Wabunge wa TANU mwaka 1959. Picha ya Facebook.
Moja ya mambo makubwa niliyojifunza
Ughaibuni ni namna wenzetu, (hasa weupe) wanavyothamini mambo YAO ya kale. Na
tunaposema “kuhifadhi” si tu watu maarufu au kadhia fulani fulani za
kiserikali.
Chukua vyakula. Zamani
Wazungu walikuwa wakioka mikate katika majiko ya mikaa, kama leo Afrika. Majiko
hayo yalikuwa aina ya tanuri. Kuna kipindi kilioneshwa mwaka jana kuhusu historia
ya mapishi. Wakachagua wapishi wanne wa kisasa. Wakawavalisha magwanda ya karne
ya kumi nane na kumi na tisa. Tukaoneshwa wakikanda unga na huku ule mvuke
na moshi vikiwaghasi. Wapishi wa “kizazi kipya” wakapata shida sana. Mikate
ilipokuwa tayari wakaionja. Wakasema mitamu sana.
Lakini ilikuwa pia na chumvi. Ambapo siku hizi
kuna uchaguzi Uzunguni wa chakula chenye chumvi au kisichokuwa nayo. Chumvi si
kitu kizuri sana kiafya hasa moyo. Moja ya mafunzo hapo ikawa kuwa leo tunaishi
kwa afya zaidi kuliko zamani. Wastani wa maisha ya wananchi karne hizo ulikuwa
miaka arobaini kama ilivyo nchi maskini.
Leo Uzunguni ni miaka 80.
Tuje kwenye umaarufu.
Kanisa la Westminster Abbey, London
Makaburi ya wafalme, wasanii,
na wagunduzi yamehifadhiwa. Mjini London kuna kanisa maarufu la Westminster
Abbey ambapo watu muhimu wamezikwa toka karne nyingi. Afrika bado tunasoma
vitabu vya mwanariwaya Charles Dickens,
mtunzi Mwingereza aliyeng’aara karne ya
19. Kaburi lake lipo Westminster Abbey. Nyumba
aliyoishi imehifadhiwa . Ukiitembelea shurti malipo.
Mwanafasalfa mashuhuri wa
Kirumi (Italia) aliyeishi karne ya 15 na 16 ni Nicollo Machiavelli.
Mwanafasalfa huyu aliyefariki 1527 anasomwa na takriban kila kiongozi duniani.
Kitabu chake mashuhuri “The Prince” ni kama msahafu kwa
wanasiasa:
“Ni
bora kuogopewa kuliko kupendwa; kama huyawezi yote mawili bora zingatia la kwanza.”
Ama: “ Ukitaka kujua akili au uerevu wa
mtawala chunguza wale waliomzunguka.”
Ingawa aliandika vitabu vingi,
The Prince (Mwana wa Mfalme) kinafahamika zaidi.
Kimehifadhiwa (pamoja na
chumba na hata meza) aliyoishi mjini Florence, Italia. Miaka mingapi?
Piga hesabu. Toka 1527!
Linganisha na sisi.
Karibuni tunaweza kuhesabu
mangapi tuliyoyaenzi?
Kaburi la Mtemi Mkwawa, pale Kalenga , Iringa.
Safi. Mti alionyongwa Mangi Meli wa Old Moshi, Uchagani, na wakoloni wa Kijerumani,
mwaka 1892. Safi. Mengine, je? Je ukitaka kusoma magazeti ya Uhuru na Mzalendo-
niliyokuwa nikiyaandika mwaka 1976?- Je, ukirudi nyuma zaidi hadi Raha Leo
aliloandikia Shaaban Robert miaka ya 1940 na 1950? Je kaburi la Shaaban Robert?
Je ni kweli kwamba ukitaka kusoma magazeti yetu ya nyuma yameishia mwaka 1982?
Je Radio Tanzania? Je ukitafuta sinema aliyoigiza mmoja wa waasisi wa taifa,
Rashid Mfaume Kawawa (Muhogo Mchungu) utaipata?
Lazima tujiulize maswali.
Maana sasa hivi kuna mgogoro na kero inayowasakama
watoto, wajukuu na familia ya aliyekuwa zamani Waziri katika awamu ya kwanza ya
Tanzania. Wangapi wanamkumbuka Lawi Nagwanda Sijaona?
Lawi Sijaona ...picha ya Mtandao wa Wazalendo.
Karibuni nilisoma ukuta wa
Facebook ambapo picha iliyopigwa mwaka 1959 Bunge la kikoloni, inawaonesha vijana wa enzi
hizo, Waafrika wa kwanza kwanza kuingia Bungeni.
Legco. Kirefu chake ni
“Legislative Assembly of Mainland Tanganyika.”
Lilianzishwa mwaka 1926 na
aliyekuwa Gavana wa Waingereza nchini, Bwana
Donald Cameron. Jumla wabunge 20. Picha hiyo ya 1959 inao Richard Wambura,
George Kahama, Amir Jamal, Paul Bomani, Rashid Kawawa na Lawi Sijaona. Vijana
hawa walikuwa miongoni mwa timu iliyokuwa sambamba na Mwalimu Nyerere
kugombania Uhuru wa Tanganyika. Baadaye tukashinda Uhuru. Wakafanywa Mawaziri.
Mishahara yao ililipwa hela ya malkia, yaani Paundi. Rais
alipata paundi 3,000 kwa mwaka na Mawaziri wake, £2,300.
Leo mtu akikupa paundi 3,000
ni shilingi milioni 8 na nusu. Ndiyo ni nyingi kwa mtu wa kawaida. Lakini enzi
hizo ilikuwa nadra sana kwa mtu kutafuta
uongozi wa kisiasa ili kuiba fedha au kufisadi. Walikuwepo “kupe” (neno Mwalimu Nyerere alilotumia kwa
“mafisadi” ) lakini ukweli hakikuwepo kitu cha kuiba. Nchi ilikuwa bado inaanza
kutembea.
Sikiliza mwandishi wa
Facebook:“Lawi Nang'wanda Sijaona ni mmoja wa wapigania uhuru wa Tanganyika,
akifanya kazi kubwa ya kuasisi vyama vya siasa vya ukombozi, tangu TAA, TANU na
hatimaye CCM. Alikuwa kiongozi na mzalendo wa mfano wa aina yake, Akifanya
mambo mengi makubwa na ya kukumbukwa....Hakuwa "Fisadi", "Mwizi"
wala "Mla Rushwa", alikuwa mwadilifu na mtu aliyelinda kwa nguvu
kubwa Rasilimali za Nchi hii. Kumbe, mwisho wake akafa, akazikwa na mema yote.
Akasahaulika!.”
Hiki ni kimoja cha visa vingi.
Tumesikia baadhi ya viongozi kuuawa kutokana
na kujaribu kutekeleza siasa za nchi. Mathalan Dk Wilfred Kleruu aliyepigwa
risasi na mkulima wa Iringa mwaka 1972.
Baadaye, Saidi Mwamwindi alinyongwa. Uzuri
wa kisa hiki ni watoto wawili wa marehemu ( Eva Kleruu na Amani Mwamindi – Meya
wa Iringa) kukutana mwaka juzi na
kufanya maridhiano – yaani kusameheana.
Hii inakumbusha pia mtoto wa
Nduli Idi Amin na Mwalimu Nyerere ambao wamekuwa wakiwasiliana miaka mingi
kufuta tofauti za baba zao.
Haya ni machache ya historia
yetu.
Lakini je mmesikia barua
iliyoandikwa na mtoto wa Waziri huyo wa zamani Lawi Nagwanda Sijaona , mwezi
jana kumtaka Mheshimiwa Rais John Magufuli ajaribu kusuluhisha jambo
linaloikera familia yake?
Barua inazungumzia kisa cha
Mwenge mwaka 1998 maeneo ya Newala, Mtwara. Mheshimiwa Waziri mstaafu Sijaona enzi
hizo (kwa mapenzi yake ya taifa) aliazima jenereta la umeme kusaidia shughuli za kukimbiza mwenge. Hadi alipofariki, 2005- barua ya mwanae inadai-mashine
haikuonekana. Barua inadai :
“Jenereta ilipotea ingali mikononi mwa Serekali na
shauri hilo kufikishwa Mahakamani kama inavyosomeka hati ya hukumu,kesi ya
jinai namba 322/1999 na inaeleza thamani yake kwa makadirio ya shs 1,500,000 na
kwamba mmiliki wake ni Mzee Lawi
Nangwana Sijaona.”
Barua inaendelea kwamba hadi
leo, viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa awamo ya nne walielezwa mgogoro.
Uamuzi wa kuandika barua ya wazi kwa Rais Magufuli unasisitiza kumbukumbu ya
mzee huyo kutothaminiwa, anadai mwanae.
Bila shaka wapo wananchi wengi waliofanya mema na ya maana nchini ambao hawakumbukwi. Marehemu Sijaona ni mmoja wa wanaotukumbusha haja ya kuwaiga wenzetu wanavyoweka heshima za mababu na mabibi zetu kwa karne nyingi.
Bila shaka wapo wananchi wengi waliofanya mema na ya maana nchini ambao hawakumbukwi. Marehemu Sijaona ni mmoja wa wanaotukumbusha haja ya kuwaiga wenzetu wanavyoweka heshima za mababu na mabibi zetu kwa karne nyingi.
Habari zaidi wasiliana na Adam
Sijaona simu 06581-45681 au 0782704208.
No comments:
Post a Comment