Sunday 22 June 2014

KISWAHILI NA MAHUSIANO YETU NA UTAMADUNI WA KIARABU


 Shangwe zilizoenea Ulaya nzima sasa hivi ni mashindano ya soka, Brazil.
 Ila wasiwasi uliowashika wanausalama wanaojua mikunjo kunjo ya shuka na kanzu za ulimwengu wetu ni tafrani kali zinazoendelea Syria na Iraq. Wasiwasi wa  mashushushu na wanasiasa Majuu ni hatari zitakazoenezwa na migogoro hii. 
 Uingereza mathalan imedai  vijana 400 wazawa  hapa, wanapigana Syria. Wakimaliza watarejea na kusambaza ugaidi  ulimwenguni.  Vyombo kadhaa vya habari Uingereza vimeonya jinsi mamia ya vijana wake wanavyomenyana pia Iraq,  Libya, Afghanmistani, Kenya na Somali  alipo mwanamke wa Kizungu anayetafutwa kuliko fedha.
Samantha, mmoja wa wanae na mumewe gaidi aliyehusika na mauaji ya London 2005. Picha toka gazeti la Mirror

 Samantha Lewthwaite, alikuwa mke wa mmoja wa magaidi wanne waliolipua mabomu na kuua  watu 51 mjini London mwaka 2005. Inadaiwa Septemba 2013, magaidi wa Al Shabaab (walipoua  67 na kujeruhi 175),  Nairobi, Mwingereza huyu mwenye watoto wanne alihusika.  Inadaiwa keshasilimu (anaitwa Sherafiya) na kuolewa na mmoja wa viongozi wakubwa wa Al Shabaab, Hassan Maalim Ibrahim.  Al Shaabab maanake ni “vijana” kwa Kiarabu, ilhali  Boko Haram  ni Elimu ya Kizungu ni Haram.
 Mauaji ya makundi haya  hufanywa  kwa madai eti yanatukuza Uislamu.


 Al Shabaab waliposhambulia duka la Westgate, waliwataka mateka watongoe kanuni za Shahada katika Koran. Aliyeshindwa aliuawa. Shahada husema “La Ilaha il Allah, Muhammad Rasulu-Ilah” ambayo maana yake “Hakuna Mungu mwingine bali Mungu na mtume (au mtumishi) wake ni Muhammad.”
   Kilugha, Shaahada (“yushaahidu”) kwa Kiarabu ni kuangalia au kutazama, yaani “kushuhudia”, kwa Kiswahili.
 Neno jingine lililotumiwa na magaidi karibuni ni “Bakiya” (Baqiya) ambapo Isis (wauaji wa Iraq sasa hivi) iliwataka mateka wao wakiri neno la sivyo kupigwa risasi au jambia shingoni. Bakiya ni “kudumisha jambo” – na Kiswahili tumechukua neno “kubaki” kutokana. Bila kuchimba sana maneno haya, shurti basi tukiri tumekitana vyema na utamaduni wa Kiarabu, kilugha na kidini. 
Kwanza kabisa,  dhana iliyoenea ni kuwa ugaidi ni eti  Uislamu.
 Tuangalie Uingereza, mathalan.
 Miezi mitatu iliyopita  serikali  ilifichua kashfa kubwa mjini Birmingham ambapo shule 12 zilidaiwa kutekwa nyara na Waislamu. Mwanzo wa mwezi huu madai hayo yaliyoitwa “Operation Trojan Horse” yalisema viongozi kadhaa wa Kisilamu walikuwa na njama za kuondoa baadhi ya waalimu wakuu wa shule za Kiingereza na kuingiza wale waliofuata nguzo na kanuni za Kiislamu. Baada ya malumbano na vurugu (ambazo zingali zikiendelea) Waziri Mkuu David Cameron aliamuru (na pia kuandika makala) iliyotaka shule zote Uingereza kufundisha mila na desturi za Kiingereza na si za wageni.
Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya  zimekataza wanawake wa Kiislamu kuvaa Hijab.  Mmoja wa magaidi husika wa London 2005, alitoroka akivalia Hijabu, ingawa baadaye alikamatwa.  Kisheria, kila mtu anatakiwa aonyeshe sura kwa sababu za kiusalama, nk.
Kwa hiyo ugaidi unaoendelea duniani unahusishwa na udini kutokana na maneno na vitendo vinavyosemwa.  Kiini cha mgogoro mzima kimekita ndani ya uchumi na siasa, yaani kutosuluhishwa ukoloni na udhalimu wanaofanyiwa Wapalestina kwa takribani miaka 70 sasa. Toka wakoloni  walipowaondoa Wapalestina na kuwapachika Wayahudi (Israel) katika ardhi yao- mwaka 1947- nchi za Kiarabu zimeathirika.
 Mstari wa mbele ilikuwa Misri iliyovamiwa na majeshi ya Israel mwaka 1967, Syria ikatupiwa makombora  1982, nk.  Tafrani hizi zilizusha kuzaliwa  vyama  vilivyokinzana na Israel kama Hezbollah ya Lebanon. Wapalestina wenyewe wamekuwa na vyama 43 vikiwepo Hamas na Fatah ya PLO(Palestine Liberation Organisation) iliyoundwa mwaka 1965 na hayati Yasser Arafat.
Ugaidi au vita visivyotumia mbinu za kawaida, (yaani askari kupambana uwanjani wakiangaliana) ulijijenga rasmi miaka ya 1970 wakati makundi ya Wapalestina yasiyokubaliana na uongozi wa PLO, yalipoteka nyara ndege za matajiri (Wazungu na Israel) kutangaza kilio chao.  Hali kadhalika Wapalestina  waliingia ndani ya matukio makubwa ya kimataifa kama michezo ya Olimpiki Ujerumani, 1972 wakawateka wanamichezo wa Israel na  kuwaua.
 Utekaji nyara huu uliitambulisha dunia tatizo la ukoloni na udhalimu waliofanyiwa Wapalestina. Wengi duniani walifuata kasumba iliyodai kwamba Wayahudi ni wana wa Mungu na kwamba kutawaliwa kwa Wapalestina ilikuwa haki ya falsafa na siasa  ya Kiyahudi, inayoitwa Zionism.
Mauaji ya Sadat mwaka 1981- moja ya chimbuko muhimu sana la Ugaidi leo...picha ya Mtandaoni....

 Jitihada za   amani kati ya Rais Anwar Sadat wa Misri, Menachem Begin wa Israel na Jimmy Carter wa Marekani zilifanywa mwaka 1978 walipokutana Camp David Marekani. Amani hiyo haikuwafurahisha wote. Oktoba 1981 Rais Sadat alipigwa risasi na  Luteni Khalid Islambouli. Wakati wa kesi Luteni Islambouli alidai sababu ya kumuua Rais Sadat ni yeye kufanya amani na Wayahudi na Wamarekani. Hapo alihamasisha makundi ya Kiislamu yaliyofurahishwa na kifo cha Rais Sadat.
 Mwaka 1982 Tanzania ilikuwa moja ya nchi chache sana duniani zilizowatambua Wapalestina kama watu huru wenye haki ya kujitawala. Serikali yetu ilifungua ubalozi wa Wapalestina na gari la PLO lilipeperusha bendera yao kitaifa.
Miaka ya Themanini ilikuwa muhimu kiharakati. Lakini hali yao haikubadilika; Wapalestina waliendelea kudhalilishwa. Mwaka 1987, harakati mpya zilizoitwa Intifada zilizuka hadi mwaka 1991. Intifada, Kiarabu inaimanisha “kuondoa kwa kujikung’uta” – kama wafanyavyo mbwa au kuku wakati wakinyeshewa mvua.
Ulimwengu ulianza kukiri tatizo na mwaka 1991 mikutano ilifanywa mjini Madrid, Hispania na hatimaye Oslo, Norway, 1993. Makubaliano yaliyofanywa Oslo baina ya Waisrael, PLO na baadhi ya mataifa ya Kizungu yaliweka baadhi ya misingi ya sasa. Moja wapo ni Uongozi wa Kipalestina (Palestinian Authority). Hata baada ya makubaliano ya Oslo, bado Wapalestina waliendelea kunyanyaswa. Mfano ni dai  kwamba Yasser Arafat aliuliwa kwa sumu na Waisraeli.
Makundi mengi yameendelea kuudhishwa na mkondo huu wa mambo.
Miongoni ni bwana Osama Bin Laden. Mwanzoni harakati za Bin Laden zilikuwa dhidi ya Marekani. Aliunda Al Kaeda 1988 na akaanza kuua mwaka 1992 mjini Aden, Yemen. Watu wawili walifariki. Bin Laden na mwasisi mwenzake wa Al Kaeda, Mamdou Salim walitamka “Fatwa” iliyosema  kuua aliyehusika na asiyehusika imo ndani ya Kur’aani.
Marehemu atakwenda “Jannah” penye bustani ya akhera na furaha. Hii imeandikwa katika Sura 56 mstari 12-40 wa Kura'ani.  Ni kama Wakristo wanavyoamini kwenda mbinguni. Ikiwa ulifanya mabaya utakwenda “Jahannam” au kwa shetani. Neno “Jahannam” limetoka  Kiyahudi yaani “bonde la Hinnom”...
Aliyetenda mabaya ataungua moto daima.
Tuendelee kuchimba mada juma lijalo.

-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili...... Juni 22, 2014.







            

No comments:

Post a Comment