Tiba na afya za dunia yetu zimegawanyika sehemu mbili
kuu.
Magharibi ni
uganga wa Kizungu unaotumia sayansi iliyofikia kilele karne ya 19 na 20. Moja
ya nguzo zake kuu ni kutibu kwa kunyamazisha- kupitia sindano, dawa na
upasuaji. Tiba ya Kizungu ndiyo inayotawala dunia yetu na ndiyo mara nyingi
Wabongo wanaojiweza wakiugua siku hizi husafrishwa nje kutibiwa.
Tiba za mashariki zinaongozwa na ustaarabu wa Kihindi na
Kichina. Wahindi hutumia mwenendo uitwao Ayurveda. Tiba hii yenye zaidi ya
miaka elfu mbili huangalia mwili mzima ukoje kabla ya kuushughulikia. Wachina
wanao pia mtindo huo huo, unaotazama mtiririko wa nguvu mwilini badala ya
dosari. Utaratibu wa Kichina na Kihindi kijumla hautibu tatizo moja kama Wakizungu. Kwa wazungu mathalani ukiumwa kichwa
utapewa dawa ya kuyaondoa maumivu hayo.
Kwa Ayuverda na
mtindo wa Wachina huchunguza mahusiano ya mwili mzima yakoje badala ya kitu
kimoja. Wachina hugawa mwili kufuatana na sheria tano kuu zinazofuata maumbile
yaani mti (mbao), maji, chuma, moto, ardhi au dunia. Utaratibu huu hutumia tiba ya sindano
(Accupuncture) ambazo husisimua umeme mwilini. Wahindi na Wachina wanaamini
miili yetu ni sehemu ya sayari za dunia na ina mitiririko ya umeme isiyohitaji
sana dawa za nje kuugangua mwili.
Tofauti ya matibabu na namna ya kutibu kati ya Magharibi
na Mashariki haikuwepo zamani. Wazungu walioanisha unajimu, utabiri, dawa asilia na
mazingira (maumbile) kukagua na kugangua. Utaratibu huo ulifutwa kutokana na
kukua mfumo wa kibepari na dini (Ukristo) vilivyotaka tiba za haraka na kugeuza
uganga kuwa wa mashindano na malipo.
Je tofauti hii huonekanaje?
Ukiingia hospitali yeyote ya kisasa (Kizungu) mganga anapokuona hujali zaidi
kuondoa haraka adha inayokukabili. Mfano mzuri ni huko kuumwa na kichwa.
Atajaribu kutafuta ufumbuzi wa kuondoa maumivu, hususan kwa vidonge.
Linganisha na tiba za Ayuverda au Kichina ambapo
uchunguzi huangalia je unalalaje? Ndoto zako zikoje? Badala ya kupima mapafu
ataangalia ncha ya ulimi. Je ulimi mwekundu nchani? Kama ulimi mwekundu
atakuuliza je vipi unajisikiaje? Una hamaki za ghafla ghafla? Mbali na hayo tiba hii itaangalia harufu ya mwili wako,
ngozi, nk.
Tiba zote mbili hukagua pia mapigo ya moyo kutaka kujua
mtiririko wa damu ukoje. Ila tofauti iko katika tiba, Mara nyingi unapokwenda
kwa Mchina atakupa dawa ya kutibu mtiririko wa nguvu na umeme mwilini.
Tiba hizi zenye mitazamo miwili tofauti zimeanza kuoanishwa nchi zinazoendelea. Wapo waganga wa
Kizungu walio tayari kukubali baadhi ya tiba za Mashariki, mathalan Accupucture
(tiba ya sindano), lakini si wote. Baadhi ya hospitali za Ulaya zimefungua
idara zinazokubali tiba hizi za sindano na pia kuafiki usingaji kwa
wagonjwa wa saratani na maradhi mengine
makali.
Kati ya tatizo kubwa la tiba za Kizungu ni madhara ya
dawa kali zinazotumika kutibu maradhi makubwa makubwa. Madhara haya (yanayoitwa
“side effects” kitaaluma), yameanza kuongezeka kutokana na dawa za maabara
zisizojali sana hatima ya mwili. Hii ni kutokana na lengo la tiba za Magharibi
ambazo ni kuondoa tu tatizo moja kuu kinyume cha athari- jumla. Uganga wa
mashariki humwangalia mtu mzima badala ya kipengele tu cha maradhi yake.
Tuchukue mfano wa shinikizo la moyo au presha.
Kambi nzima ya uponyaji
ulimwenguni inakubali kuwa maradhi ya moyo husababishwa na mambo makuu manne :
unene au kitambi, maisha ya haraka haraka na tafrani, mshtuko wa ghafla , mirathi au kurithi kifamilia.
Kinachotofautiana ni tiba.
Mara nyingi Uzunguni hutoa dawa za kupunguza shinikizo
hilo.
Kwa watu wa mashariki pamoja na tiba mbalimbali za dawa
za miti na mimea au Accupunture, huhimiza usingaji, mapumziko na hata kufanya
shughuli zinazotulizana moyo ( na roho); kupiga muziki, kuchora , kufanya kazi
za bustani ...pole pole Wazungu wameanza kupokea fikra hizi.
Yamkini dunia ya leo inaanza kuoanisha tiba hizi mbili
zinazokinzana lakini ambazo zamani zilikaribiana.
Kwetu Afrika pia tunazo tiba mbalimbali.
Tiba zetu zimegawanyika sehemu mbili: mazingaumbwe au
uchawi; na miti shamba au mimea na mali
asili. Ingawa kuna utajiri mkubwa wa kuganga na kugangua bado serikali zetu
hazijatambua umuhimu wa tiba asilia. Bado tasnia hii ni ndogo na tunategemea
sana dawa na matibabu ya Kizungu. Egemeo hili kwa Wazungu limezidi kiasi
ambacho maradhi makubwa makubwa yanatuua haraka sana.
Mbali na tiba hizo bado sisi si wepesi kukinga. Kinga
maradhi inategemea sana kufahamu mwili ukoje na nini tunapaswa kufanya
kuudhibiti.
Kati ya mambo
tunayopaswa kufahamu ni viungo vyetu. Wachina wanaamini kuwa tumbo ni kiungo
muhimu kuliko vyote. Fikra hii inatokana na kwamba kila siku tunakula milo
mitatu na vitu vingine vidogo vidogo. Kuweka huku vitu mwilini hutegemea sana
tumbo, ini, uwengo, figo na moyo kufanya kazi zake. Karibuni, figo, imekuwa tatizo la Waafrika. Kitakwimu, zamani figo ilikuwa tatizo la
wazee lakini leo watu wenye umri wa miaka thelathini hadi arobaini wana tatizo
la figo. Figo kazi yake ni kuchuja umaji maji mwilini.
Kwa kuwa siku hizi hatupiki vyakula asilia, kutokana na
maisha ya kukimbia kutafuta riziki, fedha na kazi, tunakula vyakula
visivyotengenezwa vizuri. Vyakula vyetu vina
ladha ya kuvutia lakini vinaharibu figo. Kwanini figo? Kwa vile figo
kazi yake ni kuchuja maji na masalia yake. Wiki hii mtandao umesambaza ilani
kuwaasa wazungumzaji wa Kiswahili kujali
zaidi figo. Kati ya tahadhari zilizotolewa ni kunywa maji ya uvuguvugu (Wachina
na Marasta husisitiza maji moto) badala ya baridi, kutokula vyakula vyenye
chumvi na pilipili nyingi , sukari (Watanzania tunapenda sana Soda na Cocacola
au chai yenye sukari nyingi), kutokunwya maji na kula chakula usiku sana. Nadhari
inazingatia kuwa kadri unavyokula sana usiku au kuweka ladha nyingi katika mlo
wako ndivyo unavyozipa figo zako mbili kazi na mizigo mizito. Unapokula usiku
sharti uhakikishe unakaa saa tatu kabla ya kulala. Matunzo ya figo yako ni
dhamana ya afya shauri bila chujio hilo uchafu huathiri viungo mbalimbali mwilini
mathalan kibofu, ngozi, damu nk.
-Ilichapishwa
No comments:
Post a Comment