Sijui wasomaji wangapi tunamkumbuka
mwanamuziki mashuhuri wa Nigeria, Fela Anikulapo Kuti aliyefariki 1997 akiwa na
umri wa miaka 59? Fela alikuwa binam wa
mwandishi maarufu, Wole Soyinka (pichani) aliyeshinda tuzo la fasihi (Nobel) duniani 1986.
Pamoja na kipaji cha muziki
(utunzi wenye ujumbe mzito, kuimba, kupiga saxafoni, ngoma na piano) Fela hakua
mwoga. Alikuwa mmoja wa wanamuziki
wachache Afrika ambaye hakusita si tu kuimba ukweli, bali tayari kupambana na
serikali ya nchi yake na kukemea ufisadi na rushwa vilivyoinyea(na bado
vinaendelea) Nigeria.
Serikali na majeshi
yalimchukia na kumwandama kiasi ambacho mwaka 1977 askari elfu moja walivamia
makao makuu ya bendi yake -Afrika 70-
wakampiga yeye, wake zake na wanabendi halafu wakaharibu kila kitu. Ndani ya vurugu hiyo
walimtupa mamake Fela (Funmilayo) dirishani – baadaye akafia hospitalini. Fela
aliudhika sana akatunga nyimbo mbili
kuishutumu serikali na askari wadhalimu (“Coffin for Head of State” na “Unknown
Soldier”) na kulipeleka jeneza la mama mzazi makao makuu ya jeshi yaliyoongozwa
na Jenerali Olusegun Obasanjo(aliyekuja kuwa Rais). Licha ya kipigo, baadaye alitafutiwa vijisababu akafungwa jela
miaka mitano kwa msimamo usiokua na woga wala unafiki.
Tuangalie dhana ya unafiki.
Fela Kuti alioa wake 27 (aliowaita
malkia ), mwaka 1977; waliimba na
kucheza naye jukwaani.
<--more--!>
Akijitetea katika moja ya mahojiano yake Majuu alisema.
<--more--!>
Akijitetea katika moja ya mahojiano yake Majuu alisema.
“Utamkuta mtu kaoa. Wakati
mkewe yuko usingizini atatoka nje na kulala na wengine. Ni bora akiwaleta hawa
wanawake wote nyumbani badala ya kuhangaika ovyo mitaani.”
Kitabu cha maisha yake
kilichoandikwa na Carlos Moore (“Fela- this bitch of a life”, 1982) kinawahoji wake zake 15 wanaofafanua kwanini walimhusudu.
Omolora Shosanya, mathalan, anakiri
alimpenda Fela kwa akili, ujasiri, mtazamo wake na kuwa mpenzi mzuri.
Nigeria inayo makabila mengi lakini matatu
muhimu ni Waigbo, Wahausa na Wayoruba. Fela alihimiza sana misingi ya Wayoruba
(kabila lake) kwa kuvaa, kuimba, kupamba
jukwaa, kucheza na kutambika mara kwa mara. Alisisitiza hilo kwa kubadili jina
la Fela Ransom Kuti kuwa Fela Anikulapo Kuti. Kugeuza jina kulihimiza umuhimu wa desturi za Waafrika.
Anasema katika sinema iliyotengenezwa
mwaka 1982 kwamba leo Waafrika hawajui wanakotoka wala wanakokwenda. “Mwafrika anamwiga Mzungu na katika miaka hii ameshindwa
kutunga lolote jipya kutokana na kuiga iga na kutojijua.”
Tunaona aibu kufuata desturi
zetu, anasisitiza. Analaumu kuwepo kwa “dini za kigeni” zinazotufanya tusijijue
au kujipenda wenyewe.
Anasisitiza : “Ukristo na Uislamu si dini zetu. Na tunafahamu sababu gani Ukristo na Uislamu
vimeenea bara zima la Afrika. Ni kuwadhulumu watu. Wakristo wana fikra na tabia za Waingereza na Wamerakani ilhali Waislamu
wana tabia za Waarabu. Lengo ni kutuondoa Waafrika toka mizizi na fikra zetu tu. Waafrika lazima tujijue sisi nani...”
Kufuatana na hesabu
zilizofanywa mwaka 2009, Afrika inao waumini wa madhehebu ya kijadi, 137,842,
507. Linganisha idadi hiyo na Waislamu
371,459, 142 na Wakristo 304,313,880;ilhali
waumini wa dini nyingine (mathalan Wahindu) ni 9,818, 542.
Dini zinazoongoza barani ni
Wakristo na Waislamu. Maswali aliyouliza mwanamuziki Fela Kuti mwaka 1982
yanaweza kuudhi baadhi yetu tunaoamini dini hizi. Lakini bora tujiulize alikua
na malengo gani?
Ukichunguza migogoro
inayoendelea duniani sasa hivi, masuala ya mabomu na umwagaji damu yanatokana
na nguvu za wenye mali na wasio mali, maskini na matajiri. Vita vinapopiganwa
au silaha zinapotumika, anayefaidi ni mtengenezaji na muuza vifaa hivyo. Moja
ya sababu Fela Kuti alipigwa, mamake akauawa na hatimaye yeye mwenyewe kutiwa
jela (hadi alipotolewa mwaka 1986) ilikuwa kukua kwa tawala za kijeshi na
kutumia silaha kukandamiza wananchi.
Mbali na silaha zinazouziwa
magaidi na wanajeshi wanaobaka wanawake Kongo, Sudan na Somalia sasa hivi pia
yapo makampuni makubwa makubwa mfano Microsoft, Motorola, Ford na Cocacola
yanayoshirikiana na serikali za nchi maskini kuhakikisha maslahi ya makampuni haya yanaendelezwa.
Zinapotokea fujo, mapinduzi ya kijeshi,
vita nk makampuni makubwa kama Lockheed
huhakikisha silaha zinauzwa.
Mwezi Mei mwaka jana serikali
ya Marekani ilikisia dola 9.7 bilioni kila mwezi kuendesha vita vya Afghanistani.
Fedha hizi ambazo zingeweza kutumika kuleta maendeleo ya kijamii zinanunulia
silaha za sumu. Silaha hizo hizo huuzwa kwa waasi na viongozi mbalimbali Afrika
wanaoendeleza vikundi vya kigaidi sasa hivi.
Wakati hali ya uchumi duniani
ikiendelea kuwa mbaya (toka kuanza kwa tatizo la mabenki 2008) hali ya wananchi
Afrika inazidi kuharibika. Serikali mbalimbali zinaendelea kutawaliwa na
wanasiasa wasiowajali wananchi. Neno
demokrasia ambalo lilianza kutumika rasmi 1990 baada ya dhana ya vyama vingi
kuingia barani sasa hivi limechuja maana. Katika miaka minane iliyopita hali
imezidi kuwa mbaya kiasi ambacho nchi nne zimetekwa na makundi makubwa makubwa
ya Waislamu. Nchini Mali vyama vya Iyad
Ag Ghaly ( mpinzani wa serikali toka miaka ya 1980)na Ansar Dine vimechukua
theluthi mbili ya nchi hiyo baada ya mapinduzi dhidi ya serikali iliyoshinda
uchaguzi halali kupinduliwa. Sharia, itikeli na tabia zinazofanana na zile za Mataliban wa Afghanistan zimetangazwa: TV, mpira, kuvuta sigara, pombe haviruhusiwi; wezi
na wahalifu mbalimbali hukatwa mikono au
kupigwa mawe; njaa, ukosefu wa umeme na mafuta vimeshasababisha wakimbizi laki
mbili.
Mbali na mabadiliko haya
kundi hili la Matuareg (ambao walishapigana Libya mwaka jana) karibuni limeharibu
magofu ya kihistoria yaliyopo mji maarufu wa Timbuktu. Timbuktu iliyoanza kuwika sana karne ya 12 ni
mahali penye kumbukumbu zinazoweza kufananishwa na Kilwa, Zanzibar na Bagamoyo.
Uchafuzi huu una mahusiano na
Al Kaida ambayo hulka yake ni ugaidi. Mahusiano yapo vile vile Nigeria (ambapo
Boko Haram huchoma makanisa na kuharibu jamii) na Somalia (Al Shabaab). Vikundi
hivi vya magaidi vinachafua si tu sura
na wajihi wa Waislamu (Uislamu maana
yake ni amani), bali pia vinaigwa na kufuatwa hadi Tanzania ambapo karibuni
tumeshuhudia uchomaji makanisa Dar es Salaam na Unguja. Je, nini hasa kiini cha
tatizo? Je ni dini au jambo zito zaidi?
Tutathmini zaidi mada juma lijalo.
Ilishatoka gazeti la Mwananchi....
No comments:
Post a Comment