Tuesday 4 October 2011

JE, KWANINI OMBI LA WAPALESTINA KUJIUNGA NA UMOJA WA MATAIFA NI MUHIMU KWETU SOTE?

Wiki iliyopita kiongozi wa Wapalestina, Mahmoud Abbas, alipigiwa makofi alipotoa hotuba ya dakika 35 kuutaka Umoja wa Mataifa uwatambue wananchi wake kama taifa huru.
“Wakati umefika, “ alieleza, “kwa wanaume, wanawake na watoto wetu kuwa na maisha ya kawaida. Kulala salama wakijua wataamka bila woga wa nini kitatokea kesho yake asubuhi.” 
Wapo waliompinga; mathalan Hamas, iliyodai kuna njia  bora zaidi kuwasukuma Wayahudi watambue haki za Wapalestina. Hamas ilisema Wapalestina lazima watumie nguvu kujikomboa badala “ya kuupigia magoti” Umoja wa Mataifa.

Mahmoud Abbas akiwa na bango la kiongozi maarufu wa Wapalestina Yasser Arafat....

Mrengo huo wa mawazo  unathibitishwa na Wamarekani walioshasema dhahiri kwamba watatumia kura ya “veto” ndani ya Baraza la Usalama kuzuia Wapalestina kuwa taifa huru. Kihistoria kura ya “veto” ilishatumika miaka ya nyuma kuyatia kabali masuala mbali mbali ya kimataifa. Iko mikononi mwa mataifa matano: Marekani, Uingereza, Urusi, Ufaransa na China.
<--more--!>
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliundwa mwaka 1946 likawa na kikao chake cha kwanza mjini London baada ya vita vikuu vya pili vya dunia. Baraza hilo lenye nchi 15 liliasisiwa kuhakikisha amani inakuwepo ulimwenguni. Hatua ya kuunda Baraza La Usalama ilifuatia hatima ya vita vya 1939-45 baada ya Wazungu kujiuliza vipi Mjerumani alimshambulia kila mtu bila mataifa kumudu kuungana. Awali lilikuwepo Shirikisho la Kimataifa (League of Nations) lililoundwa baada ya vita vikuu vya kwanza.
Baraza la Usalama liliundwa kurekebisha matatizo haya hasimu yaliyoua mamilioni  ya watu wakiwemo Wayahudi milioni 6.
“Veto” ni neno la Kirumi lenye maana “kuzuia.” Miaka ya mwanzo ya Umoja huu, Urusi ilitumia veto kuzuia suala lolote lililokinzana na masilahi yao mintaarafu nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Warusi (leo Ulaya Mashariki). Hatimaye hata hivyo zilijikomboa baada ya ukuta wa Berlin kuangushwa mwaka 1989. Ahueni hii ilifanikiwa kutokana na siasa za kimaendeleo za Rais Mikhail Gorbachev aliyeitaka serikali yake iondoe vizuizi vya kirasimu, demokrasia, nk. Itikadi ya Gorbachev iliitwa “Perestroika” na ingawa alipingwa vikali; iliteta mabadiliko muhimu duniani. Mojawapo ni kusambaa kwa mkondo wa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa ulimwenguni na Afrika (ikiwepo Tanzania)  baada ya 1990.
Wafaransa nao walitumia kura ya veto kupinga azimio la Umoja wa Mataifa kukubali uhuru wa visiwa vya Ngazija (Comoro) mwaka 1976. Wakati serikali ya wahaini (kama ilivyoitwa mwaka 1965 hadi 1980) wa Rhodesia ikijaribu kutaka kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, Uingereza ilipiga kura saba za veto. Rhodesia ilitokana na Cecil Rhodes mlowezi aliyeongoza maslahi ya wakoloni na wakulima wa Kiingereza na kutwaa Muungano wa Rhodesia ya Kaskazini (Zambia), Nyasaland (Malawi) na Rhodesia Kusini (Zimbabwe) karne ya 19.
Waafrika wakiongozwa na vyama vya Zanu ( Robert Mugabe) na Zapu (cha marehem Joshua Nkomo) walipambana na walowezi hawa (chini ya Ian Smith) hadi Uhuru ulipopatikana 1980 na Rhodesia ikabatizwa jina la kijadi la nchi hiyo yaani Zimbabwe.
Miaka ya karibuni Marekani imetumia veto kupinga azimio lolote lililoisakama Israel, mgomvi mkuu wa Wapalestina.
Mwaka 2002, aliyekuwa balozi wa Marekani, Umoja wa Mataifa, John Negroponte alidai Marekani itaendelea kupinga azimio kwa sababu kuu nne. Kwanza kushutumu ugaidi na uchochezi wowote wa magaidi, pili, shutuma ya vikundi vya Hamas, Islamic Jihadi na Al- Aqsa Matyrs Brigade; tatu, suluhisho la vyama vyote husika kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa kutatua mzozo na nne, majeshi ya Wayahudi kutoondoka nyumbani kwa Wapalestina bila kuwepo usalama baada ya mapigano ya Intifada mwaka 2000.
Madai ya balozi huyu (yaliyoitwa “Kanuni za Negroponte”) yametumiwa kila suala la Wapalestina lilipotajwa Umoja wa Mataifa.
Hivyo basi, baada ya Bwana Abbas kutoa hotuba yake alibishiwa vikali. Wayahudi walisema haiwezekani Wapalestina wakaruhusiwa kuwa ndani ya umoja huo bila mazungumzo kuendelea.
Kiongozi wa Israel, Benjamin Netanyahu aliijibu hoja ya Abbas kwamba kuliingiza taifa la Wapalestina ndani ya Umoja huo bila kuwepo makubaliano kutaendelea kuzua ugomvi.
Aliungwa mkono na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair. Ingekuwa ni mtu mwingine anaongea labda watu wangemsikiliza. Blair haheshimiwi sana kutokana na msimamo wake kuchangia mavamizi ambayo hayakuruhusiwa ( na Umoja wa Mataifa) Iraq akishiririkiana na George Bush mwaka 2003.
Mkwaruzano wa Wapalestina na Israel ni muhimu sana kwa ulimwengu  wetu. Hatuwezi kumalizia kuelezea misingi ya tatizo hili katika makala fupi kama hii. Hata hivyo la kuzingatia ni kwamba mzozo huu ulianzishwa na hawa hawa wakubwa.
Wapalestina wamekuwa kiamani toka walipoanza kutawaliwa na Waturuki chini ya Walii wao, Muhamad Ali, mwaka 1832; kisha wakawa chini ya Waingereza hadi mwisho wa vita vikuu vya kwanza lilipotishwa azimio la Balfour, 1917. Kuanzia hapo ikawa Waingereza wanaendesha shughuli za wananchi hawa wakitaka  nchi yao igawanywe na Wayahudi. Wakapachika serikali ya Israel katika ardhi ya Wapalestina mwaka 1948 baada ya vita vikuu vya pili.  
Mgogoro uliendelea hadi 1965 Yasser Arafat alipounda PLO iliyokuwa na mkono wa vita (Fatah ) ikisaidiana na vyama vingine kama PFLP cha Dk. George Habash. Miaka ya 1970  vikundi vingi vya Wapalestina viliamka kupigana vikitumia utekaji nyara ndege. Mojawapo ilikuwa Black September. Vita vya Wapalestina vilihusisha pia nchi za Kiarabu mfano Jordan, Misri na Syria; shauri wapiganaji wa Kipalestina ama waliishi huko au walipewa mafunzo. Kutokana na kutofumbuliwa mgogoro, matatizo ya Mashariki ya Kati yamezua milango mingi. Baadhi ya Waarabu waliowasaidia Wapalestina pia walisambaza janga mathalan Muammar Gaddafi; wafanya biashara wa Saudi Aarabia waliopandisha bei za mafuta kuzisukuma nchi tajiri ama wa Lebanon kupitia vyama kama Hezbolah. Kila tatizo lililotokea Mashariki ya Kati ndani ya kipindi cha takriban miaka 50 iliyopita kimetokana na Wapalestina. Hatima yake ni mzozo kuhusisha fikra za watu waliokuwa na msimamo mkali zaidi kama  Osama Bin Laden na Al Kaida. Sasa basi ikiwa mzozo huu hautatuliwi; matatizo ya ugaidi, vikundi vichache vya Kiislamu vinavyopingana na siasa za nchi za Magharibi haviwezi kumalizika. Leo tunawaona magaidi kama watu waliochipushwa na Al Kaida; walakin  ukichunguza kwa undani chimbuko lake ni mgogoro wa Wapalestina na Wayahudi. Bila kulitatua, amani haitopatikana duniani.
 



http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/15966-kwa-nini-ni-muhimu-parestina-kujiuna-un
Chapishwa pia  Mwananch i(makosa ya kichwa cha habari):

No comments:

Post a Comment