Miaka yote niliyosafiri na
kuishi ughaibuni nimebaini siri moja kuhusu afya. Wananchi wengi duniani hawaijali
miili hadi wanapougua. Zamani kidogo nilikuwa
nikiongea na mganga wangu wa Kichina. Nilikwenda kuchomwa zile sindano zao
zinazobandikwa sehemu mbalimbali mwilini na kuachwa zimesimama juu ya ngozi mithili
ya mishale ya nungu nungu. Accupuncture (tamka “Akapan-kcha”), ndiyo jina lake
la kitaalamu. Tiba hii iligunduliwa, kutafitiwa na kuendelezwa maelfu ya miaka
kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo na Mtume Muhammad SAW. Kazi ya
sindano hizi ni kurekebisha na
kusawazisha nguvu (au umeme) mwilini. Unapochomwa tatizo si maumivu. Haziumi
kama sindano za Kizungu tulizozoea. Kinachochachafya ni vile Mchina
anavyotafuta “njia sahihi.” Je, umewahi kushika waya wenye umeme? Unaukumbuka
ule mstuko? Ukiwa mdogo, ndivyo
Accupuncture ilivyo.
Sindano za Kichina. Picha ya Mtandaoni
Mbali na sindano mganga huacha taa zikichoma juu ya zile sindano. Ingawa husikii maumivu yeyote, kinachofanyika huiathiri mitiririko ya mifereji yako asilia. Ikiziba, ndipo mtu hupatwa maradhi. Muundo mzima wa tiba za Kichina (na Mashariki mathalan Ayudervic ya Wahindi) ni tofauti na tuliouzoea wa sayansi ya Kizungu. Unapoingia chumba cha daktari wa Kizungu (au aliyesomea mfumo wa Kizungu) anachotazama ni namna ya kutatua. Unadungwa sindano au unapewa vidonge. Bas.
Mambo yamekwisha. Tiba za Kichina ziko kinyume.
Utaombwa utoe ulimi nje. Utachunguzwa wekundu wake, nchani. Mkali sana au hafifu? Hapo atajua
hisia zako zikoje. Atakunusa. Atakuuliza unalalaje? Ndoto zako, zikoje. Atataka kujua
unapokula chakula kina vitu gani. Je mna binzari na pilipili?
Utaratibu wa tiba za Kichina umeanza kupokelewa kutokana
na dawa za Kizungu kudhuru au kuwa sugu kwa virusi. Miaka kama kumi iliyopita nilikuwa na maumivu
makali shingoni, chini ya sikio. Bahati
nzuri daktari wangu wa Kizungu alikuwa aina ya wale matabibu walioanza
kufunguka macho. Baada ya kunipima moyo, sikio, kichwa na kadhalika akakiri
hakuna noma. Hakunipa dawa. Hakunichoma
sindano.
“Nenda kwa msingaji
akakukande,” akaasa. Na kweli msingaji akaniuliza vipi ninafanya kazi gani.
Nikamwambia muziki. Kutokana na kazi ya kupinda bega moja ninapopiga gitaa, au
kuinama kinamna ninapotwanga ngoma au piano,
vyote viliathiri shingo na mabega. Baada ya kusingwa mara kadhaa ikawa neema, lakini mwezi mmoja kwisha,
yakarejea tena. Nilipokwenda kwa Mchina alinipachika hizo sindano za Accupuncture.
Sijalisikia tena tatizo; hadi kesho. Ingekuwa zamani, waganga wa Kizungu wangenipa
tu dawa za kupunguza maumivu ambazo hazingemwondoa mjusi kafiri.
Sisi Waafrika, hali
kadhalika, tuna tiba zetu asilia. Walakin,
tumezitupilia mbali.Matokeo tiba zetu zimechujwa badala yake zikabakizwa imani za
ushirikina tunazozitumia kulogana na kufanyiana uhayawani. Kama kuua Albino.
Wachina nao walitawaliwa
na wageni. Mwanzo wa karne ya 20 kwa mfano, tiba asilia za Kichina (mseto wa
miti shamba na Accupunture) zilitupwa shimoni. Wenyeji wakaenzi, sayansi za
Kizungu. Wakati wa vita vya mapinduzi yaliyoongozwa na Mwenyekiti Mao Ze Dung
miaka ya Thelathini maradhi na majeraha hayakuponyeka. Ndipo serikali mpya
iliyoundwa 1947 ikarejesha tiba asilia.
China leo inasifika (na kuuza) tiba zake asilia sehemu mbalimbali za
dunia; tena aghali.
Mwongozo mzima wa Wachina
umelala katika kinga. Hiyo hiyo,
Accupuncture ambayo sisi huchomwa tunapougua wao hufanyiwa kinga maradhi.
Anayeonja asali huchonga mzinga.
“Kazi yake,” alinieleza
Dr Xin (aliyeshastaafu), “ni kurekebisha mtiririko wa umeme wa nguvu mwilini.Si
lazima uwe mgonjwa. Hata watoto wadogo wamezoea.”
Ukiacha tiba hii ya nungu nungu, kuna mazoezi ya viungo na sanaa. Mfano mzuri ni
wazee. Hufanya mazoezi ya viungo yanayoitwa Tai Chi Chuan; aina ya dansi taratibu
inayojenga msingi na uwiano na ustahilimivu wa mifupa. Juu yake wazee
hushauriwa kujifunza kuchora, kupiga chombo cha muziki, mahesabu, nk.
Dr Xin alisisitiza kwa vile ubongo wa
mwanadamu nao huzeeka, kujifunza kitu
kipya baada ya miaka sitini au sabini huujenga. Jingine, ulaji wa miti shamba.
Mfano, mimea iitwayo Gingko na Cordyceps.
Majani ya Gingko. Picha ya Mtandaoni
Cordyceps ni aina ya Uyoga unaosaidia viini
vya mishipa ya damu na kukomaza kinga maradhi kupitia ini na viungo vya tumbo. Gingko
ni mti mkubwa unaoota China, Japan na Korea, takribani miaka 270 milioni sasa. Una nguvu na uwezo kiasi
ambacho wadudu hushindwa kuushambulia. Bomu
la Atomiki lilipopasuliwa Japani mwaka 1945, baadhi ya viumbe ambavyo
havikuharibika ni miti ya Gingko. Ingawa
iliunguzwa, mizizi na mashina yake
yalinyauka tena na mengi yangali hai, leo. Gingko hutumiwa kuimarisha ubongo na
kutibu kupotelewa kumbukumbu hasa kwa wazee na watu waliovuta bangi kipindi
kirefu. Si ajabu wenzetu China na Japan
huishi kitambo sana.
Fundisho nini?
Kazi ya waganga na
hospitali ni kututibu. Ila sehemu kubwa ya siha yetu inatutegemea sisi wenyewe.
Kijarida kinachosambazwa sehemu mbalimbali Uingereza kinasisitiza
maradhi yanayopunguza au kuondoa kabisa maisha yetu,(mbali na UKIMWI,
Malaria na aina kadhaa za Saratani) ni moyo, shinikizo la damu, kisukari na
figo kutokana na kutojiangalia sawasawa.
Chapati na sambusa..mfano wa vyakula vya wanga tulivyozoea. Vyahitaji kusaidiana na mboga mboga hata kama wala nyama.
Ushauri unaotolewa kuepuka
madhila ni kutovuta sigara, unene, kufanya mazoezi ya viungo na kuangalia damu.
Damu ikipimwa iwe chini ya vipimo 120 au
isipite 80. Vipimo hivi vinavyoitwa “sytolic” na “diastolic” huangalia mishipa
ya damu inavyokwenda. Mbali na mazoezi
ya viungo ushauri unaotolewa ni kupunguza chumvi na kunywa maji. Chumvi nyingi husababisha
shinikizo la damu au saratani ya tumbo. Chumvi nyingi ni zaidi ya gramu 1.5;
yaani kijiko kimoja au viwili vya chai kwa siku kwa mtu mmoja.
Mseto wa mboga za matango, nazi na mbegu mbichi za Mlozi. Mseto bab
kubwa huu kwa Salad. Rutuba ya madini mwilini kusaidia mifupa, ngozi,
nywele, nguvu za urijali, ngono, nk ...
Jingine muhimu ni kufanya vitendo
vinavyoendesha mapigo yako ya moyo na
mapafu kwenda haraka dakika 30, mara tano, kwa juma. Mazoezi ya viungo au
kutembea haraka. Unasisitiziwa ule aina tano za matunda na mboga kwa siku
kuhakikisha uzito unabakia kawaida. Wengi wetu hula zaidi vyakula vya wanga au
nafaka, lakini hatuzingatii mboga mbichi
za majani na matunda. Unene huchangia shinikizo la damu. Kupunguza unene,
jaribu kula nyama zisizo na mafuta, nyama za kukaanga. Unapokula vyakula
vilivyokaangwa hakikisha pia unapata mboga au maharage na kunde ili kupunguza
mafuta ya wanyama ambayo si mazuri mwilini.
Ilichapishwa Mwananchi Jumapili- 30 Novemba, 2014
No comments:
Post a Comment