Thursday, 4 April 2013

USONGO WANGU NA KISWANGLISHI : WATANZANIA HATUJAKOMAA KILUGHA-2


Kusoma na kutukuza fasihi  ya Kiswahili Fasaha kupitia vitabu na sinema  ndiyo njia pekee itakayoendeleza na kuimarisha lugha yetu...

Wiki jana tuliangalia namna ambavyo Kiswahili kimekua, kikazoa na kuburuta misamiati  ya lugha za Kiarabu, Kiingereza, Kiajemi, Kireno, Kihindi nk. Hapo hapo kanuni zake za kisarufi (“grammar”) ni za Kibantu. Ina maana Kiswahili ni lugha ya Kiafrika, inayojitosheleza.
Kukua kwa “Kiswanglish” si jambo baya. Tatizo hili si geni barani Afrika.Wala si geni ndani ya baadhi lugha mbalimbali ulimwenguni. Waspanyola wakazi wa Marekani wameunda “Spanglish”- lugha ya mitaani inayotumiwa  na walowezi waliozaliwa kule walio baina ya utamaduni wa Kimarekani na Kilatina. Tofauti ni kwamba Walatina huwalea wanao kufuata mila zao. Si kama Waafrika wengi wanaokulia Majuu- hawasisitizi wanao huku Uzunguni kuzijua mila na lugha zao. Wanaona nishai na aibu... kwamba lazima wafanane na wenyeji.
Amina Waziri ...mjukuu wa Shaaban Robert ambaye ni mmoja wa waalimu wakubwa wa Kiswahili Ughaibuni akiongea nami mwaka 2008 kuhusu haja ya kutukuza kumbukumbu ya babu yake na kuendeleza lugha hii muhimu. Picha na F Macha

Wiki jana tuliangalia namna Kenya ilivyoanza lugha ya Shenge, miaka 20 iliyopita. Lugha hii ilichanua kutokana na baadhi ya Wakenya-hasa mjini Nairobi- ambao ni wazungumzaji wazuri wa Kiingereza kuwa dhaifu katika msamiati wa Kiswahili na kuamua kuchanganya changanya. Lakini haina maana walikua duni lugha ya Kiingereza. Sisi tunaingiza Kiingereza katika Kiswahili- lakini tunasutwa (hasa na majirani wetu wa Kenya na Uganda) tulivyo wabovu kwa Kiingereza. Kabla ya kuendelea – hebu tuangalie nchi nyingine ya Kiafrika zenye mtindo wa kupikicha pikicha lugha kama Kenya.

Wakongo.
Mimi ninazungumza Kifaransa. Kila ninaposikiliza runinga za Kifaransa zinapotoa vipindi kuhusu Afrika hugundua wenzetu wa nchi za Senegal, Kongo, Cameroon, Burkina Faso, Ivory Coast nk huongea Kifaransa fasaha kabisa. Nikisema “fasaha” nina maana wamekisoma vizuri – sarufi zao hazijakaa vibaya, na hata kama matamshi yana lafudhi za makabila au lugha zao kama Kiwolof (Senegal) na Kilingala au Kingwana (Kiswahili cha Kizaire), hutiririsha Kifaransa bila noma. Hapo hapo huongea lugha zao asilia. Tukiangalia  zaidi majirani zetu wa Kongo wanao mtindo wa kukoroga Kilingala, Kiswahili (Kingwana) na Kifaransa bakuli moja. Angalia mfano wa sentensi ifuatayo:
“Dii...mambo eiko bien hata kidogo. Makuta kitoko, vraiment,  dii.”
Dii ni neno la Kifaransa linaloimanisha “kusema” (“dire” au “dit”); kama “aisee” yetu (iliyotokana na Kiingereza “I say”- Ninasema ).
Kitabu kimojawapo cha mwandishi mashuhuri wa Kiswahili, Mohammed Said Abdullah...bahati nzuri maandishi ya nguli huyu bado yanapatikana katika maduka machache ya vitabu tuliyo nayo bara na visiwani.

 “Mambo hayako bien” mambo si mazuri. “Bien” ni safi, nzuri, nk. “Makuta” ni fedha kwa Kilingala-ingawa saa nyingine pia hutumia “falanga” yenye asili ya “francs” fedha ya zamani kabla ya Euro;  ambapo “vraiment” (tamka “vreimaa”) ni “kweli” kwa Kifaransa. “Kitoko” ni “kidogo” maana viswahili mbalimbali hubatili maneno kufuatana na makabila, vitongoji, lahaja, nk...
Kwa mfano Waganda huita ugali “ka-unga”...ukichimba hapo huwezi kuwalaumu, maana “unga” ndiyo hutengenezea ugali. Kwao hao hao Waganda, kanga ni “leso”- pia hawajakosea maana tunavyojua “leso” kwa Kiswahili fasaha ni kitambaa cha mfukoni. Tofauti hizi za misamiati na lahaja katika lugha moja si jambo geni. Linganisha Waingereza na Wamarekani. Waingereza huita mashine ya kupanda ghorofani –“lift” na Wamarekani husema “elevator.” Mmarekani atasema “sidewalk” kuimanisha sehemu ambayo wapita miguu hutembelea barabarani –  Mwingereza ataiita: “pavement.”
Kireno cha Ulaya na cha Brazili hali kadhalika. Mzungumzaji Kireno Ulaya atamwita mtoto “miuda” ilhali Mbrazili na Kireno hicho hicho atasema “criança” (tamka “kriansa”).
Tukirejea tena kwa Wakongo; ingawa wao huchanganya sana lugha, ukiongea nao Kifaransa fasaha hawana tatizo kabisa. Hali kadhalika raia wa Waafrika Kusini. Huongea Kiingereza fasaha halafu ghafla wakaweka Kizulu, Kisuto au Kitswana.
Kusoma fasihi mseto wa Kiingereza na Kiswahili ni kiini cha kukuendeleza kilugha. Hapa mbali na Adam Shafi maandishi ya magwiji wawili washindi wa tuzo la Nobel- VS Naipaul (toka Trinidad) na Ernest Hemwingway...hawa ni waandishi wazuri sana wa Kiingereza.

Tunafahamu Waafrika Kusini walivyo wazuri katika sinema, uandishi wa vitabu na masuala mengine yanayotaka lugha za Kizungu. Wanamuziki wakubwa wakubwa duniani wamezaliwa huko.  Hayati Miriam Makeba alihusudu kuimba lugha mbalimbali – Kitswana, Kizulu, Kisuto – na pia Kiingereza, Kifaransa, Kireno, nk. Alipata sifa kutokana na sauti na nyimbo zake za ujanani zilizowasisimua wasikilizaji kwa vile alitumia lugha za kigeni na  mama – mfano ule wimbo anaosonya midomo (kama Wasandawi Tanzania) – Waingereza waliuita “Click Song.”
Mwandishi wa pili kupata tuzo la Nobel ya fasihi barani Afrika ( wa kwanza alikua Wole Soyinka wa Nigeria) , Nadime Gordimer ni mzawa wa Afrika Kusini. Ina maana wanapochanganya lugha, hawapotezi kitu,  wanajua kuzitumia.
Hii mifano inatufundisha kuwa wenzetu wanapochanganya lugha hufanya hivyo kujazia kile timamu walicho nacho tayari.
Wazungu lakini hawana tabia ya kuchanganya changanya lugha zao ovyo. Huwezi kumkuta Mwingereza akiongea jambo akalichanganya na sentensi ya lugha nyingine. Anaweza kukopa neno moja la Kilatini, Kiarabu, Kihindi au Kifaransa; lakini huwa neno moja tu- mara nyingi katika fasihi, sheria au taaluma za kifalsafa. Wafaransa ni  wakali na watetezi wakubwa wa lugha yao. Ukizungumza na Mfaransa ukichemsha lugha yake anaweza asikujibu. Hawataki utani au mchezo na lugha yao.
Sisi tatizo letu ni nini? Je tunakifahamu Kiswahili vizuri? Je, tunakiboresha kwa kusoma vitabu na fasihi ya Kiswahili? Na je, Kiingereza? Kwanini majirani zetu wa Uganda na Kenya wanatusuta kwamba tunazungumza  Kiingereza kibovu? Tunachotakiwa sasa hivi ni kuboresha kwanza Kiingereza kabla  kukibandika bandika kiholela juu ya sentensi za Kiswahili. Ndiyo sababu Kiswanglish kwa sasa hakina faida yeyote- maana bado hatujakaa sawa.
Kwa vipi?
 Matokeo ya “bandika bandika” na “azima azima” hii ni  wengi wetu kutomudu hata lugha moja sawasawa. Mtaka mawili yote humponyoka. Tupo wengi ambao hata lugha za kikabila zinatushinda. Tumekua na Kiswahili- lugha yetu mahsusi na asilia –lakini karibuni tumeanza kukidhoofisha na kukichuja kwa sentensi au misemo ya Kiingereza.
Profesa Euphrase Kezilahabi, mwandishi mashuhuri wa siku nyingi ambaye anafundisha Fasihi Botswana akiwa mjini Berlin na mhadhiri wa Kiswahili, Lutz Deigner anayefundisha chuo kikuu cha Humbodt, Mei 2012. Picha na F Macha.

Wale tuliobahatika kusoma shule ambazo zilifundisha lugha hizi mbili vyema hasa enzi za Mwalimu Nyerere-  tunaoelekea uzeeni- tulizoea kumsikia Baba wa Taifa akisema na kuandika Kiswahili na Kiingereza vyote viwili fasaha, hatuna shida. Mwalimu alitafsiri vitabu vigumu vya nguli wa fasihi ya Kiingereza- William Shakespeare kuja Kiswahili. Ingefaa tuvisome vitabu hivyo kwa undani zaidi.
Kwa kumalizia habari hii tukumbushane tena.
 Kuchanganya lugha kama wanavyofanya  Kenya, Kongo na Afrika Kusini si vibaya- lakini  wenzetu hawa tayari wanazimanya lugha za kigeni sawasawa. Hadi pale tutakapojua kuandika na kuongea Kiingereza fasaha- ndipo tutapokubalika kusifia na kutukuza Kiswangilish. Matumizi ya Kiswanglish kwa sasa ni kama kumpa mtoto mdogo asiyejua kukata nanasi sawasawa kisu.
Si atajikata?

 Orodha ya nyimbo na tenzi za  Kiswahili na Kiingereza  ya CD na kitabu cha mwanamuziki na mtunzi wa Mashairi (Double Focus) Nasibu "Ras Nas" Mwanukuzi. Ras Nas anayeishi Norway ni mmoja wa Watanzania wanaozimanya lugha hizi mbili na kuzitumia sawia katika maonyesho yake ya kimataifa.

Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili...

No comments:

Post a Comment