Monday 17 March 2014

VITAMBULISHO TANZANIA NA HOJA YA UGHAIBUNI...

Baadhi ya wananchi karibuni wamelalamikia suala jipya la vitambulisho. Wanadai linakera; eti  watu wameuawa. Kuna upendeleo. Ugumu, nk.
Kabla ya kusafiri ughaibuni miaka thelathini iliyopita  wakati wanamgambo walipokuwa wakisimamisha simamisha wazalendo mimi vile vile  nililiona suala la vitambulisho  ni unyanyasaji wa serikali. Ila baada ya kutembea na kuishi nchi nyingi duniani nimegundua  vitambulisho ni jambo la kawaida. Tofauti ipo namna vinavyoulizwa au vipi sera hii inavyotekelezwa na vyombo husika.
Tunavyojua suala la vitambulisho liliasisiwa Tanzania mwaka 1968 kwa sababu za kiusalama baina ya nchi jirani marafiki- Afrika Mashariki na Kati. Baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika (kutokana na sababu mbalimbali mojawapo kufariki Rais Jomo Kenyatta wa Kenya, 1978 na serikali dhalili ya Jemadari Idi Amin wa Uganda iliyoangushwa 1979), sera ilifyata. Hadi leo suala hili  limekuwa likifufuka fufuka na kutoweka, bila kujikita na kukaa kitako muda mrefu kama ilivyo mataifa mengine. Ndiyo maana leo  ni jambo geni na kero kwa raia, hasa vijana.
Idi Amin na Jomo Kenyatta -  miaka ya Sabini. Picha ya Kwekudee Blog

Mamlaka ya vitambulisho Tanzania(NIDA)- imeorodhesha vipengele kumi na moja vinavyoelezea faida zake kuu. Ndani ya orodha –  kipengele cha saba kinaahidi vitambulisho “vitafanikisha kuhakikisha kuwa mtu anapata stahili zake za jamii. Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia Tanzania anastahili.”
Kimtazamo ni ahadi nzuri na muhimu. Naomba nichangie namna mambo yanavyokuwa huku Ughaibuni. 




Kwanza, kila mwananchi hufahamika kazaliwa lini,  wapi, anaishi na kufanya kazi gani, nk. Unapohitaji huduma yeyote lazima uwe na anuani kamili ya unapoishi. Kama huna huipati. Huwezi ukaishi kiholela bila anuani.  Mawasiliano au barua zozote huletwa nyumbani kwako. Kinyume na kwetu Tanzania ambako hakuna mpangilio kamili wa anuani za kila mtu, nchi zilizoendelea huorodhesha anuani zote; hakuna kujificha. Kwetu tunapoandikiwa barua hubidi kwenda posta kufungua kasha, au kazini ulikoajiriwa.  Serikali ya Tanzania ina ugumu kumjua kila raia yuko wapi. Matokeo maskini wengi wasiojulikana na serikali huishi tu bora twende, wakitegemea kudra ya Mwenyezi Mungu na bahati nasibu...
Huku Uzunguni suala la kujulikana unakoishi,  hufuatana na suala la “kutawaliwa na kulindwa” vile vile. Tatizo linapotokea, mathalani, ajali ndani, au hata uzoaji takataka (wa kila juma )- huwa rahisi kufakinikishwa na vyombo husika. Utamaduni huu unaendana na hulka ya uhuru na demokrasia. Je, sisi tunayo?
Kipengele cha tano cha faida iliyoahidiwa na NIDA ni uhalifu na usalama.  Ulimwengu leo umekithiri ugaidi na ujambazi hasa wa dawa za kulevya. Afrika imeshageuzwa “uwanja wa fujo” wa magaidi wanaotumia dini na ujambazi wa dawa za kulevya...
Ni rahisi kuzuia uhalifu ikiwa kila habari za mwananchi zipo ndani ya mfuko wa ulinzi (“data base”). Kama ilivyotokea ndege ya Malaysia  juma hili. Uchunguzi umefanywa haraka kutokana na vyombo vya usalama vya kimataifa  (Interpol) kusaidiana kupeana habari za pasi zilizoibiwa nk.
Sisi hohe hahe lakini tunapoambiwa vitambulisho vitazuia uhalifu, tayari tunafikiria kero tu ya serikali.

Mgambo akipambana na mmachinga Tanzania ya leo.
 Picha ihsani ya Gazeti la This Day   

Nakumbuka mwaka 1981 nilisimamishwa usiku mmoja, mjini Dar es Salaam. Hali ilikuwa mbaya sana nchini. Bidhaa muhimu hazikupatikana;  walanguzi walikwenda nchi jirani  kusaka vitu (hasa mitumba) vilivyouzwa bei za juu –  msemo uliitwa “mwendo wa kuruka”...
Jioni hiyo nilifuatana na  kijana mwenzangu na dada wawili, mitaa ya Kinondoni tulipopitia baa kadhaa. Kufika Mwananyamala, mgambo walitusimamisha kwa jazba.  Mosi ilikuwa wale dada wazuri wazuri. Pili, tulishauchapa mtindi; tumechangamka. Tatu, tumebeba vifurushi. Mimi nilikuwa na shati nililonunua toka kwa mpigania Uhuru wa Afrika Kusini. Shati zuri la rangi rangi ambalo halikupatikana Bongo.
“Ndugu, simameni!” (Enzi hizo  maneno “bwana au waheshimiwa” hayakutumika).
“Wapi mnakwenda, wapi mmetoka?”
Tukasema tumetoka kazini, tukapitia baa; tunaelekea nyumbani.
“Mmebeba nini, ndugu?”                                                                      
Tukaonyesha mitumba.
“Hizi si nguo za  Mzee Kambarage!” (alivyoitwa Mwalimu).
Mimi nikasema ni mwanahabari, pia ninafanya kazi na wageni, nimepewa zawadi kazini. Ukweli niliajiriwa kama mkalimani Ubalozi wa Misri.
“Wapi kitambulisho chako?”
Bahati mbaya siku hiyo sikukibeba. Hakikuwa tayari.  Vilitakiwa kubadilishwa nembo  baada ya mauaji ya Rais Anwar Sadat. Wamisri walikuwa na Rais mpya wa muda, Hosni Mubarak. Ikawa kasheshe. Malumbano. Simu za mkononi miaka hiyo ni njozi tu za malaika. Huwezi kumweleza mgambo subiri nimpigie bosi simu adhihirishe unalolidai.
“Hizi nguo za magendo ndugu. Si za Kitanzania. Itabidi mziache hapa hapa.”
Baada ya maneno mengi, yakaisha. Maneno hayo yalimalizika kwetu kuwapa wale jamaa “chochote”...Msomaji, zingatia hilo.
Hiyo ndiyo dunia ya vitambulisho miaka thelathini iliyopita, Tanzania.
Sasa, nikupelekeni Brazil, miaka kumi baadaye. Nimetoka kazini usiku (kupiga densi) mjini Rio De Janeiro. Nimempa lifti mmoja wa wachezaji densi wa bendi. Anaishi mtaa wa Tijuca, kaskazi ya jiji. Mbali.  Wakati narejea, nikasimamisha gari kutimiza haja ndogo; ghafla nimezingirwa na taa kali za magari. Bunduki. Kelele. Vitisho.  Yote kwa Kireno.
“Piga magoti! Mikono juu!”                                
  Askari wengine wameingia garini wanalipekua.
Kwa vile nilikuwa na nywele ndefu za Rasta, wale askari waliokuwa wakipiga tarumbeta  wakaniita pale pale “jambazi”  muuza dawa za kulevya.
Nikakataa kata kata; mikono juu. Kwa Marekani Kusini, ni kawaida wananchi kuuawa na askari- popote pale hasa usiku. Hadi leo.  Nikasema mimi mwanamuziki, wathibitishe kwa gitaa langu ndani ya gari.
“Ah wapi, tunakujua wee muuza bangi mkubwa!”
Mi’ mwanamuziki, nikajitetea.
“Wapi kitambulisho?”
Nikasema kiko mfukoni. Naweza kushusha mikono nikitoe? Hawakuniamini. Wakidhani n’tatoa bastola. Mmoja akanisogelea akachopoa pochi. Kakuta pesa na kitambulisho. Huendi kokote Brazil bila kitambulisho.
Lakini kilikuwa kitambulisho maalum cha wageni( “Estrangeiro”).  Anuani ya kitambulisho ilionyesha hakika, naishi mtaa wa wageni.  
Sasa wanataka “kunitoa upepo.” Haraka nikasema jirani na rafiki yangu  ni afande wao mkuu Kanali (fulani). Waliposikia jina, wakagutuka. Tena sana.
Nikawaomba wampigie simu  wamuulize. Simu ikapigwa. Kanali akasema kweli  ananifahamu; isitoshe  anaipenda sana bendi  yetu inayopiga klabu maarufu ya Columbus ufukweni mwa, Copacabana,  Rio De Janeiro.  Unaona visa hivi viwili vilikoanza na vilikoishia?  Kwa wale mgambo Mwananyamala bila “malipo” ingekuwaje? Je, hawa wenye mitutu ya Ibilis? Nisingefahamiana na huyo Kanali mkuu ningekuwa hai leo kweli?





Mwandishi (wa pili kushoto) nikiwa na wanamuziki wenzangu Brazil, mwaka 1993.


Ilitoka Mwananchi Jumapili- 16 Machi, 2014

2 comments: