Watanzania tuamke jamani. Tumelala.
....Kiswahili kilianzia kwetu. Nchi kumi na moja
zinazungumza lugha hii iliyotuunganisha na kutuletea amani zaidi ya miaka 100!
Nchi kumi na moja!
Ongezea idhaa kadhaa za redio, TV na mitandao jamii ughaibuni inayokitukuza
Kiswahili. Jazia, vyuo.
Hapa London kiko
chuo maarufu cha lugha- SOAS ( School of Oriental and African Studies- Shule ya
Masomo ya Mashariki na Afrika).
Mtaa wa Russel Square, katikati ya jiji. Si
vichochoroni kwa walala hoi. Hapa Russel
Square alipigwa kisu mhadhiri wa Kimarekani miezi michache iliyopita na gaidi aliyechanganyikiwa akili. Na 7 Julai 2005 basi lililipuliwa na magaidi wanne
waliofariki kishabiki na kishabiki.
SOAS iko Uzunguni.
Ukiingia chuoni utashangaa namna vijana – toka mataifa
mbalimbali wanavyozungumza Kiswahili, tena kwa hamasa. Mwaka 2010 niliitwa kutumbuiza
ngoma kusheherekea kuanzishwa klabu ya wazungumzaji Kiswahili, SOAS.
Mmoja alinieleza alivyoporwa na teksi ya kihuni akitalii
Tanzania. Lakini hakulichukua tendo la kuibiwa na vibaka kujenga chuki kwa
Watanzania. Kila mahali huwepo wazuri na wabaya alisema. ”Kila kapu huwa na
matufaha yaliyooza na mazuri” – ni msemo wa Kiingereza usiopenda kuweka watu
wote katika kundi moja. Wenzetu wanakipenda Kiswahili.
Siku hiyo hiyo ya 2010, alikuwepo pia mzee wetu, mtaalamu
msifika wa Kiswahili, Dk Farouk Topan. Namheshimu.
Mwandishi nikiwa na Dokta Farouk Topan, Ismailia Centre, London, 2016. Picha na Z Macha
Wakati nikisoma bado Mzumbe kilikuwa
kipindi cha malumbano makali sana kati ya washairi wa vina na mizani (jadi ) na
washairi wa mashairi huria (guni) yasiyofuata kanuni za urari au mfanano huo. Profesa Euphrase Kezilahabi (mwandishi mashuhuri wa
riwaya za Kiswahili) alitoka na mkusanyiko wa mashairi guni ulioitwa Kichomi.
Utangulizi wake uliandikwa na Dk. Farouk Topan. Dk Topan kaandika vitabu vingi
vya taaluma ya Kiswahili na tamthiliya.
Alifundisha muda
mrefu SOAS. Kastaafu. Bado wapo
wahadhiri wengi wa Kiswahili toka Kenya na Tanzania.
Mwezi jana
nilikutana naye Dk Topan ndani ya tafrija kusheherekea miaka 400 ya maisha ya mwandishi nguli wa Uingereza William
Shakespeare. Dk Topan alialikwa rasmi kuhutubia jumba maalum la Waismailia hapa London.
Akaelezea uhusiano wa Kiswahili na fasihi zake Shakespeare. Walijazana wengi
pale hasa Wahindi waliozaliwa Afrika Mashariki. Wanakihusudu Kiswahili ingawa
walihamia nje zamani.
Dk Topan alitaja
baadhi ya waandishi wetu waliotafsiri kazi zake Shakespeare kuja Kiswahili.
Kama Mwalimu Nyerere aliyetafsiri Mabepari wa Venice (Merchants of Venice) na
Julius Kaizari, kisa cha mfalme wa Kirumi aliyeuawa na mawaziri wake.
Mitaani je?
Mwezi jana lilikuwepo tamasha la siku kadhaa kusheherekea
masuala ya watu weusi jumba maarufu la
starehe Royal Festival Hall. Nikaajiriwa
kuendesha darasa la Kiswahili
kupitia muziki. Aliyenialika ni dada wa
Ki-Eritrea anayekifagilia KIswahili. Nikatumia wimbo mashuhuri wa “Malaika” na “Sura
Yako” wa Sauti Sol- wanamuziki toka Kenya. Kwanini nyimbo hizi zilitumiwa? Kwa
sababu maneno yake yameandikwa mtandaoni na You Tube. Nani watunzi? Wa Kenya.
Zingatia wa Kenya walivyo mstari wa mbele katika utunzi wa nyimbo za Kiswahili.
Mwingine unaosifika ni Jambo Jambo (Hakuna Matata) wa bendi ya Uyoga au
Mushrooms.
Mwezi huo huo wa Septemba nilialikwa kujiunga na kundi la
mtandao jamii wa “WhatsUp” - Kiswahili
Club. Hawa wala si wazee walioishi Tanganyika enzi za Ukoloni na Ujamaa. La
hasha.. Wengi ni vijana waliozaliwa baada ya 1980. Wanakienzi Kiswahili. Hunitaka niwasahihishe kila wanapoandika au
kuzungumza....
Mnaona?
Hii ni mifano michache tu ya jinsi lugha hii inavyozidi
kusambaza matawi na mabawa duniani.
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa ulitangaza lugha kumi
zinazokua kasi duniani na kudai Kiswahili ni ya saba! Nyingine ni Kispanyola, Kichina, Kiarabu, nk.
Maana yake nini?
Mosi , biashara.
Mnaolilia ajira.
Zingatieni.
Mangapi unayoweza kuyafanya kuuza Kiswahili?
Kwanza je unakimanya vizuri ? Kama bado jifunze sarufi
sawasawa. Pili, zingatia matumizi sahihi ya maneno na lahaja. Viko Viswahili
vya aina saba. Fasaha, Kingwana (Cha Kongo), Kingazija, Cha ukanda wa Ziwa Victoria (Burundi na Rwanda), Kimvita, Kishenge (au Kiswanglish cha Kenya),
na Kimrima (cha Dar es Salaam na mwambao). Je unavifahamu?
Zingatia maendeleo mengine muhimu. Wataalamu wawili wa
Kiswahili, Profesa Saidi Ahmed Mohammed (mtunzi wa kitabu maarufu Asali Chungu,
1976)na Prof Mohammed A. Mohammed, walichapisha Kamusi ya Visawe, mwaka 2002. Imechapwa tena. Kisawe ni neno linalofanana na jingine.
Kiingereza ni “Synonym.”
Kamusi ya visawe hukusaidia unapotaka kusema neno lile lile bila kulirudia
. Kwa mfano, mathalan, bimithili, tuseme, nk. Banja, pasua, vunja, bangua, nk.
Ruhusa, idhini, ridhaa, itikio, kubalia, achia, nk.
Kamusi hii haikuwepo katika Kiswahili.
Kwa lugha nyingine kubwa, licha ya kamusi, ukiingia tu Google
kutafuta visawe vyake utavipata. Kiswahili
hakuna.
Mbali ya Kamusi ya Visawe , kamusi mpya za TUKI za
Kiingereza na Kiswahili zimetolewa upya karibuni na kurasa nyingi na maneno
zaidi. Ya Kiingereza kuja Kiswahili mathalan, imeongezeka kurasa 900 hadi 1000. Maana yake nini?
Msamiati wa Kiswahili unaongezeka. Kazi nazo zazidi kuwa nzuri.
Maendeleo hayo, yanakuja.
Kinachoharibu si wataalamu wa lugha: magwiji wanaotunga
riwaya, au kufundisha vyuo na kamusi. La hasha.
Tunaoharibu ni
wanasiasa, wanahabari, waalimu mashuleni na watunzi wa nyimbo wanaoendelea kutukuza
Kiswanglish na kuparaganya herufi L na R, kama rafiki yangu Masudi Pashamoto
Msele.
Tatizo hili
lilikuwa dogo zamani kutokana na watu wa mikoani kutojua sawasawa lugha. Linazidi
kukua. Watanzania wengi wanaoandika mitandaoni na mablogi
hawatofautishi “ bahili” na “bahiri”,
“ mhalifu” na “mharifu”, “mpira” na “mpila.” Zamani watoto wadogo walioota
mapengo ndiyo walioharibu. Siku hizi tunashindwa kupambanua. Sikiliza wimbo
mpya wa Diamond -Salome. Mara ngapi karudia neno “Sarome”?
Wasikilize watangazaji wa redio FM wanavyochanganya na
kuboronga nahau kwa kusema “Nyimbo hii”
badala ya “wimbo huu”- au “nyimbo hizi”-wanashindwa kutaksirisha wingi wa neno “wimbo” kuwa “nyimbo.”
Toba!
Sasa ikiwa wanahabari,
wasanii, wanasiasa na waalimu mashuleni tunawafundisha watoto kusema “Luninga”
kinyume cha “Runinga,” nani ataokoa jahazi la kesho? Nani atasahihisha wanaokua na kuiga
kusema “Sarome” kwa kuwa mtu maarufu kaimba vile? Je wahusika tunasoma na kujifunza Kiswahili
sawasawa? Au tunajimamasa na kubabaisha tu ?
-ilichapishwa sehemu mbili Mwananchi Jumapili 23 na 30 Oktoba 2016
No comments:
Post a Comment