Enzi hizo hatukua na UKIMWI.
Magonjwa ya zinaa hayakuua mtu. Dalili yake ilikuwa
kuwashwa na kujisikia vibaya wakati wa kwenda haja ndogo tu, basi. Yakikuzidia
unazunguka zunguka mitaani unanunua dawa rangi ya chungwa na manjano- kidonge cha
“tetracylene”- aghali ndiyo; lakini kinamaliza kabisa tatizo.
Baadaye miaka ya Themanini UKIMWI ukatangaza ufalme.
UKIMWI haukuponywa kwa kidonge kama hicho.
Na hata baada ya
miaka thelathini, UKIMWI uliposhaanza kutibika- ( nchi zilizoendelea), haikua
kidonge kimoja. Vingi. Tena bei yake si
ya porojo. Sijasikia mtu anayeweza kuingia tu sehemu akanunua msururu wa
vidonge vya kutibu UKIMWI. Tiba hii ilihimili lakini haijaondoa kirusi, abadan.
Kawaida kirusi cha
UKIMWI huwa kinamshinda mwanadamu kwa vile hushambulia mfumo mzima wa “kinga
maradhi” mwilini. Ingekua kirusi hiki hushambulia
tu ingetosha kuzuilika kama ambavyo virusi vingine huzuilika- kule kubadilika badilika kwake ndiyo kiini
cha zogo. Ndiyo maana Waswahili (tulivyo
wabunifu) tukaukatia ugonjwa majina kama “ngoma”, “bomu” “mdudu,” nk.
Watafiti lakini hawajalala. Karibuni wametangaza kuanza kuelewa namna kirusi
cha UKIMWI kinavyotekeleza ufisi wake. Waganga hao Dk Barton Haynes na John
Mascola walifanya majaribio kwa mgonjwa
wa UKIMWI toka Afrika na kuchora ramani (“mapping”) ya mwenendo mzima.
Hatimaye, tiba iko karibu ndivyo jarida la VR-Zone.Com la Marekani lilivyotangaza kwa hamasa juma
lililopita.
Hoja niliyoieleza hapa inaonyesha namna matangazo ya tiba
za magonjwa mbalimbali zinazowasakama wanadamu yalivyo muhimu.
Vijana wa shule ya sekondari ya Mwandege, mkoa wa Pwani mwaka 2009. Taifa la kesho. Baadhi yao watakuja kuwa wataalamu wetu. Picha na F Macha
Vijana wa shule ya sekondari ya Mwandege, mkoa wa Pwani mwaka 2009. Taifa la kesho. Baadhi yao watakuja kuwa wataalamu wetu. Picha na F Macha
Mbali na UKIMWI
yapo maradhi yenye virusi vikali (yanayoendelea kutusakama wanadamu) mathalan-
Malaria, Saratani na Kifua Kikuu kilichoanza kurejea karibuni...
Tatizo haliko katika haya maradhi bali katika “sugu”
ambayo virusi vimejenga. Sikilizeni kisa kifupi.
Takriban miaka 15 iliyopita nilipohamia hapa Uingereza
niliwahi kwenda zahanati ndogo ya kitongoji ninachoishi shauri ya mafua makali.
Kawaida mafua ni ugonjwa katili sana jamii hizi za nchi baridi – huja majira
yanapobadilika mwezi Mei ( toka msimu wa
baridi kuingia joto) na Novemba ( joto kuisha na kipupwe kuanza). Kufika kwa
mganga akanipima presha, moyo, pumzi nk akasema niko sawa kabisa.
“Lakini daktari silali, usiku kucha napiga chafya.”
Akaniangalia kwa macho yenye mseto wa huruma na cheko.
“Sikiliza. Wewe mzima kabisa bwa’ mkubwa; moyo na mwili
wako viko shwari shauri unafanya mazoezi,
unajiangalia; huvuti sigara, unajali unachokula, afya yako kama ya kijana wa
miaka 20 (nilikua na miaka arobaini). Nenda zako tu nyumbani kapumzike. Usitoke
toke; kunywa maji kwa wingi, lala kwa muda mrefu. Utapona tu.”
Duu, nikamwona mganga yule (ambaye aliwahi pia kufanya
kazi Tanzania) kama ana mipango mibaya nami.
“Naomba unipe dawa kali daktari. Siwezi nikakaa nyumbani
na mafua, bila dawa yeyote. Unajua mafua yanaua hapa kwenu Ulaya?”
Akacheka.
“Nimeifanya kazi hii karibu miaka 30. Usipende sana
kunywa kunywa dawa. Nenda zako tu nyumbani kapumzike. Baada ya siku tatu ukiona
hali mbaya rudi tena nitakupa hiyo dawa kali unayoitaka.”
Roho iliudhika sana. Nikaenda zangu nyumbani kichwa
upande. Usiku nilitokwa jasho, koo liliniwasha, (tunaweza kufananisha mafua ya Kizungu
na Malaria) nikalala tu. Kama
alivyoshauri nikawa nakunywa maji kwa
wingi. Na kweli baada ya siku tatu ahueni, hiyo. Siku tano kujiri, nikapona.
Sasa fundisho nini?
Waganga wa Kizungu siku hizi hawatoi kiua vijasumu - Kiingereza “anti-biotics” -kama ile niliyoongelea
mwanzoni, yaani Tetracyclene, ovyo. Kuna
wimbi lililozuka na kuenea kwamba kutumia sana dawa kali kutibu kila aina ya
maradhi yanayotukabili kumejenga “sugu” kati ya mamia ya virusi pilipili vinavyotushambulia.
Mwezi uliopita Mganga Mkuu wa Uingereza Profesa Sally
Davies alihojiwa na runinga ya SKY
akasema virusi vingi vimekua sugu hivyo tuna hatari ya kukosa tiba ya maradhi
na kurejea hali mbaya na ya kizamani karne
ya 19. Mganga mkuu huyu aliyehitimu mwaka 1972 alilinganisha hatari hii na ugaidi wa kidini unaoukabili
ulimwengu wetu sasa hivi.
Tatizo la msingi akadai, ni biashara. Makampuni makubwa makubwa
yanayowekezea utafiti wa dawa za kukinga maradhi (kama UKIMWI mathalan) “hayatengenezi
fedha” kuvumbua dawa mpya. Toka mwaka 1987 hapajagunduliwa hata dawa moja mpya. Makampuni
makubwa yanaona bora tu kuuza dawa zile zile kwa wateja wanaoendelea kuugua na
hatimaye kufa maana haiathiri biashara.
“Unapoweka dawa
mpya katika madawati ya maduka wahitaji kwanza wateja wachukue muda kuzizoea; si
rahisi kuuza.” Alidai.
Katika miaka mitano iliyopita virusi vikali kama E-Coli
(anayekaa katika nyama mbichi kutokea
kinyesi mithili michango na tegu) vimekua kwa asilimia 60 ilhali kifua kikuu kimerejea kwa kasi. Miaka
sitini iliyopita kifua kikuu kilikua na ushetani huo huo wa UKIMWI ulivyo leo.
Wiki jana niliongea na mganga mstaafu ( wa kigeni) Tanzania
-hakupenda kutangazwa jina. Alisema leo asilimia 80 ya watoto kwetu wanapewa
dawa kali kwa maradhi madogo madogo. “Kinachotakiwa ni kama asilimia 20 tu;
asilimia 80 ni nyingi sana.”
Akasema sisi Wabongo tumeshazoea kwamba kila ugonjwa
lazima uandikiwe kiua sumu (anti-biotics)- zahanatini. Utoaji huu wa dawa ni
mbinu tu kutajirisha wafanyabiashara wanaouza dawa na hujenga sugu
ya maradhi.
Utafiti uliofanywa mwaka 2010 hadi 2011 na waganga hospitali
ya KCMC , Moshi wakiongozwa na Judith
Gwimile ulithibitisha watoto wadogo wamekua wakipewa viua sumu kwa magonjwa
ya kuhara na kukohoa. Utafiti huo uliochapishwa jarida la “Pan African Medical Journal” Agosti
mwaka jana, unathibitisha dhana iliyopitwa na wakati. Kutoa dawa hizi kali kwa
maradhi yasiyo na virusi vikali sana hujenga mazoea na “sugu” katika miili ya wahusika
kiasi ambacho wakiugua baadaye si rahisi kupona. Tabia hii imepingwa na kutajwa
pia na shirika la Afya duniani WHO na wataalamu mbalimbali nchi zilizoendelea. Lengo
lake ni kutengeneza tu fedha juu ya migongo ya walala hoi wanaohadaiwa kuwa
kila ugonjwa unahitaji dawa kali.
Mwandishi wa mambo ya maradhi, Doug Kaufmann kaandika
karibuni mtandaoni kuwa viua sumu huteketeza vile virusi rafiki vinavyopambana na virusi vibaya tumboni.
“Nafasi yake huchukuliwa na kuvu au uyoga anayedhoofisha kinga maradhi na waweza
kusababisha saratani.”
Ilitoka pia Mwananchi Jumapili....
No comments:
Post a Comment