Ladha ni kitu muhimu sana.
Siku moja nilikuwa nimealikwa karamu fulani kubwa- mwenyeji ni Mzungu aliyemwoa bibi wa Kiafrika. Kufumba na kufumbua dada mmoja, (sikumbuki taifa lake, lakini alikuwa Mwafrika)-hakuwa na raha hata kidogo na misosi. Kawaida ukialikwa hizi karamu za kimataifa, si mara zote utakuta vyakula vya kwenu; ulivyozoea. Mathalan, Wazungu wanavyokula ni tofauti sana na sisi. Hutumia vitu ambavyo si mazoea yetu mfano jibini (chizi), kachumbari nzito (“mayonnaise”) yenye mayai, siki, mafuta, malai (“cream”), nk. Au kuna suala la nyama.
Siku hizi idadi ya wasiopenda nyama jamii zilizoendelea imekua kubwa kiasi ambacho ukihudhuria mikutano au makongamano ya kimataifa unaulizwa (kabla) je mlaji nyama au hapana.Basi dada hakua na raha.Meza zilijazana vyakula vya wanga, mboga, nyama na protini. Dada alilalamika ladha.
“Hiki chakula sijui kikoje; mdomoni hakiingii.”
Turudi nyuma. Mtoto mdogo hupenda
sana sukari na ndiyo maana lawalawa humnyamazisha akighafilika. Karibuni hapa
Uingereza, serikali imetahadharisha makampuni yanayojaza sana sukari na chumvi ndani ya
vyakula wanavyouziwa watoto. Wafanyabiashara wanawahadaa watoto ili kupata fedha. Sukari nyingi kuharibu meno
ya watoto; huchangia unene na kuwafanya wasitulie wakachangamka kupindukia
wakati wa masomo.
Jambo hili limeifanya jumuiya ya mataifa ya Ulaya (EEU) kupitisha sera ya
kubandika muhtasari wa nini kilichomo ndani ya vyakula madukani. Utaratibu huu unazifaa
jumuiya zenye watu waliosoma ambazo ndizo nchi tajiri. Je kwa nchi maskini? Je,
ni kila mtu atafuatilia ni kiasi gani cha sukari na chumvi iliyopo ndani ya
vyakula madukani? Ladha ni kitu kinachotumwia sana na wafanyabiashara. Kila taifa lina ladha zake maalum. Mara nyingi
ladha hizi zinapendeza mdomo lakini madhara yake mwilini hayaelezwi na makampuni
makubwa. Mathalan ukizidisha sana sukari
na usiposukutua sawasawa waweza kuharibu meno na kuongeza harufu mbaya
ya mdomo. Tuendelee.
Hatimaye malalamiko ya dada yalimfikia mmoja wa wahudumu, akaja mbio.
Dada: “Pilipili na chumvi tafadhali.”
Mhudumu akatazama huku na kule.
“Ipo Reggae Reggae
Sauce. N’kuletee?”
Dada akatokwa macho kama mtu aliyeona mwangaza baada ya umeme wa mgao kupotea juma zima.
“Reggae Reggae Sauce ndiyo yenyewe.
Na chumvi tafadhali.”
Reggae Reggae Sauce ni mseto wa pilipili, binzari, kitunguu, chumvi,
kitunguu saumu, mdalasini, siki, tangawizi,
nk. Bei ya kachupa kamoja ni wastani wa
shilingi elfu saba, London. Mseto ulivumbuliwa na mwanamuziki Mjamaika, Levi
Roots mwaka 2007.
Sasa. Mhh. Leo chumvi ni suala linaloongolewa sana katika majarida ya afya, waganga na
watu wanaohimiza chakula bora.
Mbali na chumvi kidesturi wengi wetu tumezoea kula chakula huku tukinywa chai, maji, pombe, juisi, na vinywaji vingine
vya sukari sukari. Tabia hii ya kunywa vitu huku tunakula imezoeleka kiasi
ambacho tunaiona ya kawaida, lakini si nzuri kwa ini, figo na utumbo.
Chumvi inavutia sana vinywaji shauri hukausha mdomo, tumbo na damu. Kadri
unavyozidisha chumvi ndivyo unaharibu damu yako. Wataalamu wengi wa afya
wameonya chumvi nyingi inaweza kuathiri wanawake wakati wa siku zao. Kufuatana
na maelezo ya shirika la maradhi ya presha ya moyo Uingereza, chumvi ikizidi husababisha
maradhi ya moyo, saratani ya tumbo, matatizo ya figo, ubongo (kuwa msahaulifu
uzeeni), maradhi ya mifupa (“osteoporosis”), pumu nk.
Hali ni mbaya kiasi ambacho shirika la Afya duniani (WHO) limesema ulaji
mkubwa wa chumvi unatakiwa kupunguzwa kama ambavyo uvutaji sigara unatakiwa. Mwaka
2005, WHO ilitangaza vifo 35 milioni duniani vilivyotokana na maradhi
yasiyoponyeka- kati yake asilimia 30 yamesababishwa na moyo. Kati ya maradhi haya,
manane hutokea kwa watu wenye kima cha chini cha mshahara hasa nchi
zinazoendelea likiwepo bara Afrika. Magonjwa husika ni moyo, presha na kisukari
cha aina ya Type 2 – kinachotokana na
unene, ulaji mbaya, pombe nk. WHO imeitaja Nigeria ambapo maradhi ya moyo na
presha, huathiri watu milioni 8- yaani asilimia 10 hadi 12 ya taifa hilo.
Miezi mitatu iliyopita runinga ya Sky hapa London ilitahadharisha Waafrika
na watu weusi duniani kwa utumiaji kupindukia wa chumvi, na kwamba kitakwimu
tunaongoza kwa vifo vya madhara yake.
Kiasi cha chumvi kinachotakiwa kwa
siku (kwa mtu aliye na umri wa miaka 11
kuendelea) ni gramu tano. Huu ni uzito
wa chumvi ya unga ndani ya kijiko kidogo cha chai. Kipimo hiki kimewekwa na kukubaliwa na
mashirika ya kiganga na WHO yenyewe.
Wapo watafiti wanaokinzana na kipimo; wanadai watu wanaochuruzikwa sana
jasho – wanaofanya kazi za sulubu, wanamichezo na wakazi wa nchi za joto-
wanatakiwa wale chumvi zaidi. Lakini pamoja na hayo, kutokana na vifo
vinavyoendelea, wananchi jamii hizi bado
wanakula chumvi nyingi kuliko inavyotakiwa.
Utafiti uliofanywa mwaka juzi na mganga mstahiwa, Dk Derin Balogun (anayeongoza
kampeni dhidi ya kuondoa maradhi ya moyo na presha) uligundua kwamba mahoteli
ya Waafrika na watu weusi jijini London hupika vyakula vyenye chumvi nyingi
sana. Gramu 12 zilipatikana katika wali na maharagwe, gramu 8.6 ndani ya wali (maarufu)
wa “Jollof” toka Afrika Magharibi na gramu 19 kwenye mikate. Hii ni chumvi zaidi ya gramu 5 zinazotakiwa kwa mtu mzima,
kila siku.
Akiongea Nigeria mwaka 2008, Dk Balogun alisema tatizo hili -linaloua wengi-
linasababishwa na “chakula chenye mafuta na chumvi kwa wingi; unene, kutofanya
mazoezi na kutokula mboga za majani na matunda.”
Suala la mazoezi ni muhimu sana. Jingine
muhimu ni unywaji maji.
Mseto wa majani ya Salad (bila chumvi yeyote) unaweza kusaidia kuweka uwiano kwa chakula kilichojaa chumvi, pilipili nk
Ulaji chumvi nyingi unasababisha kiu; chumvi ina madini inayonyonya damu
(“sodium”) na ndiyo sababu wengi wetu tumejenga desturi ya kupata kinywaji
wakati wa kula. Si vizuri kunywa maji pamoja na chakula. Maji yanatakiwa
kunywewa dakika 15-30 kabla au baada ya chakula ili kutoharibu umeng’enywaji
tumboni.
Kuna, aghalabu, starehe na dimba la mazoea. Ilinichukua muda kuzoea kula
bila chumvi nyingi. Ilibidi nijifunze. Wataalamu wanashauri ukimudu kupunguza
asilimia 60 ya chumvi unayotumia kila siku unajenga nguvu za moyo, miondoko ya
damu mwilini na hatimaye kuongeza urefu wa maisha yako. Vyakula na mimea vina
chumvi asilia toka ardhini na rutuba ya ulimwengu. Chumvi ni mazoea tu ya kiladha.
Zamani wanadamu hatukutumia chumvi
nyingi kama leo.
Ilitoka pia Mwananchi Jumapili....
No comments:
Post a Comment