Saturday, 30 November 2013

MASHUJAA WAWILI WA MFANO WALIOFARIKI MWEZI NOVEMBA…


Tarehe 23 Novemba 1963 wakati namalizia malizia darasa la pili,  tuliambiwa tusiende shule. Jana yake, Rais John F Kennedy wa Marekani alipigwa risasi akiwa ziarani mjini Texas. Nakumbuka Watanganyika (tulivyoitwa miaka hiyo ) tulivyosikitika. Rais Kennedy alipendwa sana. Marekani iliisaidia Tanganyika kwa  misaada na wataalamu wa kujitolea – walioitwa “Peace Corps.” Urafiki huu ulidhihirishwa na mifuko ya sembe na vyakula yenye picha ya mkono wa Mzungu na Mwafrika vimeshikana kirafiki.
Mwalimu Nyerere alipokaribishwa  na Rais John Kennedy na kuhutubia Ikulu ya Marekani- mwaka 1963. Walikuwa marafiki wakubwa. Miezi michache baadaye Rais Kennedy aliuawa.

Baada ya miaka mitano mdogo wake marehem, Robert F Kennedy naye aliuliwa kwa risasi wakati akifanya kampeni za Urais. Wengi walitazamia angekuwa kiongozi bora kama kaka mtu.
Toka walipouawa ndugu hawa, sinema mbalimbali na mandishi yametolewa kuhusu kisa na sababu. Aliyezungumziwa na anayeendelea kuongelewa ni marehem John Kennedy- rais aliyependwa kuzidi wote katika historia ya Marekani.


Mauaji ya Rais Kennedy yamechambuliwa sana. Habari zilizofahamika ni kuwa alipigwa risasi na Lee Harvey Oswald – kijana rafiki wa Warusi kutokana na msimamo wake wa siasa za mkono wa kushoto (ukomunisti). Oswald hata hivyo aliuawa siku mbili baada ya kutiwa hatiani. Aliyemtungua (Jack Ruby), naye alifariki jela – kabla ya kueleza sababu hasa za kitendo hicho. Sinema iliyotolewa na Oliver Stone, mtengezaji maarufu wa mchezo wa “Platoon” (1986) mwaka 1991 ilijaribu kuonyesha kuwa mauaji ya Rais Kennedy yalipangwa na serikali. Sinema inaitwa JFK.
Tathmini hii ingali ikiendelea. Kwa majuma mawili sasa runinga huku Majuu zimeonyesha vipindi vingi vinavyodai kwamba serikali ya Marekani ilihusika na kifo cha Rais Kennedy. Kwamba wanausalama walificha ukweli (“cover- up”) kwa kumsingizia Bwana Lee Harvey Oswald.
Sinema ya mwisho niliyoitazama wiki hii inaangalia risasi tatu zilizopigwa mchana ule wa Novemba 22. Ya kwanza iligonga taa ya barabara , ya pili ikamdunga Rais Kennedy shingoni na kutokezea alikokaa Gavana wa Jimbo la Texas (John Connally) –lakini hakufariki.  Ya tatu ilimpiga  tena Rais kichwani na kubomoa ubongo wote.
Dai linaendelea kueleza kuwa risasi ya tatu haikurushwa na Bw Oswald aliyekuwa ghorofani- ilifyatuliwa na mmoja wa wana usalama nyuma ya gari la Rais- ndani ya msafara. Dai na ushahidi vinasema baada ya Rais Kennedy kuingiwa na risasi shingoni – mwanausalama George Hickey- alichomoa bunduki akijitayarisha kujibu mapigo juu ghorofani (alipokuwa Oswald) sasa kwa vile  msafara ulibidi kukitoa mbio- katika mtafaruku na fadhaa mwana usalama Hickey akafyatua bunduki kwa bahati mbaya.
Tunaambiwa wakati maiti ikifanyiwa ukaguzi wa mwisho (“autopsy”), wanausalama hawakutaka habari zifahamike. Walificha picha za mganga za kichwa cha marehemu Rais. Kawaida mtu akipigwa risasi jeraha huonyesha ni risasi au bunduki gani. Wajihi wa hayati Kennedy ulithibitisha jeraha la kichwa na shingo vilipigwa na bunduki tofauti.
Sasa kuna hayo.
La pili ni ushujaa wake Rais John Kennedy. Alizaliwa mwaka 1917 katika familia ya watoto tisa na baba, Joseph Kennedy, alipenda siasa na utawala. Toka akiwa mdogo John aliugua ovyo- ila alikua shupavu, kitabia. Aliingia jeshi la majini la Marekani, akiwa kiongozi wa boti za kivita mwaka 1943 hadi 1945. Boti lao liliposhambuliwa vikali na Wajapani, Kennedy - aliyekuwa na cheo cha Luteni- alijitahidi kuwaokoa waliokuwa chini yake kwa muda mrefu jambo lililomfanya abugie maji chumvi na mafuta ya petroli ya meli hiyo ndogo. Kutokana na hali hii alisumbuliwa na matatizo ya tumbo- maisha yake yote.  Mwaka 1943 alipewa nishani mbili  za kishujaa. Kuanzia 1946  aliwakilisha jimbo lake la Massachusetts, bungeni. Mwaka 1955 alipewa tuzo mashuhuri ya Pullitzer (inayotolewa kwa wapiga picha, waandishi na wanahabari) alipochapisha kitabu cha  maisha ya Wabunge wanane wa Kimarekani waliopigania fikra zao bila kutetereka.
Baadaye  1961 alishinda uchaguzi wa Rais kwa kura zaidi ya mpinzani wa chama cha Republican Bw. Richard Nixon. Rais Kennedy amejulikana zaidi kwa mauaji yale ya Novemba 22 na mahusiano yake na akina mama – alikuwa mwingi wa wanawake. Kinachosahaulika ni ushujaa wake vitani, namna alivyozuia vita vya dunia mwaka 1962 na kuidhinisha muswaada wa kuwapa haki watu weusi wa Marekani, kipindi kifupi kabla ya kuuawa.
Moja ya sifa kuu ya kisiasa anayokumbukwa ni uzalendo na ukweli. Kinyume na wanasiasa wengi (duniani) hakutoa ahadi nyingi  kwa wananchi kabla na baada ya kuteuliwa kiongozi. Kennedy : “Usiulize nchi yako itakusaidiaje. Uliza nini unaweza kuchangia kwa nchi yako.”
Mwingine wa kukumbukwa aliyefariki mjini London, Jumapili iliyopita- ni mwandishi wa Kiingereza Doris Lessing. Bi Lessing aliyezaliwa mwaka 1919, alichapisha vitabu zaidi ya hamsini vya riwaya, michezo ya kuigiza, hadithi fupi na makala . Mada zake kuu zilitetea haki za binadamu, udhalimu na ubaguzi wa Waafrika – (aliwahi kuishi Zimbabwe) na haki za wanawake.
Kwanini safu inamzungumzia Doris Lessing?
Doris Lessing - akionyesha tuzo aliyopewa mwaka 2011.
Picha ya gazeti la Guardian - Uingereza

Ujuzi wa lugha Tanzania wazidi kudidimia. Leo vijana wengi – hata walio masomo ya juu chuo kikuu hawawezi kuandika au kusema Kiingereza fasaha. Wapo wanaojifaragua kwa kuchanganya hiki “Ki-Swanglishi” lakini wanajidanganya tu. Usipopika chakula kikaiva ya nini kukiwekea eti binzari, pilipili na iliki kiliike?
Moja ya njia kuu za kuboresha lugha ni kusoma. Tukiwa sekondari zamani tulishindana kusoma riwaya (mathalan James Hadley Chase na Faraji Katalambula) Kiingereza na Kiswahili. Je, vijana wangapi wanatembea na riwaya mifukoni leo? Maandishi ya Doris Lessing yameandikwa kwa usafaha sana. Hadithi  alizotungia Afrika- mathalan “Grass is Singing”, “A Man and Two Women”,  “A Proper Marriage” na “African Stories”- zina maelezo murua ya mazingira, ushairi na mandhari ya bara hili. Ingawa ni Mzungu tungo zake zina mapenzi kwa anachokielezea. Alikua mpinzani mkubwa wa ubaguzi wa rangi Zimbabwe na Afrika Kusini. Fasihi yake pia inawatetea wanawake na wanaume wanaoteseka katika mahusiano ya ndoa, mapenzi au kazi. Si ajabu alishinda tuzo mbalimbali ikiwemo –Nobel Prize- ya 2007.
Ukimsoma utaitajirisha lugha yako.
Sababu nyingine ya kuelezea habari zake ni kukukutaka msomaji uwajue waandishi wazuri, duniani. Doris Lessing alikula chumvi nyingi. Alifariki akiwa na miaka 94. Alizaliwa Uajemi (Iran) akaishi Zimbabwe na Uingereza. Ni mwandishi muhimu sana kumjua na kumsoma; sidhani atakosekana maktaba za Kiingereza, Afrika Mashariki.


Ilitoka pia -Mwananchi - KALAMU TOKA LONDON

No comments:

Post a Comment