Tuesday, 4 October 2016

WASANII WAKAZI UINGEREZA WAJIUNGA CHINI YA BALOZI MIGIRO



 Moja ya mambo yanayochekesha na kusitikitisha kuhusu Watanzania wakazi Ughaibuni ni kuogopana. Si tu kuogopana kama ilivyo  Afrika nzima, yaani hofu ya kulogana. Wala si tu  kuwa na wasiwasi wa fitina na masengenyo ya eti mwenzako atakujua unakulaje, unalalaje au utawezaje  kumsaidia.
Hofu ya kukwepa ofisi zetu za Ubalozi.


 Nakumbuka nilivyofika Ulaya mara ya kwanza miaka ile ya Themanini, ilibidi kujipiga sana moyo konde  kwenda ofisi zetu za Ubalozi. Ulipoingia ulichachafya eti  maofisa Balozi watataka kujua umekuja kutafuta nini. Je una shida? Je umefukuzwa na wenyeji? Tatizo jingine lilikuwa hofu ya wanausalama tuliowakatia jina la Mashushushu. Miye binafsi sidhani tatizo lilikuwa kubwa kiasi hicho. Ila kisaikolojia Watanzania tulichelea tu jicho la serikali. Kwamba unachunguzwa. Kwamba wako viranja wa dola, popote pale, wakikukodolea.
Unasikilizwa katika simu, barua zinasomwa (enzi za kabla ya mitandao na barua pepe), mienendo yako nje na ndani inafuatiliwa. Wasiwasi huu (usiokuwa na thibitisho la hakika) unaitwa “paranoia” kwa lugha ya kitaalam. Kamusi mpya ya TUKI (iliyochapwa upya mwaka jana) inatuainisha kuwa  paranoia ni “wazimu usiotibika wa kujiona unaonewa kila wakati,”

Kisaikolojia neno “paranoia” laweza kupambanuliwa zaidi. Lugha ya Kiingereza inasema mbali na kudhani unaonewa (“persecution complex”), kuna pia hisia za wivu usio na maana na  kujiona wewe bora zaidi ya wengine. Na hili yaweza kuwa matokeo ya mtu kuwa na tabia zenye matawi mawili,  zinazotofautiana kabisa;  (“split personality disorder”) au pia maradhi ya Schizophrenia (ambapo mtu husikia sauti zikimwambia afanye jambo fulani), hilo mara nyingi huweza kuwa matokeo ya kutumia sana dawa za kulevya. Kwa wavuta bangi hiyo ni moja ya athari kuu. Baadaye huzua uenda wazimu au kichaa. Leo ni tatizo kubwa sana nchi tajiri.
Sasa kijamii “paranoia” iliyoenea Tanzania enzi za iasa ya Ujamaa ilitokana na wasiwasi kuwa Chama na Serikali vinawatafuta wapinzani na kuwachunguza wananchi popote walipo. Tabia na hisia hii (ambayo ilikuwa kweli na pia si kweli) ilikuwepo  (au bado ipo) nchi zinazoendesha siasa za kikomunisti mathalan Korea ya Kaskazini. Nchi hizi huwa na chama kimoja tu cha kisiasa. Hairuhusiwi kuunda chama pinzani ama kusema lolote linalokinzana na watawala, nk.
Kihivyo basi tunaweza kuelewa kwanini Watanzania wengi walipofika ( na wanapofika) ugenini hawakushughulisha kwenda Ubalozini. Lakini walipofariki,  ndugu hupiga hodi milango hiyo hiyo walio igopa, kuomba msaada.

Ukweli wanaosafiri nje huenda kwa  sababu mbalimbali. Wengine huja kusoma. Wakishamaliza hurejea na shahada na taaluma zao. Au kupiga boksi yaani, kikazi. Wapo wanaokuja kutembea au kutembelea ndugu na marafiki. Hawa ni wachache ukilinganisha na wenzetu weupe ambao kimila na desturi hutalii nchi za kigeni. Halafu wapo wanaokuja kikwao. Wapo waliojibadili na kujifufua upya kama wa taifa jingine. Nahau inayotumika hapa ni “kujilipua”....
Wapo waliovuka bahari, wakakusanya fedha wakalipa nauli au wakaoa au kuolewa na wenyeji, au wana taaluma maalum za kisayansi na kisanii. Na ni wasanii ndiyo tuliokutana na Mheshimiwa Balozi Asha Rose Migiro Jumatano iliyopita.
Balozi huyu mpya (kama walivyokuwa wenzake wawili waliopita Balozi Maajar na Peter Kallaghe ) alisisitiza haja ya Watanzania kujisikia huru kutembelea Ubalozi wao.  
Balozi Migiro akiongea na wasanii aliowaalika ofini kwake Jumatano, Septemba 28.

Kati ya mengi yaliyozungumziwa ndani ya kikao hiki cha takribani saa mbili (ukiweka mazungumzo na picha zilizopigwa baada ya kikao), ni hilo la Watanzania kuogopana, Watanzania kutojishughulisha na Ubalozi. Balozi Migiro alisisitiza msimamo wa  serikali ya awamu ya tano kukiweka  kitengo cha sanaa mbele zaidi. Dk. Migiro alisema miaka iliyopita muziki, kuchora tamthiliya, fasihi, sarakasi, nk vilichanganywa ndani ya Wizara moja ya Utamaduni, Habari, Sanaa  na Michezo. Aliwahakikishia wasanii waliohudhuria kikao kuwa serikali ya Mheshimiwa John Magufuli inatambua nafasi ya sanaa si tu  kuitangaza Tanzania bali kuimarika kama tasnia muhimu ya mawasiliano.

Wasanii  tulikusanywa na mcheza sarakasi na mwanamuziki Fabrah Moses, mkazi wa London muda mrefu, aliyefungua dimba kwa kusisitiza haja ya kuwa na sauti moja na kujuana ili kuendelezana na kuijenga Tanzania ughaibuni.
Muungano huu utakaoitwa WASATU, Wasanii Tanzania Uingereza, ulichangamsha bongo kwa kujaribu kuangalia sababu gani hatuna muungano. Sababu kuu zilizotajwa ni pamoja na Tanzania kutojulikana nje.
“Wenzetu Kenya na Ethiopia wanayo riadha inayowatangaza. Hivyo ukizitaja nchi hizi kila mtu duniani anazifahamu,” alisema Fab Moses.
Jina la nchi hutegemea linavyojengwa. Tanzania haijulikani kabisa nje, kikao kilikubali. Unapolitaja jina la Tanzania hakuna mtu anayelitambua. Wengine hudhani ni Tasmania. Jingine ni amani. Kwa kuwa sisi hatuna tafrani muda mrefu basi hujiachia na kutojituma kama wenzetu, maana hakuna sababu (“comfort zone”). Ukizungumzia mlima Kilimanjaro hudhani uko Kenya...
Akifafanua hoja hiyo Mhe Balozi Migiro alisema ukweli ukiwa Kenya utaouona Mlima Kilimanjaro, hali kadhalika Tanzania. “Wenzetu hawadai mlima ni wao, ila wanachofanya ni kujitangaza tu. Wanayo bidii hiyo...”
Wasanii washiriki walikuwa, Saidi Kanda (muziki  asilia wa Tanzania), Msafiri (Mwana Bongo Fleva anayejulikana kama “Diouf Lewandoski”), Rama Sax (mpigaji wa bendi maarufu ya zamani ya Simba Wa Nyika), Hamida Mbaga (mtangazaji na muuza mavazi ya Kitanzania “All Things African”), Khadija Ismail (mwanatamthilia na mcheza ngoma aliyekuwa zamani  na Kibisa na Muungano), Neema Kitilya(Mapishi ya Kitanzania) na mwandishi wa makala haya. Tulikubaliana kuwa nafasi ya sanaa ni muhimu kuiendeleza Tanzania na kujenga uchumi ni muhimu.
Hili linaweza kufanyika ikiwa sisi wenyewe tunaungana na pia kwa msaaada wa Ubalozi ambao umeonesha kutujali. Afisa Msaidizi wa Balozi masuala ya Diaspora, Bw Allen Kuzilwa aliyehusika katika utayarishaji wa shughuli hii alisisitiza haja ya WASATU kuwa na malengo.
WASATU ilikubali kuwa kazi iliyoko mbele ni kubwa. Akifunga kikao Balozi Migiro alijumuisha yaliyoongelewa makuu ambayo ni kufahamiana na kuwasiliana, kuwepo umoja utakaowasiliana kati ya ubalozi na wasanii. Jingine ni wasanii kuwa washauri wa serikali, waendelezaji na wachangiaji wa maendeleo, maana mtu  kwao.

-Ilitumwa Mwananchi Jumapili , London, 29  Septemba  2016




No comments:

Post a Comment