Jumapili iliyopita tuliona namna
mwanamuziki Fela Kuti alivyoonya kuhusu imani
za kigeni zilivyochangia kupotosha utamaduni wa Mwafrika.
Akasisitiza : “Ukristo na Uislamu si dini zetu...Wakristo wana fikra na tabia za Waingereza na Wamarekani, ilhali Waislamu wana tabia za Waarabu.”
Msikilize mwenyewe akijieleza kinaga naga
Jadi mbalimbali duniani zilijengwa kufuatana na mazingira na hali ya hewa. Dini zilitumia mvua, jua, radi, miti, wanyama nk, kuabudu na kutambika. Dini mbili kuu za Waafrika leo zimetokana na utamaduni wa Mashariki ya Kati na Wazungu.
<--more--!>
Akasisitiza : “Ukristo na Uislamu si dini zetu...Wakristo wana fikra na tabia za Waingereza na Wamarekani, ilhali Waislamu wana tabia za Waarabu.”
Msikilize mwenyewe akijieleza kinaga naga
Jadi mbalimbali duniani zilijengwa kufuatana na mazingira na hali ya hewa. Dini zilitumia mvua, jua, radi, miti, wanyama nk, kuabudu na kutambika. Dini mbili kuu za Waafrika leo zimetokana na utamaduni wa Mashariki ya Kati na Wazungu.
<--more--!>
Ona mathalan sikukuu muhimu
ya Krismasi inayotueleza kuwa Bwana Yesu Kristo alizaliwa Desemba. Mnajimu na
mwanasayansi, Mchungaji Don Jacobs anasema katika kitabu chake “Astrology’s Pew
in Church” alichoandika baada ya utafiti wa muda mrefu kwamba Bwana Yesu alizaliwa
Machi mosi.
Hoja hii imekubalika
(Uzunguni) miaka mingi kwamba Bwana Yesu hakuzaliwa Desemba. Sababu ya kuigeuza
tarehe ya kuzaliwa kwake inatokana na dini ya Wazungu iliyoitwa Pagan (sisi
huita Upagani kutokuwa na dini lakini Mapagani waliabudu maumbile kufuatana na hali ya hewa) ambapo
matambiko muhimu ya kula na sherehe hufanywa tarehe 21 Desemba wakati jua linapokua kaskazi ya Ikweta msimu wa baridi (“Winter Solstice”).
Kinachosemwa na Wazungu ni kwamba lengo
la kuiweka Krismasi tarehe hizi ilifuatana
na shangwe za sherehe hii. Huu ni mfano wa namna dini inavyofuata desturi za
jamii. Na ndiyo sababu Mnigeria, Fela Kuti akauliza je pana uhusiano gani kitamaduni baina ya dini hizi na sisi Waafrika?
Misingi ya Uislamu ni huko
huko Mashariki ya kati. Majina ya manabii wake ni yale yale ya Wakristo, sema
kutokana na tofauti kati ya Waarabu na binam zao Wayahudi wakakinzana. Rejea
: Issa kwa Waislamu ni Yesu kwa Wakristo,
Yusufu ni Joseph, Ibrahim ni Abraham, Mariam ni Miriam, Hawa ni Eve au Eva,
Musa ni Moses, nk.
Mwaka 2005 mkutano mkubwa
ulifanywa Mashariki ya kati kutathmini mustakabal wa Waislamu. Ulihudhuriwa na wataalamu
200 wa Kiislamu toka nchi 50 ukasimamiwa na Sheikh Iz Al Din Al Tamimi na
mfalme Abdullah wa Jordan.
Washiriki walihimiza misingi ya Uislamu yaani “huruma,
heshima, uvumilivu, kusujudu na uhuru wa kidini.”
Walikumbusha nguzo kuu tatu zenye “madhahab” (madhehebu) manane : Hanafi,
Maliki, Shafii, Hanbali, Jafari, Zaidi, Ibadi na Zahiri; zinazowakataza Waislamu kuwasuta wasiofuata
dini hii kwa kutamka Takfir. Neno “takfir” lililotokana na “kafir” (kufuru au kutokuwa na heshima) huwasema
wakosaji. Ila Uislamu unasema wanaoruhusiwa kugombesha ni “walema au walama”
tunaowaita maalim na mufti (au waalimu) kwa Kiswahili. Hawa waliruhusiwa katika
sheria ya Kiislamu kuwataja au kuwashtaki makafir. Tatu, mkutano ulishutumu vurugu
na mauaji yanayotumika kwa jina la dini hiyo. Hivyo basi ikiwa misingi ya dini
inatokana na amani, je adui nani hasa?
Tukichunguza jamii zinazovurugwa
na magaidi sasa hivi Afrika tunaona
mizizi iko katika uchumi na siasa. Kufuatana na habari zilizotolewa na shirika
la kuondoa Umaskini duniani, kati ya 1975 hadi 2000, Afrika ni bara pekee
lililozama (katika njaa, umaskini na ukosefu wa elimu) licha ya Uhuru wa nusu
karne.
Tuanze na Somalia, yenye Al Shabaab. Karibuni
bei ya vitu imepanda kwa asilimia 300. Toka mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa
Rais Siad Barre mwaka 1991 utawala ni wa vikundi vichache vya makabila na familia
zenye mabavu. Kijiografia, Somalia si nchi yenye rutuba; riziki hutegemea ufugaji.
Barabara na usafiri ni dhaifu na
kufuatana na ripoti iliyotolewa karibuni na wataalamu mbalimbali wa kimataifa,
Somalia inahitaji miaka 20 kujijenga sawasawa. Hilo haliwezekani bila amani.
Boko Haram (“ elimu ya
Kizungu ni dhambi”) ilianzishwa mwaka 2001 na Mohammed Yusuf kupinga sayansi na
sheria zilizopo Nigeria.
Karibuni Nigeria
imeorodheshwa kuwa nchi ya saba duniani yenye mkusanyiko mikubwa ya makabila, dini
na utajiri wa mafuta. Ila utajiri huu unawanufaisha wachache, waasi wanaamka
wakitumia dini kama ngao na sababu.
Hali hii imestawi haraka
mwaka huu Mali.
Magaidi wa Mali, yaani Ansar
Dine (Dine inatokana na “dini” kwa
Kiarabu) wanajitengenezea fedha kwa kuwakamata wageni au matajiri kununua silaha. Lengo la Ansar Dine
si tu kujenga Sharia, bali kutawala jamii.
Iyad Ag Ghaly ( mpinzani wa
serikali miaka 30 sasa )anayeongoza “Ansar Dine” anadai amechukua theluthi
mbili ya nchi baada ya mapinduzi dhidi ya serikali iliyoshinda uchaguzi kihalali.
Sharia, itikeli na tabia zinazofanana na zile za Mataliban wa Afghanistan zimepiga marufuku
TV, mpira, pombe, kuvuta sigara; na huwakata mikono au kuwapiga
mawe wahalifu. Njaa, ukosefu wa umeme na
mafuta vimesababisha wakimbizi laki mbili.
Karibuni “Ansar Dine”
imevuruga sehemu za tambiko za kijadi zinazoheshimiwa na wananchi wa Mali kwa
karne nyingi. Waislamu wengi hawataki kuunga mkono Ansar Dine; ila vijana wasiokuwa na elimu au kazi ndiyo wanachama.
Kisa? Kama huna mustakabal au matumaini katika
maisha utafanya nini? Ansar Dine ina “wapiganaji” toka nchi za kigeni (mfano
Chad na Mauritania) ambao wameitwa “majihadi wa kijambazi” na vyombo vya
habari.
Si mwananchi wa kawaida bali
watengeneza mabomu na silaha. Kadri makundi haya yanavyoendelea kujijenga
ndivyo makampuni ya silaha Uzunguni yanavyotajirika. Mbali na silaha
zinazouziwa magaidi na wanajeshi wanaobaka wanawake Kongo, Sudan na Somalia yapo makampuni makubwa makubwa yanayoshirikiana
na serikali Afrika.
Dini si chanzo bali matokeo.
Na haya ndiyo yanayochanua Bongo.
Wananchi wamechoshwa na maneno matupu ya wanasiasa. Mauaji ya polisi, uchomaji makanisa ( Dar na
Zanzibar) kuota mabawa chama cha Uamsho, Unguja ni dalili za mvua ya radi.
Ingawa Uamsho haina nguvu kama Boko Haramu, Ansar Dine na Al Shabab, kuwepo
kwake kunadhihirisha kuenea kwa waasi wanaosingizia dini Afrika.
Miaka hamsini iliyopita
majeshi yalikuwa na desturi yakupindua
serikali kujaribu kurejesha hali njema Afrika. Leo wanadini wanachukua
nafasi hiyo hiyo. Lengo la dini ni amani
ya kiroho na ya majeshi ni kulinda taifa. Serikali si idara yao. Paka asipokuwepo Panya hutawala. Wanasiasa na
viongozi wanaposhindwa kazi wanadini au
wanajeshi hukamata pale matumaini
yalipokosekana. Hali hii inathibisha namna Afrika inavyohitaji uongozi na mabadiliko ya
kweli.
London: 6 Novemba, 2012- Ilikataliwa kuchapwa...
No comments:
Post a Comment