Shangwe
zilizoenea Ulaya nzima sasa hivi ni mashindano ya soka, Brazil.
Ila wasiwasi uliowashika wanausalama wanaojua
mikunjo kunjo ya shuka na kanzu za ulimwengu wetu ni tafrani kali zinazoendelea
Syria na Iraq. Wasiwasi wa mashushushu na
wanasiasa Majuu ni hatari zitakazoenezwa na migogoro hii.
Uingereza mathalan imedai vijana 400 wazawa hapa, wanapigana Syria. Wakimaliza watarejea
na kusambaza ugaidi ulimwenguni. Vyombo kadhaa vya habari Uingereza vimeonya
jinsi mamia ya vijana wake wanavyomenyana pia Iraq, Libya, Afghanmistani, Kenya na Somali alipo mwanamke wa Kizungu anayetafutwa kuliko
fedha.
Samantha, mmoja wa wanae na mumewe gaidi aliyehusika na mauaji ya London 2005. Picha toka gazeti la Mirror
Samantha Lewthwaite, alikuwa mke wa mmoja wa magaidi wanne waliolipua mabomu na kuua
watu 51 mjini London mwaka 2005. Inadaiwa Septemba 2013, magaidi wa Al
Shabaab (walipoua 67 na kujeruhi 175), Nairobi, Mwingereza huyu mwenye watoto wanne alihusika. Inadaiwa keshasilimu (anaitwa Sherafiya) na
kuolewa na mmoja wa viongozi wakubwa wa Al Shabaab, Hassan Maalim Ibrahim. Al Shaabab maanake ni “vijana” kwa Kiarabu,
ilhali Boko Haram ni Elimu ya Kizungu ni Haram.
Mauaji ya makundi haya hufanywa kwa madai eti yanatukuza Uislamu.