Mara ya kwanza kuvaa mkanda katika gari ilikuwa nilipopewa lifti na Mzungu mmoja miaka ya Sabini. Kipindi hicho tuliwaita weupe, walami. Sijui neno lilitokea wapi. Ila yupo jamaa aliyefasiri kuwa “mlami” ilitokana na “lami” yaani barabara safi, isiyo ya matope, makorongo, udongo au mchanga. Barabara iliyowekwa lami ikawa ya Kizungu zungu. Na enzi hizo, walami waliangaliwa kama watu walioendelea. Si tu kitabia pia kiteknolojia. Ukiwa na mlami, unaulizwa maswali. Kakupa nini? Kakupeleka wapi, mlami? Atakupeleka mtoni? Yaani, utofauti.
Kabla ya kuendelea na mada hii inayohusu magari tusisitize kuwa kila nchi niliyotembelea huwa na maneno au nahau zinazotumika kuwaita wageni. Marekani ya Kusini ni “gringo”( wanaume) na “gringa” wanawake. Kila taifa bara Ulaya huwa na matani, shutuma, majina au vigongo vya wageni.
Neno “black” lenye maana weusi saa zingine hugeuzwa kuwa “blackie” au “blackies” wingi. Wajerumani wana “auslander” (mgeni au wageni) nk. Hivyo kuwaita Wazungu walami haikuwa shutuma bali desturi ya kidunia.
Sasa nilipoingia garini nikaambiwa, nifunge mkanda. Tukabishana baadae kidogo nilipoona udhia. Mkanda ulikuwa ukinibana kiasi nilihisi tumbo linauma. Lakini miaka ilipokwenda na miye nilipoendesha magari na kuzoea mkanda (seat belt) basi yamekwisha, yakhe.
Bara Ulaya huruhusiwi kuendesha gari bila mkanda. Takwimu za ajali zenye watu wasiovalia mkanda waliofariki au kuumia sana kutokana na kukiuka sharti si ndogo. Hata tukiachilia mbali takwimu. Twa'eza toa mifano ya wanadamu, maarufu waliofariki kutokana na kutoheshimu, mikanda.
Mke wa mfalme wa Uingereza , Diana, aliyefariki Agosti 1997, ni mfano mosi. Walikuwa wanne, garini, mjini Paris. Aliyenusurika ni mmoja tu, mlinzi au askari, Trevor Rees-Jones. Inasemwa alivaa mkanda. Dereva, Henri Paul, mpenzi wake Diana, (Dodi Fayed) na Diana mwenyewe, waliofariki hawakuvaa.
Ajali nyingine ya mtu mashuhuri, ilimhusu mwanamuziki wa bendi ya wanawake watupu, TLC. TLC ilivuma miaka ya Tisini, na vibao kama Waterfall na Creep. Lisa Lopes alikuwa kwao likizo, Honduras, katika gari la abiria saba. Ilitangazwa kuwa hakuvaa mkanda. Lisa aliyejulikana kwa jina la “Left Eye” - alikuwa na umri mbichi wa miaka 30 tu.
Suala la kuvaa mikanda ni kubwa sana Majuu. Hata mabasi yanayokwenda mbali huwa na mikanda. Uvaaji mikanda husisitizwa katika magari kwa faini kwa madereva. Wiki hii tangazo la serikali kupitia polisi ,lilitoa takwimu kuhimiza kuwa asilimia 30 ya watu waliofariki katika ajali hawakuvaa mikanda. Hapo hapo hatua kali za kunyang'anywa liseni zimehimizwa. Unyang'anywaji huu hukusanya pointi au idadi za makosa mbalimbali dereva anayofanya katika kipindi.
Nyumbani bado uvaaji mikanda haujawa utamaduni wa kudumu au ulioenea., ingawa upo. Mabasi na magari yetu huwa na mikanda. Lakini ni je ni wangapi tunaozingatia utaratibu huu muhimu wa kuikinga ajali?
Ilichapishwa Mwananchi Jumapili- 6 Novemba 2022
No comments:
Post a Comment