Majuma matatu yaliyopita safu hii ilizungumzia tatizo la maradhi ya figo. Punde tu wasomaji
kadhaa waliniandikia kuulizia habari zaidi.
Takwimu za afya Ulaya zinasema figo huandama zaidi watu
weusi.
Ingawa bara lina kila aina ya virutubisho , mazao na hali
ya hewa safi, bado hatujijali kiafya.
Je maradhi ya figo yanaepukika? Na kuanzia, figo ziko
wapi na kazi yake ni nini?
Figo mbili ziko , juu ya nyonga, chini ya ubavu, mgongoni. Kawaida mabondia
wanapodundana, wakikaribiana, kila mmoja hujaribu kupiga figo. Kwanini figo
idundwe?
Figo na kibofu cha mkojo ni wachujaji maji machafu mwilini. Wachina huziiita figo hakimu mkuu.
Bila figo ni jangwa. Baada ya kula na
kunywa lazima amri itolewe kupeleka umaji maji na damu inayotakiwa mwilini
kutokana na vyakula na vinywaji. Visivyotakiwa hutimuliwa. Wanasayansi wanatueleza asilimia 75
ya mwili ni maji katika musuli na
minofu. Kiasi hutofautiana kati wanawake na wanaume.
Kazi ya kusafisha na kupiga deki hufikia kilele saa tisa
hadi moja jioni, kila siku. Ndiyo maana
wengi husikia uchovu au kutokuwa na nguvu saa hizo. Kazi kuu ya kutenga
hufanywa pia saa tisa za usiku hadi kumi na moja alfajiri.
Sasa kwanini matatizo ya figo yamezidi sana miaka hii
kwetu weusi ?
Kwanza tuzingatie
kuwa wanadamu hatufuati tena kanuni kiasilia. Zamani tulikuwa kama wanyama. Saa
ya kulala ni kila kiza kikiingia na kuamka mwangaza unapochungulia. Hilo “likafutwa”
na badala yake siku hizi tuna washa taa ili tuendelee kuangalia sinema na
kukesha.Ubundi...
Halafu ulaji.
Wazungu wana desturi ya kula mapema. Ukanda wa nchi za Scandinavia
mathalan hula chakula cha mwisho saa kumi na moja na kumbi mbili za jioni.
Ikishapita saa mbili za usiku, wenzetu hawali misosi mizito. Husema si vizuri
kwenda kitandani na tumbo lililojaa.
Ukitazama Waafrika wengi, hasa tunaioishi mijini siku
hizi, tuna tabia ya kula usiku sana. Hii ni kutokana na mbio za maisha na”
kutokuwa na muda.” Unatoka kazini hadi umalize shughul, upike , ule ni saa nne
za usiku. Mara baada ya kula usingizi huo tunajirusha vitandani.
Tatizo kubwa sana.
Mwanadamu unatakiwa ukae saa tatu nzima kabla ya kulala,
baada ya kula. Sababu kuu ni umeng’enywaji wa chakula. Ukila kisha ukaendelea
na shughuli ndogo ndogo hadi saa tatu zikipita halafu ndiyo ulale, unakuwa umeupa
mwili muda wa kufanya kazi yake, kiufanisi.
Pili, wakati
tumelala, tumbo huwa kazini. Sasa kama tumbo limejaa (kama umekula nne au tano), ukiwa umelala,
viungo havipumziki.
Juu ya hilo sasa, huku umeng’enywaji ukiendelea, hakimu
au mchujaji wa chakula kilicholiwa jana yake, kuondoa kinyesi na mikojo, ni
figo na kibofu. Haya yasipofanywa kwa
wakati wake huwa kazi ya ziada kwa viungo hivyo.
Ni kama mtu kupewa kazi moja ya kufanya halafu
ukaongezewa nyingine kabla ya kuimaliza. Hakuna ufanifu, ufanisi, au
uendelezwaji...
Tatizo la pili ni aina ya vyakula.
Zamani tulikula vyakula asilia. Mapishi yalizingatia uasilia
wake. Leo kutokana na “mbio za mapanya” wengi hatupiki. Tukiwa mitaani, tunakimbilia “chips” kwa nyama.
Mafuta yanayopikia mitaani huwa yameshatumika muda mrefu. NI kama sumu mwilini.
Ongezea sasa chumvi na ghasia nyingine za ladha. Suala la” ladha” ni janga
kubwa sana kwetu watu weusi. Sisi ( na
wenzetu wa Marekani ya Kusini , Karibi, na Asia) tunapenda sana chumvi,
pilipili, nk. Tunathamini ladha badala
ya virutubisho vya misosi. Mbali na chumvi, lazima tubwie vitu vingine wakati
tunakula. Kunywa huku unakula ni kazi kubwa kwa tumbo na figo. Wengi hukata kiu
wakila kwa chai, Cocacola, bia au soda. Hapa kuna mawili. Chumvi na sukari
pamoja ni unaa. Vikifika mwilini lazima vichambuliwe. Hiyo si kazi tu ya tumbo
(hydrocholoric acid kwa waliosomea kimia mashuleni), uwengu, na ini. Ni mtihani
kwa hakimu au mchujaji wa maji maji mwilini yaani figo. Ukitaka kunywa
chochote, kinywe saa moja au zaidi kabla au baada ya msosi. Si kunywa na
chakula. Na ni bora maji kuliko sukari sukari.
Sasa hapa tunamzungumzia mtu mwenye afya na mwili wa
kawaida. Ukiwa mnene au usiyefanya mazoezi ndiyo kabisa unajichongea. Ndiyo
maana tatizo la kibofu, figo, presha nk huwa kali zaidi kwa wanene au wana
vitambi. Hata hivyo haina maana kwamba usipokuwa mnene, weka sana chumvi nyingi
katika chakula chako.
Je matatizo ya figo huwaje?
Dalili ziko nyingi.
Uchovu usioeleweka, miguu na mikono kuvimba, pumzi za
shida, kujisikia ovyo ovyo (kichefu chefu) bila sababu maalum- mathalan kama si
mja mzito au uliyekunywa sana pombe jana. Kutapika tapika bila sababu. Pili, mkojo. Kuwa na damu katika mkojo.
Kutokojoa sawa sawa au kukojoa kojoa mara kwa mara. Kuwa na maumivu ukifanya
haja ndogo. Haja hiyo ndogo kuwa na harufu au rangi isiyo ya kawaida, kijani,
kahawia au mapovu mapovu, utadhani
unarusha sabuni ya Omo.
Jingine ni
maumivu. Maumivu sehemu za siri hasa
korodani kwa wanaume. Maumivu kinenani au tumboni. Maumivu nyongani, chini ya
mbavu , nyuma, zilipo figo zenyewe. Kwa watoto huwa hawana nguvu , hukereka
ovyo au wana mkojo wenye harufu mbaya sana.
Kupima ni vyema kwenda kwa mganga kuangaliwa mkojo na
damu. Kati ya tiba asilia ni magadi na kula vyakula vyenye virutubisho.
Mathalan vitunguu, vitunguu saumu,matunda hasa yale yenye mbegu mbegu ndogo
ndani (Berries), matufaha,kabichi, koliflawa, samaki na kutumia mafuta ya
mzaituni kupikia au kwenye Salad.
Salad na Mwafrika. Mmh.
Ni muhimu sana
kula Salad na chakula. Salad hii iwe ya mboga mbichi za majani : nyanya, tango,
nazi, parachichi, mbegu mbegu mbichi (korosho, ulozi, karanga) nk. Watu weusi
tuna tabia ya kuweka chumvi hadi katika Salad yaani mboga za majani. Tumezidi.
Hili linachangia sana kuumiza figo.
Juu ya yote haya tunapofanya mazoezi ya viungo na kulala
muda unaotakiwa wa saa 7-8 kwa siku, tunazipunguzia figo, mzigo.
Ilichapishwa Mwananchi Jumapili 9, Oktoba 2016.
No comments:
Post a Comment