Monday 18 August 2014

KWA WANAOLILIA MAPENZI NA WAGENI AU WAZUNGU...- Sehemu ya 1

Miaka ya karibuni  wananchi wengi- hususan vijana- wameulizia mahusiano ya kimapenzi na wageni  hasa Wazungu. Hayakuanza leo, jana wala juzi. Yamekuwapo daima. Ukweli idadi fulani ya watu wa mataifa yote duniani hutaka kuwa na mahusiano na wageni. Mosi, kutaka kuondokana na udhia wa wananchi wenzao; pili, kutafuta maisha bora; tatu,mapenzi na ndoa na nne, udadisi (kipya kinyemi).
Mwandishi nikitumbuiza ngoma wakati wa  Carnival  la London, Agosti, 2012.

Miaka arobaini au hamsini iliyopita nakumbuka waliopenda mahusiano na wageni walikuwa zaidi wanaume. Wanawake waliojamiiana na wageni waliitwa malaya, na wachache ni wale tu waliofanya kazi mahoteli makubwa ya kitalii kutafuta ajira. Mathalan nakumbuka miaka ya Sitini na Sabini, Tanzania ilijazana wakimbizi. Sera ya TANU na siasa ya Azimio la Arusha ilisaidia walioathirika na udhalimu wa kikoloni, ubaguzi nk. Toka Kongo, Afrika Kusini,Palestina, Malawi, Marekani, Uganda, nk.


Wengi wa wakimbizi wa Kongo (iliyoitwa Zaire enzi za utawala dhalimu wa Jemadari Joseph Mobutu) walikuwa wanaume, hasa wanamuziki,  waliohusudiwa sana na wanawake wetu. Mzaire aliongea  Kiswahili -chenye lafudhi ya Kifaransa na Kilingala-  kilichomfanya avutie kwa utofauti na mwanaume wa Kitanzania.  Au wakimbizi wa Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe. Tuliwaita Waafrika Kusini,  “Wasoweto” kutokana na harakati au machafuko ya kitongoji cha Soweto mjini Johannesburg mwaka 1976. Wasoweto walikuwa tofauti. Walivalia suruali pana pana. Waliongea Kiingereza fasaha. Vijana wa kiume na kike tuliona akheri kubwa kwenda na Wasoweto kuliko wazalendo wenzetu. Miye kwa mfano nilikuwa na sahiba  aliyependa fasihi, mashairi na kupiga muziki.

Awali nilipata shida sana – na miaka yangu ishirini na moja au miwili-, kupata sahiba wa kike aliyependa fasihi na muziki. Wasichana wa rika langu walitaka kwenda baa, kunywa bia – na vile ka- mshahara kangu ka uanahabari magazeti ya Chama (Uhuru na Mzalendo) kalivyokuwa nyau, haikuwa rahisi kubembelezana na dada zangu, hata wawe wazuri namna gani. Aghalabu, kadri uzuri ulivyozidi ndivyo karaha ilivyoongezeka.
Wasoweto hawakujali. Azma yao ilidai uhuru; walipenda utamaduni wa michezo na kusoma vitabu. Mkikosa fedha ya basi au teksi mnatembea tu kwa miguu mkiongelea haiba ya mawingu, maua waridi, misufi, twiga, muziki wa Jazz, Taarabu, hadithi za Ali Nacha na siasa za Wapalestina. Mkifika hivyo hivyo ugali  kwa maharage na ndizi kisukari. Mnasoma mashairi ya Shaaban Robert na Christopher Okigbo (Mshairi wa Nigeria aliyefariki angali kijana mwaka 1967) baadaye usingizi wa mapenzi ya joto la Dar es Salaam. Au mnakwenda tu ufukwe wa bahari kufurahia mandhari. Hayo ndiyo mapenzi ya kweli. Si mapenzi ya kutegemea mfuko kwanza. Fedha na  baa hufuata baadaye. Kinachotangulia mapenzi asilia.
 Kwa kina dada mambo pia hayakuwa rahisi. Kijana wa kikwetu akishakutoa dada, -akikununulia zito, jepesi na la wastani- ukishafurahi unakuwa sasa mtwana wake. Kuna siku utapigwa. Utasutwa.  Iko miezi utawekwa hata mimba na jamaa hatoonekana kumtunza mtoto. Baadaye utagundua ala kumbe! Kapata mwingine.
Uafadhali ulionekana kwa Wamarekani weusi. Warefu, wazungu weusi, wenye tabia tofauti na zetu. Waliongea kile Kiingereza cha “bradha- man” na “sista-du” kiliichoonekana kitamu. Wakimbizi na watembezi wa Kimarekani walijazana Tanzania ya kipindi hicho. Walizikimbia tafrani za Marekani: ubaguzi wa ngozi, harakati za chama cha Black Panther kilichochukua bunduki kupigana na nguruwe weupe. Hadi leo haujaisha. Enzi hizo mwanamke wa Kitanzania akimwona “Mniga” (kama tulivyowaita mitaani) ni kama kumshuhudia mdogo wake Mungu. Astakafurlah! Macho huwatoka kina dada; ndimi nje. Walijua kuongea na mwanamke, walifuzu mapenzi. Ni kama Wanigeria wanavyohusudiwa na wanawake wetu leo. Kipya kinyemi. Baadaye iligundulika hawakuwa tofauti na wanaume wazalendo.
Miaka imevuta miguu; leo wanawake weusi hawataki wanaume weusi ki- jumla. Mwanaume mweusi hakosi nyumba ndogo au tatu. Mwanamke mweusi keshamfahamu kaka yake. Keshamjua. Akishamkubalia huba au mahaba, hatokuwa yeye tu. Hilo limeenea Majuu yote. Limeenea kiasi ambacho dada weusi hawana imani na kaka zao. Wameanza kusaka Wazungu. Zamani Mzungu hakupendwa sana na mwanamke mweusi. Wapo dada wachache waliokwenda na Wazungu ndiyo; ila wengi walidai ah Mzungu hana nguvu kitandani. Au walilalamika wajihi wa ngozi haukuwavutia.
 NGOZI IKOJE SIJUI...
Leo mengine. Kinachotafutwa ni mapenzi na mahusiano si kitanda au fedha tu..
Hivyo basi, mapenzi yanayodumu, yanayowezekana ni baina ya mwanamke mweusi na Mzungu. Sikiliza...
Wakati harakati za ukombozi wa wanawake wa Kizungu zilizofoka moshi miaka ya Sitini, wanawake waligeuza mahusiano. Miaka ya Sabini uzunguni kote ulikuwa wakati wa wanawake kudai usawa makazini, kuwataka wanaume waache udhalimu nk. Leo wanawake wa Kizungu ndiyo watawala wa nyumba,  hata sehemu za kazi za kijamii. Wanawake wa Kizungu wanatawala mazingira kiasi ambacho kura za kisiasa zinawaegemea. Hapa Uingereza kuna mfano mzuri, kisiasa.
 Mwezi uliopita Bwana David Cameroon, Waziri Mkuu (na kiongozi wa chama cha Conservative) alibatilisha baraza lake la Mawaziri. Badala yake alichagua wanawake zaidi. Inadaiwa kafanya hivyo kutafuta kura za wanawake uchaguzi ujao wa 2015.
 Mbinu hizi zilitekelezwa pia na Waziri Mkuu wa zamani, Chama cha Leba, Tony Blair, alipoingia madarakani, 1997. Alifanya historia kwa kuwa na wabunge 101 wa kike , baadhi walishika vyeo vya uwaziri!  Waliitwa “Blair’s Babes.”Hadi leo wengi bado wamo serikalini. Huo ni mfano mdogo unaodhihirisha namna mahuasino yalivyobadilika kuanzia mapambano ya haki za akina mama yalipochachamaa Ulaya miaka hamsini iliyokwenda.
Wanawake wanatawala na ni wakali. Baadhi ya wanaume wa Kizungu huona afadhali kuwa na wanawake wa mataifa mengine –  Asia na Afrika. Hawa nao huwa wamechoshwa na wanaume wasioaminika. Hapa basi watu wawili hawa  walioshakereka, hukutana. Ndiyo maana leo mahusiano baina ya wanawake weusi na wanaume wa Kizungu yanastawi sana.
Tanzania je? Wengi wanaandika kuulizia mahusiano na Wazungu. Ugumu wa maisha unajenga ari za kumpata mgeni kujiendeleza. Je kuna wepesi na uzito gani? Tuendelee na mazungumzo juma lijalo.


-Ilichapishwa 10 Agosti 2014 na Mwananchi Jumapili










                

No comments:

Post a Comment