Saturday, 12 November 2016

KISWAHILI KINAVYOPARAGANYA HERUFI “R” NA “ L”- 2



Tatizo la Kiswahili kuanza kudidimia siku hizi linatokana na sababu nyingi. Juu kabisa ni Watanzania  kutojielewa kinafsiya. Ndiyo tunajijua sisi Watanzania. Tunaishi wapi kijiografia. Lakini sidhani tunaelewa vizuri nafasi yetu kitamaduni hapa duniani. Matumizi yetu ya lugha yanaonesha “kuchanganyikiwa” huku kunakodhihirisha ulimbukeni fulani.
Miye Mtanzania siogopi kujitoboa jicho.
Chukua mfano wa mitandao jamii. Mtanzania atatoa maoni fulani tuseme ukuta wa Facebook.  Labda jambo zuri limeandikwa kwa  Kiswahili. Kujionesha ataandika maoni yake  Kiingereza au Kiswanglish. Au jambo limeandikwa Kiingereza, yeye ataweka maoni Kiswahili.


  
Hii haitokei tu Facebook, pia simu za mkononi, Instagram, Twitter, WhatsUp na kadhalika.  Mtanzania bado haelewi kuwa kila lugha ina mahali na wakati wake. Kama unazungumza na Mzungu( au Mwafrika wa nchi nyingine )asiyejua Kiswahili- tumia  Kiingereza, Kifaransa nk.  Pengine unazungumza na mtu wa kabila lako, ah basi chapeni,  kikwenu. Zungumza  Kiswahili  na Mtanzania. Una haja gani ya Kiingereza? Huenda yakawa mazingira ya kikazi, kiofisi, kielimu au kiserikali ambapo Kiingereza kinatakiwa, basi chapa Kimombo.  Kiingereza,  ni lugha tu.
 Haina maana ukijua, kuandika au kuzungumza Kimombo wewe mtu wa juu au kipekee. Lugha ni sufuria ya mawasiliano. Tumechanganyikiwa kiasi ambacho Rais Magufuli alipohutubia mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwezi Septemba, kuna mtu aliandika makala kumkosoa “eti hajui Kiingereza.”

 Watanzania kadhaa mitandaoni wakazusha kuwa Rais wetu alinunua tu udokta wake ndiyo maana “hajui” Kiingereza. Unaona tunavyojiparaganya?
 Kiswahili ni sura na wajihi wa Mtanzania. Kama kilivyo Kimandarin au KiCantonese kwa Mchina , Kirusi kwa Mrusi, Kiarabu kwa Mwarabu nk. Sasa je wananchi wenzangu hatujawahi kumwona Rais Vladimir Putin  akiongea Kirusi na mkalimani anapohutubia wageni? Haina maana hafahamu Kiingereza. Zamani Putin alikuwa askari usalama au shushushu wa KGB.  Alifanya kazi zake nchi nyingi.  Angesafirije bila Kiingereza?
Rais wa zamani Cuba,  Fidel Castro alipoanza uongozi alikuwa na tabia ya kuchapa Kiingereza. Baadaye hakukigusa. Alizungumza Kispanyola na mkalimani. Anachofanya Rais wetu Magufuli ni sambamba na viongozi wa nchi nyingine  zinazojitambua kinafsiya. Kila mmoja huongea kikwao kuonesha wajihi (“identity”),  kitaifa.

Kitaaluma, Rais John Magufuli ni dokta na ni msomi.  Hakufikia hapo bila Kiingereza...
Kujielewa huanzia ulikozaliwa; kisha kabila au mbari. Kutoka hapo tunaingia utaifa na silaha ya mawasiliano yaani Kiswahili. Ukisafiri sasa nje ya Tanzania, kuwasiliana na dunia ndipo unapotumia Kiingereza. Watanzania tunatakiwa tujue Kiingereza fasaha na sio Kiswanglish. Wenzetu  Kenya na- hasa Waganda- hutucheka eti hatuwezi kuzungumza Kiingereza sawasawa. Na hili nimeliandika mara nyingi siku za nyuma. Moja ya sababu kuu inayochangia Watanzania- hasa wa kizazi kilichozaliwa baada ya mwaka 1980- kutokimanya  Kiingereza sawasawa ni Kiswanglish. Kiswanglish ni ubabaishaji. Ubabaishaji ( au “kubangaiza” wanavyosema Kenya) - aina ya uvivu wa kifikra.  Kutotaka kufanya kazi kiakili.
Tuko tayari kupata fedha kwa kudanganya danganya; kununua vyeti vya kitaaluma badala ya kuvisomea. Tunapenda rahisi rahisi.
Lakini tujikumbushe kuwa utajiri, uchumi, fedha na fursa zote huanzia kwenye ulicho nacho. Kwanini Wajapani  wanaongoza kiteknolojia ? Walitumia na kuanzia kwao.  Hawakuziita mashine au biashara  majina ya kigeni. Walitumia  Suzuki, Toyota, Honda, Mitsubishi, Nissan, Yamaha nk,... sio majina ya Kiingereza au Kijerumani. Ni ya Kijapani. Tujiulize kwanini?
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa ulitangaza lugha kumi zinazokua kasi duniani na kuorodhesha Kiswahili nafasi ya saba!
Maana yake nini?
Fursa. Biashara. Uwezekano. Maslahi. Maendeleo.
Tunaolilia ajira.
Tuzingatie.
Kiswahili ni ajira kubwa kwetu. Rasilmani asilia. Ukikaa chini Mtanzania ukajichunguza sana, je unawezaje kuwasiliana vizuri zaidi na vyepesi kwa lugha gani kama si Kiswahili? Sasa kama unayo silaha hii kwanini, mosi usiijue kwa undani zaidi na pili ukaitumia kunyoosha mkono kuchuma maembe na mibuyu juu ya miti?
Angalia Kiswahili kinavyoweza kuwa uchumi wako Mtanzania. Kwanza kukifundisha. Ijue. Itangaze. Itumie. Wenzetu Kenya wameligundua hilo miongo mingi. Nyimbo maarufu za Kiswahili duniani hazitoki Tanzania. Zimerekodiwa na Wakenya. Malaika, Jambo Jambo- Hakuna Matata...
Kila mwanamuziki wa Afrika Mashariki huzipiga. Ukiwa ughaibuni wageni watakuomba.
 “Can you play Malaika please?”
 Sasa, je, kuna chambo kinachosaidia kutangaza  lugha yako kama muziki? Wasikilize Wakongo wanavyopendwa shauri ya muziki wao wa Kilingala.  Mwafrika yupi asiyependa au kununua Ndombolo? Fursa kwa Wakongo hiyo.
Kilichochangia lugha hii kuhusudiwa ni Kilingala. Wasenegali hali kadhalika. Youssou Ndour ni mashuhuri na tajiri , tena huimba Kiwolof ingawa anachapa Kifaransa bila noma. Albino mashuhuri , Salif Keita vile vile. Hu ghani kikwao cha Mali. Wala hatuelewi wanaimba nini – lakini tunanunua miziki yao.  Hawa ni magwiji. Zamani Fela Kuti aliimba Kiyoruba na Kiingereza. Je kuna lugha tamu kimuziki kama Kiyoruba? Na Kiswahili kinapendeza sana masikioni. Kila nikiimba Kiswahili wananchi Ughaibuni husisitiza wanavyokipenda.
(“Swahili sounds so musical...”)
Fursa hizo. Kuuza kazi za muziki, kanga, mavazi,  vitabu vya  Kiswahili.
Watanzania tusikubali kuchakachua.
 Tukiwa ughaibuni hatuongei kikwetu na watoto.  Mtoto atajuaje lugha kama wewe mzazi huongei naye lugha hiyo? Watanzania wangapi tunaoabisha tunapowatembelea wenzetu na kuwakuta wanao wanashindwa kusema Shikamoo, huku Ulaya na Marekani? Mtanzania ataanza na “Hello!” Na lafidhi mbovu akizungumza na watoto wa Mtanzania mwenzake.
Eti hudai  hatutaki mwanae achanganyikiwe. Wanasaikolojia wa lugha wamekiri ni rahisi zaidi  kujifunza lugha mseto ukiwa bado mtoto.
Wiki jana tulitaja uzembe unaoenea  kuchanganya  herufi R na L. Jingine baya zaidi ni uharibifu wa silabi, mathalani H.
“abali” badala ya “habari”.....

 Matatizo hayapungui. Yanaendelezwa na  wanahabari, waalimu, wasanii na baadhi ya  wanasiasa viongozi.
Wachapishaji vitabu nao badala ya kuuza kazi za fasihi wanajali tu vitabu vya kufundisha mashuleni. Ndiyo maana wenzetu Kenya wametupiku kabisa biashara hii. Waandishi nguli  Adam Shafi na Profesa Said Ahmed Mohammed wanakimbilia kuchapisha vitabu Kenya. Shauri wachapishaji vitabu nao hawana msimamo imara ukiacha Mkuki Na Nyota anaeelewa nafasi ya vitabu kuendeleza lugha na utamaduni kitaifa.

-Ilitolewa sehemu mbili na Mwananchi Jumapili, Novemba 2016




No comments:

Post a Comment