Sunday, 2 January 2011

MAAZIMIO YAKO 2011 YAWE KUJIENDELEZA KIFIKRA...

Kabla ya kuendelea na mada ya mazoezi tuliyoiongelea Jumapili iliyopita tuutazame mwaka mpya 2011, kijasiri. Msomaji huenda hufurahishwi na hali ya uchumi, wanasiasa wanaotuongopea na maisha yanayoendelea kuwa  magumu.
Hisia hii imeenea ulimwenguni. Imekithiri kiasi ambacho kuna fikra mwisho wa dunia unakuja. Wapo wanaoeneza falsafa kwamba mtabiri wa zamani Nicodemus aliambiwa na Yesu Kristo kuwa dunia itakwisha 2012. Mfano mzuri ni blogu la “2012 Doomsday Prophecies” (Tabiri za Siku ya Kiama 2012) linalonukuu Biblia (Yohanna Sura ya 3:8) na hali ya mafuriko, matufani na matetemeko makubwa miaka hii (Haiti, 2010) kama ishara ya angamio hilo.
<!--more-->
 Bila shaka msomaji umesikia namna msimu wa barafu ulivyokuwa mkali Ulaya na Marekani. Usafiri umeathiriwa, watu 60 walifariki mwezi Desemba nchini Ujerumani, Urusi, Ubeljiji na Poland. Viwanja vya ndege vimedhurika na safari kuvunjwa.
Blogu la “Doomsday” linapiga makofi kusifia ukweli wa tabiri zake Nicodemus. “Doomsday” linatukuza kalenda ya Maya inayosisitiza mwisho wa ulimwengu na mwanzo mpya...
Barani Afrika, leo, imani kuwa uhai umelaaniwa zimeshika hatamu. Kutokana na maafa ya vita, magonjwa ya UKIMWI na malaria, Waafrika wengi waliodhalilishwa na viongozi waongo wanaowaibia na kuwadanganya kila siku wamekimbilia dini. Imani zetu za jadi ambapo mababu na mabibi zetu walitambikiwa na kuaminiwa  zimetupwa shimoni. Badala yake wengi tuko tayari kupigana hadi kufa kutetea dini zilizoletwa na wageni miaka michache tu iliyopita. Dini hizi zinazotukuza upendo, amani na Mungu kuwa suluhisho zimekuwa ndiyo ahueni ya mawazo na hisia. Kimsingi wanadamu dunia nzima tunaupokea mwaka 2011 kwa utata.
Je, ni kweli mwisho wa dunia utakuwa 2012?
Mwezi ujao natimiza miaka 56. Toka nikiwa mtoto nimezisikia hadithi hizi za mwisho wa dunia. Mwaka 1962 nikiwa darasa la kwanza hofu iliyoenea ilikuwa bomu la Atomiki na vita vikuu vya tatu vitakavyotokea kutokana na uhasama baina ya Wamarekani na Warusi. Uhasama uliota kichuguu wakati Rais Fidel Castro wa Cuba na makamu wake Che Guevara walipoamua kumwambia Mmarekani afilie mbali, asiendelee kuonea mataifa na watu maskini. Mgogoro wa Cuba na Marekani, 1962, uliitisha dunia nzima. Na haukuwa wa kwanza miaka ya Sitini. Uliendelea Vietnam, Kongo na hata Zanzibar. Kila mahali wanadamu walipojaribu kudai haki zao toka ukoloni na hali ngumu kiuchumi walitishwa na tembo wawili yaani Urusi na Marekani.
 Kipindi chote nilichosoma shule ya msingi hadi naingia sekondari 1969 kilikuwa cha hofu ya bomu la Atomiki; kwamba dunia italipuka dakika yeyote. Tukiwa watoto habari hizi zilichanganya migogoro ya kivita Vietnam, mauaji ya viongozi mashuhuri  Rais John Kennedy wa Marekani (1963), Malcolm X (1964), Martin Luther King (1968) na Waziri Tom Mboya wa Kenya aliyepigwa risasi mjini Nairobi, 1969.
Miaka ya Sabini ilizidi kuchubua.
 Kila mahali wanadamu walidai haki zao, wakipingana na tawala zilizowatesa. Hapa Bongo migomo ilitokea viwandani, mashuleni na moja ya mambo makubwa  ni kuuawa kwa  Rais wa kwanza Zanzibar, Abeid Amani Karume, mwaka 1972. Bara zima la Afrika lilichachamaa  na wapigania Uhuru, Angola, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, nk. Nchi zilipinduliwa  na lililotuathiri zaidi Wanabongo ilikuwa Jemadari Idi Amin Dada aliyemtoa Rais Milton Obote madarakani  Uganda, mwaka 1971.
 Kilichonguruma zaidi ni Wapalestina. Wanaharakati waliteka nyara ndege wakidai kutambuliwa; huku nyuma nchi tajiri za Kiarabu zilizotoa petroli zikipandisha bei mafuta hayo kuwakamua matajiri wa Ulaya na Marekani walioisaidia Israeli dhidi ya Wapalestina. Hapa ndipo mgogoro uliopo leo Mashariki ya Kati na Afghanistani ulipoanzia. Ndege zilitekwa nyara na tatizo la Wapalestina likajulikana. Wakati haya yakiendelea  hali ya uchumi iliharibika kiasi ambacho nchi tajiri zilipunguza kabisa bei za mazao toka nchi changa. Uchumi mgumu tulionao leo ulikuwa pia taswira ya miaka ya Sabini. Kiama kilizungumziwa. Fasihi na sanaa vilijitahidi kuliwaza. Mwanareggae Bob Marley, toka Jamaika, aliimba kuhimiza mapenzi, amani na harakati.
Miaka ya Themanini iliangukiwa na UKIMWI. Mwanzoni UKIMWI ulisemekana tu  tatizo la wasenge. Ila mwaka 1987 UKIMWI ulienea hata wasiokuwa firauni. Afrika Mashariki UKIMWI ulikatiwa jina la SLIM kutokana na jinsi ulivyokondesha walioupata. Miaka ya Themanini na Tisini uliwapa Waafrika imani kuwa bara letu limelaaniwa. Laana iliraruka  mwaka 1994 kutokana na mauaji ya Watusi na Wahutu, laki nane, Rwanda.
Kiulimwengu miaka ya Tisini ilikuwa ya mauaji ya jumla jumla. Aprili 1995 mji wa Oklahoma, Marekani, ulistuliwa na gaidi Timothy McVeigh, aliyejeruhi 680, akaua   168, (kati yao watoto 19) na kuharibu majengo 324 kwa mabomu. Ni kipindi hiki kila mtu alipoongelea mwisho wa dunia yaani 1999 kuangukia, 2000. Mwanamuziki  wa Kimarekani, Prince alitunga wimbo uitwao 1999.
 Ugaidi na mabomu ya Waarabu walioudhiwa na siasa za Magharibi kuhusiana na Wapalestina wakiongozwa na Al Kaida ya Osama Bin Laden yalisambaa kuanzia Dar es Salaam (1998) hadi New York, Septemba 2001.
Kifupi hakuna kipindi chochote nilichoishi ambapo hapakuwepo  fikra kwamba mwisho unakuja. Ukishunguza historia yetu wanadamu kila kipindi  kimekuwa na vita au machafuko ya mazingira.
Msomaji zingatia kwamba masha yetu ni mseto wa mabadiliko, mvutano wa maumbile, mabaya na mazuri, moto na baridi, jike na dume, matajiri na maskini, wenye uwezo na wasio uwezo.
Je, utamuduje?
Mwaka 2008 nilimhoji mwanasaikolojia wa Kiingereza, Dk. John Conolly, pia mganga wa wenda wazimu. Alisema wagonjwa wa vichaa wanaongezeka duniani kutokana na baadhi yetu kushindwa kuyaelewa maisha ili kuyamudu. Alishauri kila mtu kujiuliza maswali akiamka au akienda kulala.
Unapoamka jiulize je, leo nitafanya jambo gani kujiendeleza kitaaluma?  Je, nitafurahishaje nafsi yangu? Na kama sina raha nitachukua hatua gani kukabili na kutawala mazingira na maisha yangu badala  ya kuyahofia?
Je Watanzania wangapi wanaazimia kununua kitabu mwaka huu kujisomea? Idara ya Elimu ya Umoja wa Mataifa mwaka jana ilikiri kwamba watoto 72 milioni duniani hawasomi;  na kwamba elimu ni tatizo mosi la jamii maskini ulimwenguni.
 Fidel Castro wa Cuba anasema katika kitabu cha maisha yake kuwa tumeumbwa kuuendeleza ulimwengu wetu. Tuko hapa tuwazae wanadamu wengine watakaochangia uhai.  Hivyo basi, mwaka 2011 uwe wako kujiendeleza, ndugu msomaji.

 -London, Jumanne, 28 Desemba,  2010.


Ilichapishwa gazeti la Mwananchi, Jumapili, Januari 2, 2011.


http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/38-johari/7961-maazimio-yako-mwaka-2011-yawe-ya-kujiendeleza-kifikra


No comments:

Post a Comment