Shangwe
zilizoenea Ulaya nzima sasa hivi ni mashindano ya soka, Brazil.
Ila wasiwasi uliowashika wanausalama wanaojua
mikunjo kunjo ya shuka na kanzu za ulimwengu wetu ni tafrani kali zinazoendelea
Syria na Iraq. Wasiwasi wa mashushushu na
wanasiasa Majuu ni hatari zitakazoenezwa na migogoro hii.
Uingereza mathalan imedai vijana 400 wazawa hapa, wanapigana Syria. Wakimaliza watarejea
na kusambaza ugaidi ulimwenguni. Vyombo kadhaa vya habari Uingereza vimeonya
jinsi mamia ya vijana wake wanavyomenyana pia Iraq, Libya, Afghanmistani, Kenya na Somali alipo mwanamke wa Kizungu anayetafutwa kuliko
fedha.
Samantha, mmoja wa wanae na mumewe gaidi aliyehusika na mauaji ya London 2005. Picha toka gazeti la Mirror
Samantha Lewthwaite, alikuwa mke wa mmoja wa magaidi wanne waliolipua mabomu na kuua
watu 51 mjini London mwaka 2005. Inadaiwa Septemba 2013, magaidi wa Al
Shabaab (walipoua 67 na kujeruhi 175), Nairobi, Mwingereza huyu mwenye watoto wanne alihusika. Inadaiwa keshasilimu (anaitwa Sherafiya) na
kuolewa na mmoja wa viongozi wakubwa wa Al Shabaab, Hassan Maalim Ibrahim. Al Shaabab maanake ni “vijana” kwa Kiarabu,
ilhali Boko Haram ni Elimu ya Kizungu ni Haram.
Mauaji ya makundi haya hufanywa kwa madai eti yanatukuza Uislamu.
Al Shabaab waliposhambulia duka la Westgate, waliwataka
mateka watongoe kanuni za Shahada katika Koran. Aliyeshindwa aliuawa. Shahada
husema “La Ilaha il Allah, Muhammad Rasulu-Ilah” ambayo maana yake “Hakuna
Mungu mwingine bali Mungu na mtume (au mtumishi) wake ni Muhammad.”
Kilugha, Shaahada (“yushaahidu”) kwa Kiarabu
ni kuangalia au kutazama, yaani “kushuhudia”, kwa Kiswahili.
Neno jingine lililotumiwa na magaidi karibuni
ni “Bakiya” (Baqiya) ambapo Isis (wauaji wa Iraq sasa hivi) iliwataka mateka
wao wakiri neno la sivyo kupigwa risasi au jambia shingoni. Bakiya ni
“kudumisha jambo” – na Kiswahili tumechukua neno “kubaki” kutokana. Bila
kuchimba sana maneno haya, shurti basi tukiri tumekitana vyema na utamaduni wa
Kiarabu, kilugha na kidini.
Kwanza kabisa,
dhana iliyoenea ni kuwa ugaidi ni
eti Uislamu.
Tuangalie Uingereza, mathalan.
Miezi mitatu iliyopita serikali ilifichua kashfa kubwa mjini Birmingham ambapo
shule 12 zilidaiwa kutekwa nyara na Waislamu. Mwanzo wa mwezi huu madai hayo
yaliyoitwa “Operation Trojan Horse” yalisema viongozi kadhaa wa Kisilamu
walikuwa na njama za kuondoa baadhi ya waalimu wakuu wa shule za Kiingereza na
kuingiza wale waliofuata nguzo na kanuni za Kiislamu. Baada ya malumbano na
vurugu (ambazo zingali zikiendelea) Waziri Mkuu David Cameron aliamuru (na pia
kuandika makala) iliyotaka shule zote Uingereza kufundisha mila na desturi za
Kiingereza na si za wageni.
Ufaransa na
nchi nyingine za Ulaya zimekataza
wanawake wa Kiislamu kuvaa Hijab. Mmoja
wa magaidi husika wa London 2005, alitoroka akivalia Hijabu, ingawa baadaye alikamatwa.
Kisheria, kila mtu anatakiwa aonyeshe
sura kwa sababu za kiusalama, nk.
Kwa hiyo ugaidi
unaoendelea duniani unahusishwa na udini kutokana na maneno na vitendo
vinavyosemwa. Kiini cha mgogoro mzima kimekita
ndani ya uchumi na siasa, yaani kutosuluhishwa ukoloni na udhalimu wanaofanyiwa
Wapalestina kwa takribani miaka 70 sasa. Toka wakoloni walipowaondoa Wapalestina na kuwapachika
Wayahudi (Israel) katika ardhi yao- mwaka 1947- nchi za Kiarabu zimeathirika.
Mstari wa mbele ilikuwa Misri iliyovamiwa na
majeshi ya Israel mwaka 1967, Syria ikatupiwa makombora 1982, nk.
Tafrani hizi zilizusha kuzaliwa
vyama vilivyokinzana na Israel
kama Hezbollah ya Lebanon. Wapalestina wenyewe wamekuwa na vyama 43 vikiwepo
Hamas na Fatah ya PLO(Palestine Liberation Organisation) iliyoundwa mwaka 1965
na hayati Yasser Arafat.
Ugaidi au
vita visivyotumia mbinu za kawaida, (yaani askari kupambana uwanjani
wakiangaliana) ulijijenga rasmi miaka ya 1970 wakati makundi ya Wapalestina
yasiyokubaliana na uongozi wa PLO, yalipoteka nyara ndege za matajiri (Wazungu
na Israel) kutangaza kilio chao. Hali
kadhalika Wapalestina waliingia ndani ya
matukio makubwa ya kimataifa kama michezo ya Olimpiki Ujerumani, 1972
wakawateka wanamichezo wa Israel na kuwaua.
Utekaji nyara huu uliitambulisha dunia tatizo
la ukoloni na udhalimu waliofanyiwa Wapalestina. Wengi duniani walifuata
kasumba iliyodai kwamba Wayahudi ni wana wa Mungu na kwamba kutawaliwa kwa Wapalestina
ilikuwa haki ya falsafa na siasa ya
Kiyahudi, inayoitwa Zionism.
Mauaji ya Sadat mwaka 1981- moja ya chimbuko muhimu sana la Ugaidi leo...picha ya Mtandaoni....
Jitihada za
amani kati ya Rais Anwar Sadat wa Misri, Menachem Begin wa Israel na
Jimmy Carter wa Marekani zilifanywa mwaka 1978 walipokutana Camp David Marekani.
Amani hiyo haikuwafurahisha wote. Oktoba 1981 Rais Sadat alipigwa risasi na Luteni Khalid Islambouli. Wakati wa kesi
Luteni Islambouli alidai sababu ya kumuua Rais Sadat ni yeye kufanya amani na Wayahudi
na Wamarekani. Hapo alihamasisha makundi ya Kiislamu yaliyofurahishwa na kifo cha Rais Sadat.
Mwaka 1982 Tanzania ilikuwa moja ya nchi
chache sana duniani zilizowatambua Wapalestina kama watu huru wenye haki ya
kujitawala. Serikali yetu ilifungua ubalozi wa Wapalestina na gari la PLO
lilipeperusha bendera yao kitaifa.
Miaka ya
Themanini ilikuwa muhimu kiharakati. Lakini hali yao haikubadilika; Wapalestina
waliendelea kudhalilishwa. Mwaka 1987, harakati mpya zilizoitwa Intifada
zilizuka hadi mwaka 1991. Intifada, Kiarabu inaimanisha “kuondoa kwa
kujikung’uta” – kama wafanyavyo mbwa au kuku wakati wakinyeshewa mvua.
Ulimwengu
ulianza kukiri tatizo na mwaka 1991 mikutano ilifanywa mjini Madrid, Hispania
na hatimaye Oslo, Norway, 1993. Makubaliano yaliyofanywa Oslo baina ya
Waisrael, PLO na baadhi ya mataifa ya Kizungu yaliweka baadhi ya misingi ya
sasa. Moja wapo ni Uongozi wa Kipalestina (Palestinian Authority). Hata baada
ya makubaliano ya Oslo, bado Wapalestina waliendelea kunyanyaswa. Mfano ni dai kwamba Yasser Arafat aliuliwa kwa sumu na
Waisraeli.
Makundi
mengi yameendelea kuudhishwa na mkondo huu wa mambo.
Miongoni ni
bwana Osama Bin Laden. Mwanzoni harakati za Bin Laden zilikuwa dhidi ya
Marekani. Aliunda Al Kaeda 1988 na akaanza kuua mwaka 1992 mjini Aden, Yemen.
Watu wawili walifariki. Bin Laden na mwasisi mwenzake wa Al Kaeda, Mamdou Salim
walitamka “Fatwa” iliyosema kuua
aliyehusika na asiyehusika imo ndani ya Kur’aani.
Marehemu
atakwenda “Jannah” penye bustani ya akhera na furaha. Hii imeandikwa katika
Sura 56 mstari 12-40 wa Kura'ani. Ni
kama Wakristo wanavyoamini kwenda mbinguni. Ikiwa ulifanya mabaya utakwenda
“Jahannam” au kwa shetani. Neno “Jahannam” limetoka Kiyahudi yaani “bonde la Hinnom”...
Aliyetenda
mabaya ataungua moto daima.
Tuendelee
kuchimba mada juma lijalo.
-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili...... Juni 22, 2014.
No comments:
Post a Comment