzo hapo ikawa kuwa leo tunaishi kwa afya zaidi kuliko zamani. Wastani wa maisha ya wananchi karne hizo ulikuwa miaka arobaini  kama ilivyo nchi maskini. Leo Uzunguni ni miaka 80.
Tuje kwenye umaarufu.
Kanisa la Westminster Abbey, London

Makaburi ya wafalme, wasanii, na wagunduzi yamehifadhiwa. Mjini London kuna kanisa maarufu la Westminster Abbey ambapo watu muhimu wamezikwa toka karne nyingi. Afrika bado tunasoma vitabu vya  mwanariwaya Charles Dickens, mtunzi Mwingereza  aliyeng’aara karne ya 19. Kaburi lake lipo  Westminster Abbey. Nyumba aliyoishi imehifadhiwa . Ukiitembelea shurti malipo.
Mwanafasalfa mashuhuri wa Kirumi (Italia) aliyeishi karne ya 15 na 16 ni Nicollo Machiavelli. Mwanafasalfa huyu aliyefariki 1527 anasomwa na takriban kila kiongozi duniani.
Kitabu chake  mashuhuri “The Prince” ni kama msahafu kwa wanasiasa:
  “Ni bora kuogopewa kuliko kupendwa; kama huyawezi yote mawili  bora zingatia la kwanza.”
 Ama: “ Ukitaka kujua akili au uerevu wa mtawala chunguza wale waliomzunguka.”
Ingawa aliandika vitabu vingi, The Prince (Mwana wa Mfalme) kinafahamika zaidi.
Kimehifadhiwa (pamoja na chumba na hata meza) aliyoishi mjini Florence, Italia.  Miaka mingapi?
Piga hesabu. Toka 1527!
Linganisha na sisi.
Karibuni tunaweza kuhesabu mangapi tuliyoyaenzi?
 Kaburi la Mtemi Mkwawa, pale Kalenga , Iringa. Safi. Mti alionyongwa Mangi Meli wa Old Moshi, Uchagani, na wakoloni wa Kijerumani, mwaka 1892. Safi. Mengine, je? Je ukitaka kusoma magazeti ya Uhuru na Mzalendo- niliyokuwa nikiyaandika mwaka 1976?- Je, ukirudi nyuma zaidi hadi Raha Leo aliloandikia Shaaban Robert miaka ya 1940 na 1950? Je kaburi la Shaaban Robert? Je ni kweli kwamba ukitaka kusoma magazeti yetu ya nyuma yameishia mwaka 1982? Je Radio Tanzania? Je ukitafuta sinema aliyoigiza mmoja wa waasisi wa taifa, Rashid Mfaume Kawawa (Muhogo Mchungu) utaipata?
Lazima tujiulize maswali.
 Maana sasa hivi kuna mgogoro na kero inayowasakama watoto, wajukuu na familia ya aliyekuwa zamani Waziri katika awamu ya kwanza ya Tanzania. Wangapi wanamkumbuka Lawi Nagwanda Sijaona?
 Lawi Sijaona ...picha ya Mtandao wa Wazalendo.

Karibuni nilisoma ukuta wa Facebook ambapo picha iliyopigwa mwaka 1959  Bunge la kikoloni, inawaonesha vijana wa enzi hizo, Waafrika wa kwanza kwanza kuingia Bungeni.
Legco. Kirefu chake ni “Legislative Assembly of Mainland Tanganyika.”
Lilianzishwa mwaka 1926 na aliyekuwa Gavana wa  Waingereza nchini, Bwana Donald Cameron. Jumla wabunge 20. Picha hiyo ya 1959 inao Richard Wambura, George Kahama, Amir Jamal, Paul Bomani, Rashid Kawawa na Lawi Sijaona. Vijana hawa walikuwa miongoni mwa timu iliyokuwa sambamba na Mwalimu Nyerere kugombania Uhuru wa Tanganyika. Baadaye tukashinda Uhuru. Wakafanywa Mawaziri.
Mishahara yao  ililipwa hela ya malkia, yaani Paundi. Rais alipata paundi 3,000 kwa mwaka na Mawaziri wake, £2,300.
Leo mtu akikupa paundi 3,000 ni shilingi milioni 8 na nusu. Ndiyo ni nyingi kwa mtu wa kawaida. Lakini enzi hizo ilikuwa nadra sana kwa mtu kutafuta  uongozi wa kisiasa ili kuiba fedha au kufisadi. Walikuwepo “kupe”  (neno Mwalimu Nyerere alilotumia kwa “mafisadi” ) lakini ukweli hakikuwepo kitu cha kuiba. Nchi ilikuwa bado inaanza kutembea.
Sikiliza mwandishi wa Facebook:“Lawi Nang'wanda Sijaona ni mmoja wa wapigania uhuru wa Tanganyika, akifanya kazi kubwa ya kuasisi vyama vya siasa vya ukombozi, tangu TAA, TANU na hatimaye CCM. Alikuwa kiongozi na mzalendo wa mfano wa aina yake, Akifanya mambo mengi makubwa na ya kukumbukwa....Hakuwa "Fisadi", "Mwizi" wala "Mla Rushwa", alikuwa mwadilifu na mtu aliyelinda kwa nguvu kubwa Rasilimali za Nchi hii. Kumbe, mwisho wake akafa, akazikwa na mema yote. Akasahaulika!.”
Hiki ni kimoja cha visa vingi.
 Tumesikia baadhi ya viongozi kuuawa kutokana na kujaribu kutekeleza siasa za nchi. Mathalan Dk Wilfred Kleruu aliyepigwa risasi na mkulima  wa Iringa mwaka 1972. Baadaye,  Saidi Mwamwindi alinyongwa. Uzuri wa kisa hiki ni watoto wawili wa marehemu ( Eva Kleruu na Amani Mwamindi – Meya wa Iringa)  kukutana mwaka juzi na kufanya maridhiano – yaani kusameheana.
Hii inakumbusha pia mtoto wa Nduli Idi Amin na Mwalimu Nyerere ambao wamekuwa wakiwasiliana miaka mingi kufuta tofauti za baba zao.
Haya ni machache ya historia yetu.
Lakini je mmesikia barua iliyoandikwa na mtoto wa Waziri huyo wa zamani Lawi Nagwanda Sijaona , mwezi jana kumtaka Mheshimiwa Rais John Magufuli ajaribu kusuluhisha jambo linaloikera familia yake?
Barua inazungumzia kisa cha Mwenge mwaka 1998 maeneo ya Newala, Mtwara. Mheshimiwa Waziri mstaafu Sijaona enzi hizo (kwa mapenzi yake ya taifa) aliazima jenereta la umeme kusaidia shughuli  za kukimbiza mwenge. Hadi alipofariki,  2005- barua ya mwanae inadai-mashine haikuonekana. Barua inadai :
  “Jenereta  ilipotea ingali mikononi mwa Serekali na shauri hilo kufikishwa Mahakamani kama inavyosomeka hati ya hukumu,kesi ya jinai namba 322/1999 na inaeleza thamani yake kwa makadirio ya shs 1,500,000 na kwamba mmiliki wake ni Mzee Lawi  Nangwana Sijaona.”
Barua inaendelea kwamba hadi leo, viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa awamo ya nne walielezwa mgogoro. Uamuzi wa kuandika barua ya wazi kwa Rais Magufuli unasisitiza kumbukumbu ya mzee huyo kutothaminiwa, anadai mwanae.
Bila shaka wapo wananchi wengi waliofanya mema na ya maana nchini ambao hawakumbukwi. Marehemu Sijaona ni mmoja wa  wanaotukumbusha haja ya kuwaiga wenzetu wanavyoweka heshima za mababu na mabibi zetu kwa karne nyingi.
Habari zaidi wasiliana na Adam Sijaona simu 06581-45681 au 0782704208.

 

-

No comments:

Post a Comment