Thursday 4 December 2014

WATANZANIA TUJIFUNZE KUWEKA AFYA MIKONONI, TUSISUBIRI KUDRA YA WAKUBWA AU MUNGU





 Miaka yote niliyosafiri na kuishi ughaibuni nimebaini siri moja  kuhusu afya. Wananchi wengi duniani hawaijali miili hadi wanapougua.  Zamani kidogo nilikuwa nikiongea na mganga wangu wa Kichina. Nilikwenda kuchomwa zile sindano zao zinazobandikwa sehemu mbalimbali mwilini na kuachwa zimesimama juu ya ngozi mithili ya mishale ya nungu nungu. Accupuncture (tamka “Akapan-kcha”), ndiyo jina lake la kitaalamu. Tiba hii iligunduliwa, kutafitiwa na kuendelezwa maelfu ya miaka kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo na Mtume Muhammad SAW.   Kazi ya sindano hizi  ni kurekebisha na kusawazisha nguvu (au umeme) mwilini. Unapochomwa tatizo si maumivu. Haziumi kama sindano za Kizungu tulizozoea. Kinachochachafya ni vile Mchina anavyotafuta “njia sahihi.” Je, umewahi kushika waya wenye umeme? Unaukumbuka ule mstuko? Ukiwa mdogo, ndivyo  Accupuncture ilivyo. 
 Sindano za Kichina. Picha ya Mtandaoni