Kusoma na kutukuza fasihi ya Kiswahili Fasaha kupitia vitabu na sinema ndiyo njia pekee itakayoendeleza na kuimarisha lugha yetu...
Wiki jana tuliangalia namna
ambavyo Kiswahili kimekua, kikazoa na kuburuta misamiati ya lugha za Kiarabu, Kiingereza, Kiajemi, Kireno,
Kihindi nk. Hapo hapo kanuni zake za kisarufi (“grammar”) ni za Kibantu. Ina
maana Kiswahili ni lugha ya Kiafrika, inayojitosheleza.
Kukua kwa “Kiswanglish” si
jambo baya. Tatizo hili si geni barani Afrika.Wala si geni ndani ya baadhi lugha
mbalimbali ulimwenguni. Waspanyola wakazi wa Marekani wameunda “Spanglish”-
lugha ya mitaani inayotumiwa na walowezi
waliozaliwa kule walio baina ya utamaduni wa Kimarekani na Kilatina. Tofauti ni
kwamba Walatina huwalea wanao kufuata mila zao. Si kama Waafrika wengi
wanaokulia Majuu- hawasisitizi wanao huku Uzunguni kuzijua mila na lugha zao.
Wanaona nishai na aibu... kwamba lazima wafanane na wenyeji.
Amina Waziri ...mjukuu wa Shaaban Robert ambaye ni mmoja wa waalimu wakubwa wa Kiswahili Ughaibuni akiongea nami mwaka 2008 kuhusu haja ya kutukuza kumbukumbu ya babu yake na kuendeleza lugha hii muhimu. Picha na F Macha
Wiki jana tuliangalia namna
Kenya ilivyoanza lugha ya Shenge, miaka 20 iliyopita. Lugha hii ilichanua
kutokana na baadhi ya Wakenya-hasa mjini Nairobi- ambao ni wazungumzaji wazuri
wa Kiingereza kuwa dhaifu katika msamiati wa Kiswahili na kuamua kuchanganya
changanya. Lakini haina maana walikua duni lugha ya Kiingereza. Sisi tunaingiza
Kiingereza katika Kiswahili- lakini tunasutwa (hasa na majirani wetu wa Kenya
na Uganda) tulivyo wabovu kwa Kiingereza. Kabla ya kuendelea – hebu tuangalie
nchi nyingine ya Kiafrika zenye mtindo wa kupikicha pikicha lugha kama Kenya.